Follow by Email

Wednesday, April 25, 2018

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA RAIS WA BENKI YA AfDB NCHINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika nchini
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina atafanya ziara ya siku nne (4) nchini kuanzia tarehe 25 hadi 28 Aprili, 2018 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Lengo la ziara ya Dkt. Adesina nchini ni kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya miradi ya miundombinu nchini.
Akiwa nchini, Mhe. Dkt. Adesina ataonana kwa mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Magufuli pamoja na kuzindua Barabara kutoka Dodoma kwenda Babati hafla itakayofanyika katika eneo la Mradi wa Barabara wa Mayamaya-Mela-Bonga Wilayani Kondoa.
Aidha, Dkt. Adesina atatembelea Mtambo wa Kusafirisha Umeme wa Iringa kwenda Shinyanga pamoja na Kituo Kidogo cha Umeme cha Zuzu cha Mkoani Dodoma.
Dkt. Adesina ambaye ameambatana na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anatarajiwa kushiriki Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Mkoani Dodoma tarehe 26 Aprili, 2018.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza kwa kupokea misaada kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF). Aidha, tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa nchini mwaka 1971, Tanzania imenufaika kwa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani bilioni 3.5 huku miradi ya maendeleo ya miundombinu ikipewa kipaumbele.
Aidha, hadi kufikia mwezi Novemba 2017 Benki ya Maendeleo ya Afrika imekuwa ikitekeleza miradi 25 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.9. Kati ya miradi hiyo, 22 ni ya Sekta ya Umma yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 huku miradi mitatu (3) ikiwa chini ya Sekta Binafsi kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 187.0.
Kati ya miradi yote, miradi ya maendeleo ya miundombinu inachukua asilimia 73 ambapo kati yake miradi ya Barabara ni asilimia 51, Maji na Usafi wa Mazingira asilimia 12 na Nishati asilimia 10. Asilimia 27 zilizosalia zinasaidia miradi ya sekta binafsi hususan katika kilimo na ustawi wa jamii.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 24 Aprili, 2018
-Mwisho-
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.