Follow by Email

Friday, February 24, 2017

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje azungumza na Balozi wa Sweden nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima akizungumza na Balozi wa Sweden hapa nchini, Mhe. Katarina Rangnitt. Katika mazungumzo yao walijadili namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden. Mazungumzo hayo yalifanyika Wizarani tarehe 24 Februari, 2017
Balozi Rangnitt nae akimweleza jambo Balozi Mlima wakati wa mazungumzo yao
Mazungumzo yakiendelea. Kulia ni Bi. Tunsume Mwangolombe, Afisa Mambo ya Nje na kushoto ni Afisa kutoka Ubalozi wa Sweden.
Balozi Mlima akimpatia Balozi Rangnitt kadi yake ya mawasiliano ikiwa na  anuani mpya za Dodoma.

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Samwel Shelukindo awasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Rais François Hollande jijini Paris leo


Mheshimiwa Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa akiwasilisha Hati zake za Utambulisho kwa Mheshimiwa François Hollande, Rais wa Jamhuri ya Ufaransa leo tarehe 23 Februari, 2017, Ikulu ya Ufaransa. Katikati ni Mheshimiwa Jean Marc Ayrault, Waziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa wa Ufaransa
Balozi Shelukindo akiwa kwenye mazungumzo rasmi na Mheshimiwa Rais François Hollande baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho.
Balozi Shelukindo na Mheshimiwa Hollande wakiendelea na mazungumzo kwenye Ikulu ya Ufaransa. Kulia kwa Mheshimiwa Hollande ni Waziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa ya Ufaransa, Mheshimiwa Jean-Marc Ayrault na kulia kwa Balozi Shelukindo ni Bwana Stephen Wambura, Afisa Mambo ya Nje Mkuu na Kaimu Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania mjini Paris.
Balozi Shelukindo akiagana na Mhe. Rais Hollande wa Ufaransa, baada ya kuwasilisha hati za utambulisho kwenye Ikulu ya nchi hiyo leo tarehe 23 Februari, 2017Thursday, February 23, 2017

Rais wa Uganda kufanya ziara ya siku mbili nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ziara ya siku mbili ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni atakayoifanya hapa nchini tarehe 25 na 26 Februari, 2017.Kulia ni Balozi Innocent Shiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na kushoto ni Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizarani.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleimani Seleh (wa kwanza kushoto) akifuatilia kwa makini mkutano wa waandishi wa habari na Waziri Mahiga.Kulia ni sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo.
Juu na chini ni sehemu ya waandishi wa habari wakiendelea kumsikiliza Waziri Mahiga (hayupo pichani) .
Mkutano na Waandishi wa habari ukiendelea 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 


Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uganda nchini


Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 25 na 26 Februari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Mhe. Rais Museveni anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 25 Februari, 2017 majira ya asubuhi  na atapokelewa na Mhe. Dkt Magufuli pamoja na Viongozi wengine wa Serikali. 

Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uganda na Tanzania pamoja ‎na kujadili masuala mbalimbali ya kikanda, kimataifa na maeneo ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan katika maeneo ya Biashara, Nishati, Uchukuzi na yale yanayohusu ujirani mwema.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Museveni  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. 

Pia, Mhe. Rais Museveni na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Siku ya pili, tarehe 26 Februari, 2017, Mhe. Rais Museveni atatembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Viwanda vya Kampuni ya Said Salim Bakhresa ambaye amewekeza pia nchini Uganda na baadaye Bandari ya Dar es Salaam.

Mahusiano ya Uganda na Tanzania

Mahusiano ya Tanzania na Uganda ni mazuri na yamekuwa yakiimarika kila mara. Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa ukaribu sana katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisisasa, kiusalama, kijamii na kikanda hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia kumekuwepo ziara za mara kwa mara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais Uganda, Mhe. Museveni ambaye alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi Novemba, 2015. Aidha, Rais Magufuli pia alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Rais Museveni mwezi Mei, 2016.

Mahusiano katika Sekta ya Biashara

Mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Uganda yameendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni. Katika kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa ni mazuri ambapo Tanzania iliweza kufanya mauzo (exports) ya kiasi cha Shilingi bilioni 126.744 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 99.882 mwaka 2015. Mauzo ya Uganda nchini Tanzania (imports) kwa mwaka 2016 yalikuwa ni Shilingi bilioni 66.849 bilioni ikilinganishwa na Shilingi 78.31 mwaka 2015.

