Follow by Email

Thursday, August 9, 2018

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)

Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (The 38th Ordinary of the SADC Summit of Heads of State and Government) utafanyika tarehe 17-18 Agosti, 2018.

Mkutano huu utatanguliwa na mikutano ifuatayo;

(i)            Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security) utakaofanyika tarehe 16 Agosti 2018 ambao utapitia na kujadili hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda kwa kipindi cha Agosti 2017 hadi Agosti 2018. Mkutano huu utahusisha nchi tatu za SADC Organ TROIKA na wajumbe wake ambao ni Angola (Mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama), Zambia (Makamu Mwenyekiti wa Organ) na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mwenyekiti wa Organ aliyemaliza muda wa uenyekiti wa Asasi).

(ii)           Mkutano wa Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14 Agosti 2018 pamoja; na

(iii)         Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika utakaofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 11Agosti 2018.

Prof Adolf Mkenda, Katibu Mkuu, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anaonagoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Makatibu Wakuu akisaidiana  na Eng. Joseph Nyamhanga, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ( Ujenzi), Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango. Mhe Augustine Mahiga (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ataongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utapokea, kujadili na kutolea maamuzi ya mapendekezo mbalimbali yanayotokana na mikutano ya kisekta na kamati za jumuiya kwa kipindi cha mwaka 2017/18. Pamoja na mambo mengine mkutano huu;

1.    Utafanya uteuzi wa Mwenyekiti wa SADC na inatarajiwa kuwa Jamhuri ya  Namibia ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa  Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha 2018/2019. Nafasi ya Makamu mwenyekiti itajazwa pia na nchi itakayoteuliwa itajulikana tarehe 17Agosti 2018


2.    Uteuzi wa Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC. Inatarajiwa kuwa Jamhuri ya Zambia, ambayo ni Makamu Mwenyekiti wa sasa itateuliwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha 2018/2019. Hivi sasa Tanzania ni Mwenyekiti anayemaliza muda wake kwenye Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ on Politics, Defence and Security)

3.    Maeneo mengine yanayotarajiwa kujitokeza na kujadiliwa katika mkutano huu ni haya yafuatayo

(i)            masuala ya fedha;
(ii)           Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Viwanda wa SADC ( Report on the operaionazaition Maendeleo ya viwanda;
(iii)         Kutia saini itifaki mbalimbali ikiwa ni pamoja na tifaki ya Kulinda Hakimiliki ya Wagunduzi wa aina Mpya za Mbegu za Mimea ya mwaka 2017.

(iv)         Pia Mkutano huu utatoka na Tamko la nchi wanachama wa SADC la kutokomeza malaria katika ukanda wa SADC ifikapo mwaka 2030. 
=======================================================


Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), Dkt. Stergomena L. Tax  (kushoto) akishuhudia makabidhiano ya uongozi katika nafasi ya Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa SADC baina ya mwenyekiti anayemaliza muda wake, Bw. K E Mahoai Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Mwenyekiti mpya, Balozi Selma Ashipala-Musavya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Namibia.
Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC uliofanyika katika Hoteli ya Safari Mjini Windhoek, Namibia tarehe 09 Agosti 2018. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda (kati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu(kushoto)  na Mkurugenzi wa Idara ya ushirikiano wa Kikanda (kulia), Balozi Innocent Shiyo wakifuatilia majadiliano wakati wa mkutano wa Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

Mwenyekiti wa Makatibu Wakuu wa SADC,Balozi Selma Ashipala-Musavyi akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano huo ambapo aliwashukuru wajumbe kwa kuwa na imani naye na kumpa jukumu hilo na pia alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha anashirikiana na wanachama kusimamia suala la ulinzi na usalama linapatikana ndani ya jumuiya ili kuruhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Bw. K E Mahoai akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa mkutano mara baada ya kukabidhi nafasi ya uenyekiti ambapo aliwashukuru wajumbe kwa ushirikiano alioupata wakati wa uongozi huo kwa taifa lake. 

Wajumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania ikifuatilia majadiliano katika mkutano wa Makatibu Wakuu wa SADC.

Picha ya pamoja Katibu Mkuu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stergomena L. Tax (wa nne kutoka kushoto) na Makatibu Wakuu wa Jumuiya hiyo Mjini Windhoek, Namibia.
  

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.