Friday, January 21, 2022

WAZIRI MULAMULA AZISISITIZA BALOZI KUTUMIA FURSA ZINAZOPATIKA KWA MASLAHI YA TAIFA

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula ameyasema hayo alipozungumza na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda tarehe 20 Januari 2022.

Waziri Mulamula alikutana na watumishi wa Ubalozi huo alipokuwa nchini Uganda kwa ziara ya siku mbili ambapo, pamoja na mambo mengine alishiriki Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) uliomalizika tarehe 19 Januari 2022.

“Balozi zilizopo mipakani zina fursa nyingi kiuchumi hivyo, ni muhimu  kufanya Vikao vya Ujiraini Mwema na kuendelea kuhuisha mipango kazi kila inapohitajika kufanya hivyo kwa lengo la kutatuta changamoto na kuainisha maeneo mapya ya ushirikiano”, alisema Waziri Mulamula.

Pia, akaeleza Wizara inaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha Balozi zote zinakuwa na Rasilimali zinazojitosheleza kuwezesha majukumu ya kisekta kutekelezwa kwa tija.

Vilevile akahimiza umuhimu wa kuongeza kasi ya kuzitangaza shughuli zinazofanyika sambamba na fursa mbalimbali zinazopatikana katika nchi hiyo hususani shughuli za kiuchumi ili ziweze kunufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima alieleza kuwa Ubalozi ulifanikisha kikao cha ujirani mwema kilichofanyika kati ya Tanzania na Uganda, mwaka 2017 mjini Bukoba, Kagera.

Pia, kufuatia kupungua kwa masharti ya ugonjwa wa UVIKO- 19, Ubalozi unaendelea kuratibu shughuli nyingine zenye lengo la kuhakikisha Diplomasia ya uchumi na Diplomasia ya Umma inatekelezeka kikamilifu.

Kadhalika, Waziri Mulamula alitumia ziara hiyo kutembelea mali za Ubalozi huo ikiwemo majengo na viwanja, ambapo alipata ufafanuzi juu ya maboresho yanayotarajiwa kufanyika pamoja na uanzishaji wa miradi mipya katika maeneo hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ( kati) akipokea maelezo kutoka kwa Balozi wa Tanzania Nchini Uganda, Mhe. Dkt. Aziz Mlima ( kulia ) tarehe 20 Januari 2022 jijini Kampala, Uganda. Kushoto ni maafisa wa Ubalozi huo.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.