Saturday, October 23, 2021

Dunia yatakiwa kujipanga kukabili magonjwa ya Mlipuko

Dunia yatakiwa kujipanga kukabili magonjwa ya Mlipuko

Ugonjwa wa Corona (UVIKO-19) umesababisha changamoto nyingi duniani katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, uchumi, usafirishaji, maji na utalii, hivyo dunia imetakiwa kuchukua changamoto hizo kama funzo ili kujipanga upya na namna ya kukabiliana na majanga ya mlipuko.

Hayo yemeelezwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) alipokuwa anahutubia katika sherehe za kuadhimisha Miaka 76 ya Umoja wa Mataifa (UN DAY) zilizofanyika leo jijini Dodoma kwenye viwanja vya Nyerere Square.

Dkt. Tax alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu “Kujijenga tena kwa kujenga mifumo ya afya bora” ni kielelezo cha wazi kuwa dunia haina budi kushirikiana ili kujenga mifumo madhubuti ya afya yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko. Lengo la mifumo hiyo ni kuhakikisha kuwa nchi hazipati athari kubwa zinazosababishwa na majanga kama hili la mlipuko wa UVIKO-19.

Dkt. Tax aliushukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake katika sekta mbalimbali nchini na kuuahidi umoja huo na wadau wengine wa maendeleo kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana nao katika kukabiliana na janga la Corona. Alifafanua kuwa Serikali itaendelea kufuata miongozo yote inayotolewa na Shirika la Afya Duniani pamoja na kujenga mfumo imara wa afya wenye kuhakikisha vituo bora vya afya, watumishi wa kutosha, vitendea kazi, dawa na miundombinu mingine ili kutoa huduma bora za afya nchini.

Alisema Serikali ilishaweka mikakati ya utekelezaji wa haya yote katika Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma hivi karibuni.

Alihitimisha hotuba yake kwa kuwahimiza wananchi kutumia fursa ya chanjo zilizopo nchini, kwa kuwa chanjo hizo zinapatikana kwa tabu na hadimu duniani.  

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Ziatan Milisic alisema kuwa kufanyika kwa maadhimisho hayo, inaashiria kuwa Umoja wa Mataifa una dhamira ya dhati ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama za afya, elimu mazingira ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). 

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax na wageni wengine waalikwa wakiwa wamesimama kwa ajili ya Wimbo wa Taifa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akikagua Gwaride maalum lililoandaliwa kwa heshima yake ikiwa ni moja ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akishuhudia upandishaji wa Bendera ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni moja ya tukio muhimu katika sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa.
Wanajeshi kutoka Jeshi la Wananchi walioshiriki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa wakifuatilia hotuba za viongozi akiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Dua ya kubariki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa
Dua ya kubariki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zaitan Milišić akisoma Hotuba katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa jijini Dodoma.
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Lumumba ya mjini Zanzibar wakiimba ngonjera ya kuhamasisha watu kujitokeza kwa ajili ya kupata chanjo ya UVIKO-19.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Macocha Tembele akitoa neno kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi ambaye ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuzungumza na wageni waalikwa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akihutubia mamia ya watu walioshiriki sherehe za kuadhimisha Siku ya Umojha wa Mataifa jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka akitoa neno la shukurani kufuatia sherehe za kuadhimisha Siku ya Umoja wa Mataifa kufanyika Dodoma.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akipokea cheti kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Zaitan Milišić.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari za Lumumba na Chinangali ambao waliimba ngonjera na shairi kwa ajili ya kuhamasisha chanjo ya UVIKO-19.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.