Follow by Email

Tuesday, May 30, 2017

Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mahiga katika hotuba yake aliliomba Bunge kupitisha kiasi cha shilingi150,845,419,000 ambapo katika kiasi hiki cha fedha shilingi142,845,419,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 8,000,000,000 imetengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Bajeti hii ya mwaka 2017/2018 pamoja na mambo mengine imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu ya Wizara kama ifuatavyo;
 • Kutangaza mazingira mazuri ya nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa;
 • Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi wahisani, mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo;
 •  Kuendelea kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali katika kuvutia wawekezaji na watalii, kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko; 
 • Kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
 • Kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi mbalimbali wa kitaifa;
 • Kuendelea kusimamia balozi zetu katika kutekeleza majukumu ya uratibu hasa kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu;

 • Kuendelea kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo;
 • Kuongeza uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Konseli Kuu na kuendelea kununua, kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya makazi na ofisi za Balozi kwa kadri hali ya fedha itakavyoruhusu; 
 • Kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi ya Taifa letu; 
 • Kuendelea kutetea na kusimamia maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali zilizotoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini. Kwa mfano, ahadi za G8 na ile ahadi ya kila nchi tajiri kutoa asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kwa nchi zinazoendelea na kutoa asilimia 0.2 ya pato lake kwa nchi maskini sana duniani kama msaada; 
 • Kuendelea kutambua jumuiya za watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa; 
 • Kuratibu maandalizi na kushiriki kwenye majadiliano katika mikutano ya Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mikutano ya Vikundi Kazi na Wataalam; 
 • Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Afrika Mashariki, miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 • Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika kuelekea kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 • Kuratibu zoezi la mapitio ya Sheria za Tanzania ili kuwezesha Watanzania kunufaika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
 • Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na COMESA na SADC pamoja na Eneo Huru la Biashara la Afrika; 
 • Kuratibu majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi (reli, barabara, bandari, nishati, viwanja vya ndege na hali ya hewa) na kijamii (elimu, afya, mazingira, jinsia na watoto) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 • Kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha katika biashara baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 • Kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki;
 • Kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia mfumo wa Confederation; 
 • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Baraza la Usalama la Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa Afrika Mashariki; 
 • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 • Kutoa Elimu kwa Umma juu ya fursa zitokanazo na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
 •  Kuratibu mapitio, utafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
 • Kuratibu na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Taasisi ya TradeMark East Africa Wizarani, Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na sekta binafsi; na 
 • Kukamilisha kuandaa Sera Mpya ya Mambo ya Nje 
Hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018  mara baada ya kuwasiliswa ilijadiliwa na kuchangiwa na Wabunge mbalimbali na hatimaye kupitishwa na Bunge hilo.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga  (Mb) akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb) akijibu hoja mbalimbali za Wabunge wakati wa Kikao cha Bunge baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya Wizara Mjini Dodoma.

Baadhi ya Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya  Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bungeni mjini Dodoma

Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akifurahia jambo na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Peter Msigwa mara baada ya kuwasilisha hotuba ya bajeti Bungeni mjini Dodoma

Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba, Katibu Mkuu  Balozi Dkt. Aziz Mlima na Waziri Kivuli wa Wizara Mhe. Msigwa wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi na baadhi ya Wabunge.

Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima wakishirikishana jambo baada ya kuwasilisha hotuba ya Madirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2017/2018 katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma

Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akijibu hoja za wa Bunge Bungeni.


Waziri Mhe.Dkt. Mahiga na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Wizara mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara Bungeni Mjini Dodoma

 HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI DKT. AUGUSTINE PHILIP MAHIGA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA BAJETI YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA
 FEDHA 2017/2018
Soma zaidi
  
Yaliyomo


ORODHA YA VIFUPISHO

AF
Adaptation Fund
AfDB
African Development Bank
AGOA
African Growth and Opportunity Act
APRM
African Peer Review Mechanism
BBC
British Broadcasting Corporation
CGTN
China Global Television Network
COMESA
Common Market for Eastern and Southern Africa
COP
Conference of Parties
DW
Deutsche Welle
EAC
East African Community
EPA
Economic Partnership Agreement
FAO
FIB
Food and Agriculture Organization
Force Intervention Brigade
GCF
Green Climate Fund
GEF
Global Environment Facility
GIZ
The Deutsche Gesellschaft für Internationale Zusammenarbeit GmbH
GPEDC
Global Partnership for Effective Development Cooperation
IAEA 
International Atomic Energy Agency
IGAD
Intergovernmental Authority on Development
ILO 
International Labour Organization
IMF 
International Monetary Fund
IOM
International Organization for Migration
IORA
Indian Ocean Rim Association
KCB
Kenya Commercial Bank
KOICA
Korea International Cooperation Agency
LDCF
Least Developed Countries Fund
MINUSCA
United Nations Multidimensional Integrated Stabilisation Mission in the Central African Republic
MK-ICC
Mt. Kilimanjaro International Convention Centre
MONUSCO
United Nations Organisation Stabilisation Mission in the Democratic Republic of the Congo
NPT
Non – Proliferation Treaty
PSPF
Public Sector Pension Fund
RFI
Radio France International
RMB
Renminbi
SADC

