Follow by Email

Wednesday, March 13, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARITAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Prof. Kabudi kushiriki Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika

Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anatarajiwa kuondoka nchini tarehe 14 Machi, 2019 kuelekea Windhoek, Namibia kwa lengo la kuhudhuria Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya  ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 17 Machi 2019.

Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mawaziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mawaziri wa Fedha pamoja na Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama wote wa SADC. Mkutano huu utatanguliwa na Kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Machi 2019 ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe anashiriki.

Aidha, mkutano huu utajadili  masuala mbalimbali ikiwemo: Taarifa ya utekelezaji wa mipango na mikakati ya SADC; Taarifa ya Kamati ya Fedha na Kamati ya Usimamizi wa Rasilimali watu; Hatua zilizofikiwa katika mchakato wa Visiwa vya Comoro kujiunga na SADC na Mpango wa Kuanzisha Chuo cha Uhawilishwaji cha SADC (SADC University of Transformation).

Masuala mengine yatakayojadiliwa ni; Utekelezaji wa Mkakati wa Kanda wa Mawasiliano; Mabadiliko ya Kitaasisi katika Umoja wa Afrika; na Majadiliano ya Ubia Mpya Baina ya Nchi za Kundi la Afrika, Carribean na Pasifiki (ACP) na Umoja wa Ulaya (EU) baada ya mkataba wa sasa wa Cotonou kumalizika mwaka 2020.

Mhe. Prof. Kabudi ambaye ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, atatumia fursa hiyo kuendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha utangamano na ushirikiano katika Kanda na kufanya Jumuiya ya SADC kuwa chanzo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, 13 Machi 2019.No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.