Follow by Email

Thursday, December 7, 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa afanya uzinduzi wa ofisi za Umoja wa Mataifa mkoani Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa  akihutubia katika sherehe za uzinduzi wa majengo ya ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini zilizofanyika mkoani Dodoma tarehe 7 Disemba 2017.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akihutubia katika sherehe za uzinduzi wa ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa zilizofanyika mkoani Dodoma tarehe 7 Disemba 2018.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez akihutubia kwa lugha ya kiswahili katika sherehe za uzinduzi wa Ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Dodoma tarehe 7 Disemba 2017.


==============================================

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amezindua rasmi Ofisi za Umoja wa Mataifa, mkoani Dodoma tarehe 7 Disemba 2017. 

Ofisi hiyo ambayo ipo katika Mtaa wa Mlimwa, Area D, nje kidogo ya Mji wa Dodoma, itakuwa na Ofisi za Mashirika saba (7) kati ya 23 ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi nchini Tanzania hivi sasa. Mashirika hayo ni pamoja na UNICEF, UNDP, UNFPA, UN Women, IOM, FAO na WHO.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jabir Shekimweri, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Alvaro Rodriguez, Mwakilishi wa Nchi wa UNICEF, Bi. Maniza Zaman, Maofisa wa Serikali na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Akizindua Ofisi hiyo Mhe. Waziri Mkuu aliwapongeza Umoja wa Mataifa kwa hatua yao ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano(5) ya kuhamishia Makao makuu ya nchi mjini Dodoma “Serikali ya awamu ya tano(5) iliazimia kuunga mkono kwa vitendo tamko la Baba wa Taifa la Mwaka 1973 la kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi". alisema.

Aidha, alifafanua kuwa hadi sasa Waziri Mkuu, Mawaziri, watendaji wa Serikali na watumishi wa umma zaidi ya 2000 wamehamia Dodoma na mwisho wa Mwezi huu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhamia Dodoma na Mheshimiwa Rais anatarajiwa kuhamia Dodoma mapema mwakani. 

Halikadharika, Waziri Mkuu ameyahakikishia Mashirika ya Kimataifa kuwa Serikali imeandaa utaratibu mzuri wa kuhakikisha mashirika hayo pamoja na ofisi za ubalozi zinazowakilisha nchini zinapata viwanja kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi mkoani Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb), alisema "Umoja wa Mataifa umeonesha dira na kuwa nyota kwa Mashirika mengine ya Kimataifa na Balozi mbalimbali zinazowakilisha hapa nchini kwa kufungua ofisi zao hapa Dodoma".

Vilevile Mhe. Waziri Mahiga alielezea mchango wa Tanzania kwa kushiriki katika mchakato wa maboresho ya Mashirika ya Umoja wa Mataifa ili yaweze kufanya kazi kwa Pamoja, pia  alifafanua kuwa Tanzania na Ireland ndio walipewa jukumu la kukusanya maoni na kuja na andiko la kuboresha utendaji kazi wa Masharika ya Umoja wa Mataifa na andiko hilo ndilo lilozaa “United Nation delivering as One”, na kwa sasa utaratibu huu unatoa fursa ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kutoa huduma zao katika jengo moja.

Kwa upande mwingine, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Bw. Rodriguez, alisema, “ Uzinduzi wa Ofisi hii utawezesha kukuza ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Serikali hasa katika kipindi hiki muhimu Serikali inapohamia Dodoma na kwamba mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kwa karibu na Serikali"


Malengo ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa tangu miaka 72 iliyopita ni pamoja na kusimamia na kuleta maelewano baina ya nchi na nchi,kuhamasisha na kuleta maendeleo hasa kwa nchi zinazoendelea, kulinda, kuleta heshima kwa watu wote hasa kwa watu wanaonyanyaswa na wale wa makundi maalum na kusimamia na kulinda haki za binadamu ikiwemo haki ya kujitawala. Umoja wa Mataifa  una jumla ya Mashirika 50 Duniani na hapa Tanzania inawakilishwa na jumla ya Mashirika 23.

Mhe.Waziri Mkuu akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa majengo ya ofisi za mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Dodoma. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw.Jabir Shekimweri, Mhe. Waziri Mahiga na wengine ni wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini.
Bw. Alvaro Rodriguez akikabidhi zawadi ya ngao kwa Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Dodoma wakitumbuiza katika sherehe za uzinduzi wa ofisi za Mashirika ya Umoja wa Mataifa Mkoani Dodoma.

Vikundi vya ngoma vikitumbuiza.

Picha ya pamoja meza kuu pamoja na wawakilishi wa Taasisi za Serikali.
Picha ya pamoja meza kuu pamoja na watumishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.