SDGs
Southern African Development Community
Sustainable Development Goals
TAZARA
Tanzania-Zambia Railway Authority
TBC
Tanzania Broadcasting Corporation
TEHAMA
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
TMEA
Trademark East Africa
UKIMWI
Upungufu wa Kinga Mwilini
UNAMID
United Nations African Union Mission in Darfur
UNDP

UNDAP
United Nations Development Progamme
United Nations Development Assistance Plan
UNEP 
United Nations Environment Progamme
UNESCO
United Nations Educational Scientific and Cultural Organization
UNFPA
United Nations Population Fund
UN-HABITAT
United Nations Human Settlement Programme
UNHCR
United Nations High Commission for Refugees
UNICEF
United Nations Children’s Emergency Fund
UN-ICTR
United Nations International Criminal Tribunal for Rwanda
UNIDO
United Nations Industrial Development Organization
UNIFIL
United Nations Interim Force in Lebanon
UNISFA
United Nations Interim Security Force for Abyei
UNMISS
United Nations Mission in the Republic of South Sudan
UNWTO
United Nations World Tourism Organization
UTT
Unit Trust of Tanzania
VoA
Voice of America
WHO
World Health Organization
WWF
World Wildlife Fund


UTANGULIZI

1.     Mheshimiwa Spika, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuweka mezani Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
2.        Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa fadhila na rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana tena katika Bunge lako Tukufu kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu.
3.        Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu walionitangulia kuwashukuru na kuwapongeza watoa hoja waliozungumza kabla yangu wakiongozwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Mheshimiwa Dkt. Philip Isdory Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango ambao kwa hakika hotuba zao zimekuwa dira na msingi wa kuainisha masuala muhimu ya Kitaifa na Kimataifa ambayo baadhi yake yanagusa majukumu ya Wizara yangu. 
4.        Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi wa Mhe. Balozi Adadi Mohammed Rajab (Mb) na Makamu wake Mhe. Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis (Mb) pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hiyo. Miongozo na ushauri wao katika masuala mbalimbali imekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu.
5.        Mheshimiwa Spika, ninaposimama mbele yenu kusoma hotuba hii nyuma yangu kuna kundi kubwa la watendaji na watumishi wanaoniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa. Sina budi kutoa shukrani zangu za dhati kwao kwa kuwa kwa kiasi kikubwa ndio wamewezesha nisimame mbele yenu leo kuwasilisha hotuba hii. Kwa namna ya kipekee kabisa, napenda kumshukuru Mhe. Dkt. Susan Alphonce Kolimba (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Mhe. Balozi Dkt. Aziz Ponary Mlima, Katibu Mkuu; Mhe. Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu; Mabalozi; Wakurugenzi; na Wafanyakazi wengine wote kwa weledi, umahiri na ufanisi wao katika kunisaidia kutekeleza majukumu ya Wizara yangu.
6.        Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa pongezi kwa Wabunge walioteuliwa na Mheshimiwa Rais kulitumikia Taifa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, sina budi kutoa pongezi maalum kwa Wabunge Wateule wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki. Ni dhahiri kuwa kuchaguliwa kwao ni kielelezo cha kuaminiwa na Taifa letu. Ni matarajio yetu kuwa watakuwa wazalendo, watatetea na kusimamia maslahi ya nchi yetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kutunza misingi ya mshikamano uliopo baina ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla.
7.        Mheshimiwa Spika, napenda pia kumshukuru kwa dhati mke wangu mpendwa Mama Elizabeth Mahiga, Watoto na familia yangu yote kwa ujumla kwa kunivumilia, kuniunga mkono na kunipa utulivu wa kutosha kuniwezesha kutekeleza  majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais katika kujenga taifa na kutetea maslahi ya taifa letu nje na ndani ya nchi.
8.        Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, naungana na wabunge wenzangu kutoa salamu za pole na rambirambi kwa familia za wabunge wenzetu wawili, Marehemu Hafidh Ally Tahir na Marehemu Dkt. Elly Marko Macha waliotangulia mbele ya haki wakati wakiendelea kulitumikia Taifa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, natumia fursa hii kutoa salamu za pole na rambirambi kwa familia za wafanyakazi wenzangu Wizarani, marehemu Hadija Mwichande na Marehemu Dkt. Cuthbert Leonard Ngalepeka waliotutoka katika kipindi hiki. Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awapumzishe mahala pema peponi. Amina.
9.        Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Mei, 2017 Taifa lilizizima kwa majonzi makubwa baada ya kupoteza watoto 32, walimu wawili na dereva mmoja wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea Wilayani Karatu. Kwa majonzi makubwa mno naomba nichukue fursa hii kutoa salamu za pole kwa wazazi, walimu, Mkoa wa Arusha na Watanzania wote kwa ujumla. Aidha, ninaomba nifikishe salamu za rambirambi kwa Bunge lako Tukufu kutoka Balozi mbalimbali za nchi za Nje zilizopo hapa nchini na mashirika mbalimbali ya kimataifa.
10.    Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuwashukuru wasamaria wema Dkt. Steeve Mayor, Dkt. Jennifer Milby, Dkt. Maanda Volker na Bw. Kelvin Negaard, raia wa Marekani kwa moyo wao wa upendo waliouonesha kwa kuwahudumia marehemu na majeruhi wa ajali hiyo. Ninawashukuru sana kwa msaada wao ambao haukuishia kwenye eneo la ajali bali pia walitafuta usafiri wa kuwapeleka majeruhi nchini Marekani kwa matibabu zaidi kwa gharama zao. Shukrani za dhati ziende pia kwa taasisi ya Bill Graham kwa kukubali kutoa usafiri wa ndege kuwasafirisha majeruhi, wazazi, na wataalam wa afya wa Tanzania hadi North Carolina na baadae kuchukuliwa na ndege maalum ya wagonjwa wa dharura hadi Hospitali ya Mercy iliyopo Sioux City, Iowa, Marekani wanapotibiwa hadi hivi sasa na hali zao zinaendelea vizuri. Hakika ukarimu na upendo mkubwa waliouonesha kwa watoto hawa hautasahaulika katika mioyo ya Watanzania.
11.    Mheshimiwa Spika naishukuru pia Serikali ya Jamhuri ya Kenya kwa kututia moyo wakati wa tukio hili la kuhuzunisha. Aidha, ninawashukuru watanzania wote waliojitolea kwa namna moja ama nyingine katika mazishi na matibabu ya wahanga wa ajali hiyo. Tuendelee kuwaombea majeruhi wapone haraka ili waweze kuendelea na masomo yao.

