Follow by Email

Sunday, January 14, 2018

Mawaziri wa Tanzania na Rwanda kujadili Ujenzi wa Reli

Mawaziri wa Tanzania na Rwanda wanaoshughulikia masuala ya miundombinu wameagizwa kukutana mara moja kujadili ujenzi wa Reli ya kiwango cha Kimataifa kutoka Isaka hadi Rwanda. 

Kauli hiyo imetolewa leo Ikulu jijini Dar Es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mbele ya waandishi wa habari akiwa na mgeni wake, Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame ambaye amefanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini. 

“Kipande cha kutoka Isaka hadi Rwanda ni kilomita 400 tu, hatuwezi kushindwa kukijenga, tumewaagiza Mawaziri wa miundombinu wakutane ili wajadili namna ya kupata fedha na kabla mwaka huu haujaisha tunataka kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo”, Rais Magufuli alisema.

Rais Magufuli alieleza kuwa ujenzi wa reli hiyo utasaidia kukuza biashara kati ya Tanzania na Rwanda ambayo kwa sasa, licha ya kuongezeka kidogo lakini kiwango cha biashara kati ya nchi hizo bado kipo chini, akitolea mfano wa kuongezeka kwa mizigo ya Rwanda inayopitia Bandari ya Dar Es Salaam ambayo kwa mwaka jana imefikia idadi ya tani laki tisa na nusu.

Rais Magufuli ambaye alimtaja Rais Kagame kuwa ni mwanamapinduzi wa Afrika, licha ya kumpongeza kwa kushinda kiti cha Rais kwa ushindi wa kishindo mwaka 2017 alimsifu pia kutokana na mipango yake ya kuibadilisha Rwanda na dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wa nchi hiyo. “Watanzania na watu wengine wanajua Rwanda ilipotoka na hatua ulioifikisha hivi sasa”, Rais Magufuli alisema.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alimuhakikishia Rais Kagame anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa kipindi cha Mwaka 2018 kuwa Tanzania pamoja na marafiki zake itamuunga mkono kwenye nafasi hiyo. Mhe. Rais alielezea matumaini yake kuwa Rais Kagame atatumia nafasi yake hiyo kwa kushirikiana na viongozi wenzake kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazolikabili Bara la Afrika ikwemo ukosefu wa ajira unaosabisha vijana wengi kukimbia nchi zao. 

Kwa upande wake, Rais Kagame alielezea matumaini yake kuwa Tanznaia itaendelea kushirikiana na Rwanda katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili. 

Akijibu swali kuhusu hatua gani atazichukuwa atakapokuwa Mwenyekiti wa AU kukabiliana na wimbi la vijana wengi wa Afrika kukimbilia ughaibuni kutafuta maisha.

Rais Kagame alijibu kuwa nchi moja moja na kwa ujumla wao barani Afrika ziongeze biashara na uwekezaji baina yao ili kuongeza ajira kwa vijana. Aidha, aliwaasa vijana kuwa jukumu la Serikali zote duniani ni kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara, hivyo vijana hawanabudi kutumia fursa zinazopatikana katika nchi zao badala ya kukimbilia ughaibuni na kutangatanga. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
14 Janauri 2018
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Baadhi ya viongozi wa Serikali mara baada ya kuwasilia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe.Paul Kagame aliyefanya ziara ya kikazi ya siku moja leo Jijini Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame akishuka kutoka katika ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terminal I leo Jijini Dar es Salaam. Rais Kagame amefanya ziara ya kikazi ya siku moja. Baadhi ya wananchi wakimlaki Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame mara baada ya kupokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Dkt. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo Jijini Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kulia) akimkaribisha mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame Ikulu Jijini Dar es Dar es Salaam leo. Rais Kagame amekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam kuelezea masuala waliojadili na mgeni wake Rais Kagame. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu mazungumzo baina yake na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame (kushoto) leo Ikulu Jijini Dar es Dar es Salaam. Rais Kagame amekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu mazungumzo baina yake na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli (kulia) leo Ikulu Jijini Dar es Dar es Salaam. Rais Kagame amekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Baadhi ya Viongozi wa Serikali waliokuwa Ikulu kushiriki katika ziara ya Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame. Baadhi ya viongozi wakifuatilia mkutano wa Marais Dkt. John Pombe Magufuli wa Tanzania na Mhe. Paul Kagame wa Rwanda mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu Jijini Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mikono na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe. Paul Kagame leo Ikulu Jijini Dar es Dar es Salaam. Rais Kagame amekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.