Follow by Email

Thursday, March 22, 2018

Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israeli


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Waziri Mahiga afanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Israeli

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli Mhe. Avigdor Liberman. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kupokelea wageni maalum(VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere,Jijini Dar es Salaam, tarehe 22 Machi,2018.

Mazungumzo haya yalijikita zaidi katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Israeli. Akiongea katika mazungumzo hayo Waziri Mahiga alisema ziara hii ina maana kubwa sana kwa Tanzania na itazidi kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizi mbili. Kama inavyofahamika nchi ya Israeli ina Utaalam wa hali ya juu  katika maeneo mbalimbali hasa katika masuala ya Ulinzi na Usalama, Kilimo cha Umwagiliaji, mbinu za kisasa za kupambana na Ugaidi, Uhalifu wa Kimtandao na Teknolojia ya tiba na vifaa tiba.

"Tunatarajia Tanzania kunufaika zaidi  na Utaalam huu hasa katika maeneo ya mbinu za Kilimo bora cha umwagiliaji, Teknolojia ya tiba na vifaa tiba, mbinu za kupambana na Ugaidi, Ulinzi wa Mipaka na Uharamia, Biashara na Ushirikiano wa Teknologia na mafunzo mbalimbali ya kujenga uwezo wa Wataalam wa Tanzania hasa katika Sekta ya Viwanda, Afya na Kilimo" alisema Waziri Mahiga.

Naye Mhe. Liberman amesema Israeli inaishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kulinda Amani ya Dunia hasa kwa kushiriki katika Ulinzi wa amani nchini Lebanon na nchi nyingine za afrika zenye migogoro, na ameahidi nchi yake  itaendelea kuongeza maeneo ya Mashirikiano zaidi na Tanzania. 

Katika Ziara hii Mhe. Liberman alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mhe. Liberman ameondoka tarehe 22 Machi, 2018, kurejea nchini Israeli baada ya Ziara ya siku tatu(3) hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo kwa Waziri wa Ulinzi wa Taifa la Israeli ambaye pia ni Naibu Waziri wa Taifa hilo Mhe. Avigdor Liberman walipokutana kwa mazungumzo tarehe 22 Machi,2018, mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa kupokelea wageni Maalum(VIP) Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mashariki ya Kati Bw. Ayoub Mdeme na Bi. KisaDoris Mwaseba wakifuatilia mazungumzo hayo
Balozi wa Israeli nchini, ambaye Makazi yake yapo Jijini Nairobi Mhe. Balozi Noah Gal Gendler na Msaidizi wa Viongozi wakiwa katika mazungumzo hayo.
Waziri Mahiga akiagana na Mhe. Liberman baada ya kumaliza mazungumzo, 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.