Follow by Email

Monday, August 14, 2017

RAIS WA MISRI AWASILI NCHINI NA KUPOKEWA NA MWENYEJI WAKE RAIS DKT. MAGUFULI


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea mgeni wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na mgeni wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama na mgeni wake wake Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi wakati nyimbo za mataifa mawili ya Tanzania na Misri zikipigwa uwanjani hapo
 Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi akikagua gwaride la Heshima mara baada ya nyimbo za Taifa kupigwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijini Dar es Salaam.
Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi akiangalia vikundi vya ngoma za asili mara baada ya kuwasili nchini.
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Tanzania na Misri kushirikiana katika viwanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema kuwa Misri ina historia kubwa katika Nyanja mbalimbali za maendeleo yaliyofikiwa na mwanadamu katika dunia ya leo.

Kauli hiyo aliitoa jana Ikulu, Dar Es Salaam akiwa pamoja na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fatah Al Sisi ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili tarehe 14 na 15 Agosti 2017.

Rais Magufuli alisema kuwa ukizungumzia maendeleo ya uhandisi huwezi kukosa kuitaja Misri na ushahidi hadi leo upo namna ujenzi wa piramidi ulivyofanyika. Aidha, katika masuala ya dini, Rais Magufuli alisema kuwa maandiko yanabainisha kuwa Yesu Kristu alikimbilia nchi hyo alipotaka kuuwawa na Herode. 

“Kwa kuwa hata Manabii walikimbilia Misri nimeona nami shida zangu nizikimbizie huko na Mhe. Al Sisi amekubali tushirikiane ili kwa pamoja tutatue changamoto za kiuchumi zinazotukabili”. Rais Magufuli alisema.
Viongozi hao wawili wamekubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo, afya, elimu, utalii, ulinzi na matumizi ya maji ya mto Nile.

Kwa upande wa Ufugaji, Misri imekubali kuanzisha kiwanda kikubwa cha kusindika nyama nchini ili kukidhi mahitaji makubwa ya nyama nchini Misri na pia kutoa ajira, mapato na soko kwa wafugaji wa hapa nchini.
Aidha, Tanzania itaendelea kujifunza kutoka Misri katika sekta ya kilimo, hususan utaalamu wa umwagiliaji. “Nchi ya Misri ina eneo kubwa kidogo kuliko Tanzania lakini asilimia 95 ya eneo hilo ni jangwa ambalo huwezi kufanya shughuli za kilimo. Licha ya eneo linalotumika kwa kilimo kuwa dogo, lakini nchi hiyo inazalisha chakula cha kutosha na ziada ya kuuza nje”. Rais Magufuli alisema.

Kuhusu masuala ya afya, Misri imeahidi kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu nchini Tanzania ambapo Rais Magufuli alisema kiwanda hicho kitakapokamilika na kuanza kazi, kitaokoa fedha nyingi za Serikali zinazotumika kwa ajili kuagiza dawa nje ya nchi.
Suala la matumizi ya maji ya mto Nile, Rais Magufuli alieleza kuwa wamekubaliana na mgeni wake kuwa wataendelea kujadiliana ili kupata utaratibu mzuri wa kutumia maji hayo utakaokuwa na maslahi kwa nchi zote zinazopitiwa na mto huo.

Viongozi hao pia wamekubaliana kubadilishana uzoefu katika sekta ya utalii ambapo Misri imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Misri inapokea watalii zaidi ya milioni 10 kila mwaka ukilinganisha na idadi ya watalii milioni 2 ambayo Tanzania inapata kwa mwaka. Hivyo, Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Misri ili kuongeza idadi ya watalii wa kutembelea Tanzania kwa mwaka.

Rais Nagufuli alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa Ziara ya Mhe. Al Sisi imeimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Misri, Marehemu Gamal Abdel Nasser. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kibiashara kati ya nchi hizo mbili ambapo kwa takwimu zilizopo kiwango cha biashara kwa mwaka ni Dola milioni 778 na uwekezaji wa Misri nchini ni Dola milioni 887, viwango ambavyo bado ni vya chini mno.

Kwa upande wake, Rais wa Misri alipongeza hatua mbalimbali zinazochokuliwa na Rais Magufuli za kuiendeleza nchi kiuchumi pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi. Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mtangamano ndani ya Afrika na kupata msimamo mmoja wa Bara la Afrika katika masuala mbalimbali ya kimataifa.    
Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15 Agosti 2017

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.