Follow by Email

Thursday, March 28, 2019

Balozi Seif Ali Iddi akutana na Rais wa Bunge la Cuba.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Bunge la Cuba, Mhe. Esteban Lazo Harnandez, mjini Havana, Cuba.
Mhe. Harnandez kulia akipokea zawadi ya mlango wa mji Mkongwe kutoka kwa Balozi Seif kama ishara ya kufunguliwa milango ya kuitembelea Zanzibar.

 Mhe. Harnandez akimtembeza Mhe. Balozi Iddi katika sehemu mbalimbali za jengo la Bunge ya Cuba lenye historia ya muda mrefu ambazo zimewekwa kama kumbukumbu ya taifa hilo.
Mhe. Balozi  Iddi wa pili kutoka kulia na ujumbe wake akifanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya mjini Havana, Cuba.

=====================================


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amelitembelea Bunge la Cuba na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa bunge la nchi hiyo, Mhe. Esteban Lazo Harnandez.  
Katika mazungumzo baina ya viongozi hao wawili, Mhe. Harnandez ameahidi kuwa, Cuba itaendelea kudumisha ushirikiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuendeleza wananchi wake licha ya taifa hilo la Caribean kupita katika mabadiliko ya kisiasa, uchumi na utamaduni. 
Mhe. Harnandez alieleza kuwa, kutokana na mabadiliko yaliyopo sasa katika mfumo wa dunia  katika masuala ya uchumi, siasa na utamaduni Jamhuri ya Cuba imelazimika kufanya mabadiliko ya katiba yake ili yalingane na mfumo huo wa dunia inayoizunguka.
Alifafanua kuwa, tayari Bunge la Cuba limeshafanya marekebisho katika katiba yake kutoa nafasi kwa wananchi wake kuwa na uwezo na uhuru wa kumiliki nyumba, ardhi pamoja na uwepo wa waziri mkuu atakayekuwa na mamlaka ya kusimamia utendaji wa serikali.
Mhe. Harnandez alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kwamba katika vikao vya bunge hilo vinavyotarajiwa kuanza wiki ijayo baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa wabunge, serikali ya nchi hiyo itakuwa imepiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo kutokana na mabadiliko hayo.
Rais huyo wa Bunge la Cuba alisisitiza kwamba taasisi za kifedha zitalazimika kuzingatia ukusanyaji bora zaidi wa mapato katika maeneo yote ya uchumi ili kuimarisha ushiriki wa wananchi waliowengi katika mfumo huo.
Mhe. Harnandez alihitimisha kwa kumuhakikishia Balozi Seif kwamba,  uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili utaendelea kuimarishwa na kukuzwa katika muda wote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Iddi alimpongeza Mhe. Harnandez kwa kuchaguliwa tena kuliongoza bunge hilo na kueleza kuwa, hatua hiyo inaonesha wazi ishara halisi ya kukubalika vyema na wananchi wa nchi hiyo kupitia viongozi wake.
Halikadhalika, Mhe. Balozi Iddi alieleza kuwa, kwa ujumla Zanzibar itaendelea kufuatilia mabadiliko ya Cuba na kuangalia endapo inaweza kuiga mabadiliko hayo ili kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi walio wengi.
Mhe. Balozi Iddi na ujumbe wake ulihitimisha ziara yake  nchini humo kwa kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Afya ya Cuba uliokuwa ukiongozwa na Naibu Waziri, Mhe. Bibi Marcia Cobas,  katika makao makuu ya wizara hiyo yaliyopo Havana, Cuba.
Katika mazungumzo hayo ya ushirikiano wa kindugu, Balozi Iddi alisema matunda ya darasa la madaktari wazalendo waliosimamiwa na wataalamu pamoja na wahadhiri wa nchi ya Cuba yameanza kutoa matumaini.Alifafanua kuwa, kitendo cha Serikali ya Cuba kukubali kupunguza gharama kubwa ya kuwaendeleza madaktari hao wazalendo wapatao 15 katika shahada ya juu ya udaktari wa uzamili nchini humo kinaendelea kuleta faraja kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na watu wake.
Alisema wakati Zanzibar ikiendelea kutekeleza sera ya afya ya kuwa na miuondombinu ya huduma za afya katika umbali usiozidi kilomita tano kundi hilo na madaktari linaloendelea kuongezeka kila mwaka litakuwa mkombozi wa utekelezaji wa sera hiyo muhimu.
Naye Kaibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Bibi Asha Ali Abdullah, aliueleza uongozi huo wa Wizara ya Afya Cuba kwamba, hivi sasa Zanzibar  inapita katika kipindi cha kujiimarisha kwenye mapambano yake dhidi ya maradhi yasiyoambukiza.
Bibi Abdullah alisema maradhi yasiyoambukiza kama Kisukari pamoja na Shindikizo la Damu hivi sasa yamekuwa yakiathiri wananchi walio wengi na kuleta vifo vingi. Hata hivyo, jitihada zinachukuliwa ili kupunguza kasi  ya athari za maradhi hayo na kuimaliza kabisa kadhia hiyo kabisa.
Alibainisha kuwa, maradhi ya Malaria hivi  sasa yamepungua kutokana na kampeni kubwa iliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na taasisi na mataifa wahisani katika kuangamiza vilui lui vya maradhi hayo.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alimuhakikishia Naibu Waziri wa Afya wa Cuba kwamba ushauri wote walioupata katika ziara yao kwenye taasisi za Afya nchini Cuba likiwemo suala la upatikanaji wa dawa litazingatiwa na iwapo linaweza kuleta afueni ya gharama kwa Zanzibar litachukuliwa hatua mara moja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.