Follow by Email

Saturday, March 16, 2019

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Canada nchini

Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb.), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Pamela O’Donnell, Balozi wa Canada nchini. Mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika yalifanyika kwenye ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salam tarehe 15 Machi, 2019.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria wa Tanzania na Canada ambao ulijengwa tangu enzi za Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.

Tanzania na Canada zimekuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya, biashara, uwekezaji, utawala wa Sheria pamoja na haki za binadamu.

Katika mazungumzo hayo, pamoja na mambo mengine, Mhe. Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa ushirikiano unaolenga kuleta tija katika kuinua maisha ya Watanzania.

Mhe. Dkt. Ndumbaro alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo kuhusu mafanikio ya Serikali katika kujenga uchumi na kuomba Serikali ya Canada iendelee kutoa ushirikiano kwa Tanzania kwa lengo la kuleta maendeleo zaidi kwa wananchi. Aidha, alimhakikishia  ushirikiano kutoka Wizarani ili kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa manufaa ya ushirikiano wa nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Damas D. Ndumbaro (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini, Mhe. Pamela O’Donnel. 
Mazungungumzo kati ya Mhe. Dkt. Ndumbaro na Balozi O'Donnel yakiendelea huku  Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas A. Nyamanga akifuatilia mazungumzo hayo.

 Picha ya pamoja
==================================================


...MKUTANO KATI YA KAIMU MKURUGENZI WA IDARA YA ULAYA NA AMERIKA NA BALOZI WA ITALIA NCHINI

 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Bw. Jestas A. Nyamanga amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Roberto Mengoni, Balozi wa Italia hapa nchini.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 15 Machi 2019 yalilenga katika kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na Italia hususan katika masuala ya kimataifa, utamaduni,  biashara na uwekezaji.

Aidha, walikubaliana kuimarisha ushirikiano zaidi na  kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

Bw. Nyamanga alimhakikishia Balozi huyo ushirikiano kutoka kwake na Wizara  kwa ujumla katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.


Pichani ni Bw. Jestas A. Nyamanga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika akiwa kwenye mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni

Bw. Nyamanga akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mengoni mara baada ya kumaliza mazungumzo kati yao

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.