Follow by Email

Tuesday, November 6, 2018

TAARIFA YA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA MISRI,
TAARIFA YA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATI YA TANZANIA NA MISRI, 
Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Misri limefunguliwa leo katika hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam. Kongamano hilo limeandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Misri hapa nchini chini ya uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wafanyabiashara na wawekezaji wapatao 35 kutoka Misri wameshiriki kwenye Kongamano hilo kwa lengo la kutafuta  fursa katika sekta za kilimo, mifugo, viwanda, madini na ujenzi.

Mgeni rasmi katika Kongamano hilo alikuwa ni Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mahiga aliwakaribisha wafanyabiashara hao kuja kuwekeza nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo, madini na utalii. Aidha, Waziri Mahiga alisifia mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Misri na juhudi za Serikali ya Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya biashara hapa nchini ili kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji.

Kongamano hilo linafanyika leo na kesho na linaenda sambamba na mikutano ya ana kwa ana (B2B) kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Misri kwa lengo la kuangalia fursa mbalimbali zitakazowezesha kuanzishwa kwa ushirikiano katika Nyanja za biashara na uwekezaji. Aidha kesho kuna mikutano kati ya taasisi za serikali na wafanyabiashara hao (B2G). Taasisi zinazotarajiwa kutoa mada ni TIC, Tanzania Food and Drug Authority (TFDA) na Tanzania Bureau of Standard (TBS).

Ujumbe huo wa wafanyabiashara utaelekea Zanzibar tarehe 08 Novemba 2018 kwa ajili ya kushiriki kwenye Kongamano katika hoteli ya Hyatt Park, Zanzibar tarehe 09 Novemba, 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.