Follow by Email

Friday, April 13, 2018

Balozi Luvanda awasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Sri Lanka

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda (kushoto) ambaye anawakilisha pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka akiwasilisha Hati za Utambulisho kwa Mheshimiwa Maithripala SIRISENA, Rais wa nchi hiyo.

Balozi Luvanda akisalimiana na maafisa waandanizi wa Ikulu ya Sri Lanka 
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda aliwasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka, Mheshimiwa Maithripala SIRISENA.

Hii ni hatua muhimu katika kuendeleza, kuimarisha na kukuza uhusiano wa kirafiki na ushirikiano mwema uliopo kati ya Tanzania na Sri Lanka ambao ulianza mnamo miaka ya tisini. Wakati huo, Sri Lanka ilikuwa inawakilishwa nchini Tanzania kupitia Ubalozi wake wa mjini Kampala, Uganda ambao baadaye ulifungwa na Tanzania ikiwakilishwa nchini Sri Lanka kupitia Ubalozi wake wa New Delhi. Kwa sasa Sri Lanka inakusudia kumteua Balozi wake mjini Nairobi ambaye pia ataiwakilisha nchi hiyo nchini Tanzania.

Katika hafla hiyo, Balozi Luvanda aliambatana na Mwambata Jeshi wa Tanzania nchini India, Col. Amri Salim MWAMI. Aidha, Balozi Luvanda alifanya mazungumzo na Mkuu wa Itifaki wa Sri Lanka pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya Afrika, ambapo ameahidi kushirikiana kwa karibu na watendaji hao katika kudumisha uhusiano uliopo kati ya nchi hizi mbili na ambao utazinufaisha zaidi, hususan katika kuhakikisha uhaulishaji wa uzoefu, teknolojia na utaalam wa Sri Lanka kwa Tanzania kwenye sekta ya viwanda vya nguo, madini na vito mbali mbali na kilimo.

Sri Lanka ni nchi yenye uchumi unaoendelea ingawa imepitia kipindi kigumu cha vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa takriban miaka 25, vita ambavyo vilimalizika mwaka 2009.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.