Follow by Email

Saturday, August 11, 2018

Wizara ya Mambo ya Nje yahamasisha uwekezaji katika sekta ya Kilimo na Mifugo


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amefanya mazungumzo na kampuni ya Burmeister & Partiners  (PTY) LTD ya nchini Namibia tarehe 10 Agosti 2018 mjini Windhoek, Namibia.

Akiongea na uongozi wa kampuni hiyo Prof. Mkenda alieleza Tanzania ina eneo kubwa la ardhi yenye rutuba  ambayo haitumiki na rasilimali watu ya kutosha hivyo ni fursa kwa mwekezaji mwenye nia thabiti kuwekeza nchini.

“Lengo la Serikali ni kupata mwekezaji aliye makini kama wewe nimeona una mradi mkubwa wa shamba la mifugo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya machinjio nina imani ukija kuwekeza Tanzania hautajutia kabisa kwakuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika miradi itaongeza thamani ya mazao na bidhaa zitakazozalishwa na kuwezesha kupatikana kwa soko la kimataifa” alisema Prof. Mkenda

Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Mhandisi Hendrik Boshoff alieleza  kampuni imekuwa ikifanya kazi katika mataifa mbalimbali ambapo kampuni hiyo imefungua kampuni ya maziwa nchini Rwanda ambayo inauza na kusafirisha mataifa mengine pia imewekeza nchini Angola katika miradi ya uvuvi na imekuwa ikifanya vizuri katika biashara zake zote.

Pia alisema kampuni imebobea katika miradi ya ujenzi, nishati, miradi ya maji, usafiri, usanifu majengo, ujenzi wa majengo, miradi ya machinjio, mashamba ya mifugo na pia ipo katika mpango wa kuanzisha miradi ya viwanda vya dawa za binadamu ambapo utekelezaji wake utaanza mara baada ya kukamilisha mazungumzo na wataalamu kutoka nchini Cuba.

Prof. Mkenda alieleza miradi yote kutoka katika kampuni hiyo inatija kubwa kwa maendeleo ya taifa la Tanzania hivyo akaikaribisha kampuni hiyo kuja mapema nchini ili kuweza kujionea rasilimali zilizopo na kuainisha miradi watakayoweza kuanza nayo. Vilevile akaeleza  kampuni hiyo ina nafasi ya kutumia fursa za mji wa Dodoma katika uwekezaji kufuatia kuhama kwa mji wa Serikali kutoka Dar es Salaam.

Kampuni ya Burmeisters & Partiners (PTY) LTD ilianza kufanya kazi zake nchini Namibia mwaka 1984 na baadae kuwa miongoni mwa kampuni kubwa zilizowekeza nchini humo. Pia ni kampuni  hiyo inatoa huduma za  kihandisi na huduma za usimamizi wa miradi katika taaluma mbalimbali.


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda(kulia) akizungumza na mwakilishi wa kampuni ya Burmeister and Partners (PTY) LTD alipowatembela katika ofisi za kampuni hiyo iliyopo Windhoek, Namibia tarehe 10 Agosti 2018. Kulia kwa Katibu Mkuu ni  wajumbe walioambatana naye katika ziara hiyo, Mratibu wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa katika Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo Tanzania, Bi. Magreth Ndaba, Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika Mashariki , Bw. James Lugaganya na Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Sylivester Ambokile.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Burmeister & Partners (PYT) LTD, Mhandisi Hendrik Boshoff akielezea usanifu wa miradi mbalimbali unaofanywa na kampuni ya Burmeister & patners (PTY) LTD.

Sehemu ya ofisi iliyosanifiwa na kampuni hiyo.

Mazungumzo yakiendelea.

Mwakilishi kutoka kampuni hiyo akiwasilisha miradi mbalimbali iliyosanifiwa na kampuni ya Burmeister & Partners (PTY) LTD

Prof. Mkenda akifafanua tunu na rasilimali zilizopo nchini ambazo ni fursa kwa uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.