Aidha, nchi ya Uganda ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kutokana na jiografia yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa nchi jirani tunayopakana nayo. Uganda ni nchi isiyokuwa na bandari (landlinked country) hivyo inaitegemea Tanzania kwa ajili ya kupitisha mizigo yake. 

Nchi hiyo imezidi kuwa na umuhimu kufuatia uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta nchini Tanzania, kutoka Kabaale-Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga. Bomba hili litakuwa na urefu wa kilomita 1443 na kipenyo cha inchi 24. Mradi wa ujenzi wa Bomba hili unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020.

Utekelezaji wa mradi huu unategemewa kuwa na faida nyingi kwa taifa ikiwemo kufungua fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea shughuli za kiuchumi kwa mikoa bomba hilo litakapopita,  kufungua ukanda wa biashara wa kaskazini mwa Tanzania na Uganda  na kuimarisha uhusiano katika soko la Afrika Masahariki.

 Ushirikiano kupitia Tume ya pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Uganda

Mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda ulisainiwa Kampala, Uganda tarehe 13 Machi, 2007. Mkataba huo unaainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano ambayo yalipaswa kutekelezwa kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC). Maeneo yaliyoainishwa ni pamoja na Miundombinu, Viwanda, Biashara, uwekezaji, Nishati, Utalii, Kilimo, Uvuvi, Mazingira, Ulinzi na Usalama.

Ushirikiano katika jitihada za usuluhishi wa Mgogoro wa Burundi

Jitihada za usuluhishi wa mgogoro nchini Burundi zinaendelea vizuri. Mhe. Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa usuluhishi wa mgogoro huo kwa kushirikiana na Rais Msataafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni Mwezeshaji wa mazungumzo ya upatanishi wamekuwa wakifanya jitihada za dhati za kurejesha amani nchini Burundi. 

Mhe. Rais Museveni na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini tarehe 26 Februari, 2017.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 23 Februari, 2017
 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana na Mjumbe Maalum wa Mto Nile kutoka Ujerumani


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba akiwa kwenye mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Mto Nile kutoka Ujerumani. Balozi Rolf Welberts (kushoto). Katika mazungumzo yao Balozi Welbert alimwelezea Dkt. Kolimba dhumuni la kuhakikisha Maji ya Mto Nile yanatumiwa  kwa amani na nchi zote zinazopitiwa na mto huo.Mkutano huo umefanyika Wizarani Jijini Dar es Salaam.Sehemu ya Maafisa Mambo ya Nje wakifuatilia mazungumzo kati ya Dkt. Kolimba na Balozi Welbert
Mazungumzo yakiendelea
Naibu Waziri, Dkt. Susan Kolimba akiagana na Balozi Welbert mara baada ya kumaliza mazungumzo naye.

Wednesday, February 22, 2017

Waziri Mahiga apokea ujumbe wa Mhe. Rais kutoka kwa Mfalme wa Qatar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea ujumbe wa Mfalme wa Qatar, Mtukufu Sheikh Tamim Hamad Bin Khalifa Al-Thani kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ujumbe huo uliwasilishwa leo katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam na Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Abdullah Jassim Al Maadadi.
Waziri Mahiga akizungumza na Mhe. Jassim Al Maadadi ambapo pamoja na kuzungumzia masuala ya ushirikiano Waziri alimpongeza kwa hatua nzuri za maandalizi ya Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika nchini Qatar mwaka 2022. Vilevile alimuarifu kuhusu hatua iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kukamilisha ufunguzi wa Ofisi za Ubalozi mjini Doha, Qatar.


Mhe. Jassim Al Maadadi alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania kuzichangamkia fursa za ajira zilizopo nchini Qatar wakati huu wa maandalizi ya Kombe la Dunia kwa kuwa nchi hizi zilikwisha saini mkataba wa ushirikiano kwenye kazi na ajira mwaka 2013.
Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga, Afisa Mambo ya Nje, Bw. Hangi Mgaka na Katibu wa Waziri, Bw. Gerald Mbwafu wakifuatilia mazungumzo.
Mazungumzo yakiendelea
Picha ya pamoja.

Waziri Mahiga akutana na Mkurugenzi wa UNDP nchini


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Hawa Dabo alipomtembelea leo katika Ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mahiga akiendela na mazungumzo na Bi. Gabo huku Bi. Ngusekela Nyerere (kulia), Afisa Mambo ya Nje akinukuu.

