Follow by Email

Monday, July 23, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA MHE. MKAPA NCHINI MSUMBIJI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARITAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mkutano wa Pili wa Chama Tawala cha Msumbiji FRELIMO yatafanyika katika Jimbo la Niassa nchini Msumbiji tarehe 25 Julai 2018. Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi alimwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kushiriki maadhimisho hayo. Kutokana na majukumu mengine ya kitaifa Mhe. Rais Magufuli hatoweza kushiriki. Hivyo, kwa kuona umuhimu wa mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji na umuhimu wa maadhimisho hayo kwa historia ya nchi hizi mbili, amemteua Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa amwakilishe kwenye sherehe hizo na ataambatana na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (Bara), Mhe. Philip Mangula.

Mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji

Mahusiano kati ya Tanzania na Msumbiji ni mazuri na yamekuwa yakiimarika kila wakati. Mahusiano kati ya nchi hizi yalianza enzi za harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Kireno nchini Msumbiji. Mahusiano hayo yalijengwa na waanzilishi wa mataifa haya mawili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Moises Machel na yameendelea kuwa mazuri siku hadi siku na kuendelezwa na Viongozi wote Wakuu waliofuata wa nchi hizi mbili.  Ziara za Viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali na vyama tawala vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na FRELIMO wameendelea kutembeleana na kudumisha uhusiano huo.

Ushirikiano katika Chuo cha Diplomasia (Mozambique - Tanzania Centre for Foreign Relations (CFR)

Chuo cha Diplomasia (Mozambique-Tanzania Centre for Foreign Relations – CFR) kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam  ni moja ya alama muhimu za ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji. Chuo cha Diplomasia kilianzishwa mwaka 1978, kwa makubaliano ya nchi za Tanzania na Mozambique. Chuo hichi kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Mambo ya Nje kutoka katika nchi hizi mbili katika taaluma ya Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia.

Awali, kabla ya kubadilishwa kuwa Chuo cha Diplomasia, ilikuwa ni kituo cha harakati za kupigania uhuru wa Msumbiji. Hivyo, katika harakati za Ukombozi kutoka kwa wakoloni, wapigania uhuru wa kutoka Msumbiji wakiongozwa na Hayati Eduardo Mondlane waliweka kambi chuoni hapo na kuanzisha chama cha Ukombozi cha FRELIMO mnamo mwaka 1962. Mwaka 1970 Hayati Samora Machel alishika madaraka ya kukiongoza chama hicho baada ya kuuawa kwa Mhe. Mondlane

Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara

Tanzania na Msumbiji zimeendelea kushirikiana katika masuala ya kiuchumi na biashara kwa kuzingatia ujirani na muingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili, hususan  katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara kwa upande wa Tanzania, na Majimbo ya Niassa na Cabo Delgado kwa upande wa Msumbiji.  Tanzania na Msumbiji zinauziana bidhaa mbalimbali za kilimo na viwandani.

Kadhalika kuna Makampuni makubwa kadhaa ya Kitanzania yaliyowekeza mitaji mikubwa nchini Msumbiji.  Vile vile, wapo Watanzania wanaomiliki makampuni ya usafirishaji wa abiria na biashara za kati na ndogo. Ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na misingi imara ya kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizi mbili, Tanzania na Msumbiji ziliamua kujenga Daraja la Umoja linaloziunganisha nchi hizo kwenye mpaka wa Mto Ruvuma ili kuboresha na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi.

Mhe. Mkapa na Ujumbe wake wanatarajia kuondoka nchini tarehe 24 Julai, 2018 na kurejea tarehe 26 Julai, 2018.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma.
23 Julai 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.