Tuesday, February 21, 2017

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje afungua kikao cha Makatibu Wakuu wa SADC-ISPDC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz P. Mlima, akifungua Mkutano cha Makatibu Wakuu nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Kamati Ndogo ya Mawaziri ya Siasa na Diplomasia ya SADC (Inter State Politics and Diplomacy Sub Committee-ISPDC) unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 na 24 Februari, 2017. Mkutano wa Makatibu Wakuu unafanyika kwa siku mbili  katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wajumbe wa Mkutano kutoka katika mataifa ya nchi wanachama wakifuatilia mkutano.
Kaimu Mkuu wa Mabalozi Mhe. Balozi Edzai Chimonyo (wa kwanza kushoto) na wajumbe wengine wakifuatilia mkutano.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Stergomena Tax (wa pili kushoto)  na wa kwanza kulia ni Balozi Simba Yahya, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakifuatilia mkutano.

Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano.

Monday, February 20, 2017

Balozi wa Tanzania nchini Comoro aagwa kwa kutunikiwa Tuzo na Rais

Balozi wa Tanzania kwenye Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Chabaka Kilumanga akitunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Azali Assoumani hivi karibuni.

Nishani hiyo imetolewa na Mhe Azali  kwa kutambua mchango wa Balozi Kilumanga katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Hafla hiyo ilifanyika Ikulu ya Comoro kwa ajili ya kumuaga Balozi Kilumanga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini humo

Mhe. Rais Azali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Kilumanga na Mkewe
Balozi Kilumanga akipongezwa na Mkuu wa Utawala Ubalozini, Bw. Mudrick Soragha mara baada ya kutunikiwa nishani na Rais wa Comoro
============================================

BALOZI WA TANZANIA VISIWANI COMORO ATUNUKIWA MEDANI YA JUU YA HESHIMA NA MHE. AZALI ASSOUMANI, RAIS WA MUUNGANO WA VISIWA VYA COMORO TAREHE 16 FEBRUARI 2017

Balozi wa Tanzania ndani ya Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Chabaka Kilumanga ametunukiwa Nishani ya Juu (highest civilian honor) na Rais wa nchi hiyo Mhe. Azali Assoumani. Mhe. Balozi ambaye aliongozana na Mkewe Bi Irene Kilumanga walishiriki katika hafla hiyo iliyofanyika Bait Salam, Ikulu ya Comoro tarehe 16, Februari 2017. Wageni waalikwa walioshuhudia  hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro,  Mhe. Baccar Dossar na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Comoro Mhe. Yousef Mohamed Yousef.

Hafla hiyo ilifanyika ikiwa ni sehemu ya sherehe ya kumuaga Balozi huyo ambaye amemaliza muda wake wa kazi Visiwani Comoro na kuelekea kustaaafu ifikapo tarehe 17 Machi, 2017. Mhe. Chabaka Kilumanga anakuwa ndio Balozi wa mwanzo kutunukiwa nishani hiyo miongoni mwa mabalozi wenzake wanao tumikia nchi zao Visiwani Comoro. Wakati akimtunuku medani hiyo, Mhe Azali alieleza kutambua mchango mkubwa aliofanya Balozi huyo katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Comoro, pamoja na kumpongeza kwa utumishi uliotukuka. 

Kwa upande wake Mhe. Balozi alieleza kufarijika sana kwa kutunukiwa Nishahi hiyo ambayo imekuwa ni heshima kubwa kwake. Aidha, Balozi Kilumanga alipongeza juhudi za Serikali ya Mhe. Azali kwa hatua inazochukua katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Comoro. Pia alipendekeza kwa Serikali hiyo kuanza kufanya taratibu za kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro.

Kutunukiwa kwa nishani hiyo kulikuwa ni kwa kushtukiza kwani Mhe. Balozi hakutarajia kabisa kutunukiwa nishani hiyo ambayo kwa kawaida hupewa raia wa Comoro ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa lao. Hivyo hii imekuwa ni heshima kubwa sio tu kwa Mhe. Balozi bali pia kwa Tanzania. 

Wakati wakiagana na Mhe. Rais, Mhe. Balozi na Mkewe Bi Irene Kilumanga walieleza kuwa kamwe hawatasahau upole na ukarimu wa Wacomoro na kwamba Comoro itaendelea kuwa mioyoni mwao daima.