 

TATHMINI YA HALI YA DUNIA


12.    Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa tathmini ya hali na mwelekeo wa siasa duniani na jinsi Tanzania ilivyojipanga kushiriki, ningependa kulikumbusha Bunge lako Tukufu juu ya misingi ya Sera yetu ya Mambo ya Nje.
13.    Mheshimiwa Spika, baada ya Tanzania pamoja na nchi nyingine za Afrika kujikomboa kutokana na ukoloni na ubaguzi wa rangi, Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania inaendelea kujikita katika misingi ifuatayo;
1.   Kulinda uhuru, umoja na heshima ya nchi yetu;
2.   Kuendeleza ujirani mwema katika kanda yetu na kukuza umoja na ushirikiano barani Afrika;
3.   Kuheshimu kanuni ya kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine;
4.   Kutofungamana na upande wowote na kuchagua kwa hiari bila masharti marafiki katika Jumuiya ya Kimataifa;
5.   Kushirikiana kikamilifu kimataifa na nchi, mashirika na taasisi mbalimbali katika nyanja za diplomasia, siasa, uchumi, utaalam na teknolojia; na
6.   Kukuza na kutekeleza diplomasia ya uchumi, hususan uchumi wa viwanda katika Awamu hii ya Tano.
14.    Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje kama ilivyoainishwa hapa, Serikali ya Awamu ya Tano itazingatia mikakati na vipaumbele vifuatavyo:
1.   Kuanzisha mahusiano mapya ya kidiplomasia ambayo yataongeza tija kwa maslahi ya nchi hususan maendeleo ya kiuchumi na teknolojia;
2.   Kushiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu ya migogoro kwa njia ya amani kwa kuzungumza moja kwa moja na wadau husika na kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kimataifa au kitaifa katika kutatua migogoro hiyo.
15.    Mheshimiwa Spika, kwa kifupi Tanzania itaendelea na mkakati wake endelevu wa kutetea uhuru na haki kimataifa huku ikizingatia vipaumbele vyake vya maendeleo na siasa yake ya kutofungamana na upande wowote.
16.    Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya kisera naomba kutoa tathmini ya hali ya dunia.
17.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2016/2017 dunia imeshuhudia ongezeko dogo katika kasi ya ukuaji wa uchumi hususan katika mataifa ya magharibi yenye uchumi mkubwa hali inayochangia kuendelea kudorora kwa biashara ya kimataifa. Aidha, Dunia imeendelea kushuhudia ongezeko la machafuko ya kisiasa, migogoro ya kivita na vitendo vya kigaidi katika baadhi ya mataifa. Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la wakimbizi na wahamaji haramu. Kwa upande mwingine, mabadiliko ya tabianchi yamezidi kuleta athari kubwa katika ikolojia na kutishia uhai wa viumbe na shughuli za kibinadamu. Athari hii ni kubwa zaidi kwenye mataifa yanayoendelea kutokana na uwezo mdogo wa mataifa hayo kukabiliana na changamoto hizo, hivyo kurudisha nyuma juhudi za kujikwamua na umaskini. Matukio hayo ya kidunia yameibua hisia kuwa ipo haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya jitihada mahsusi kukabiliana nayo ili kuimarisha ustawi wa Dunia kwa ujumla. Baada ya kutoa tathmini hiyo ya jumla, sasa naomba uniruhusu nitoe tathmini ya maeneo machache kama ifuatavyo:-
Hali ya Ulinzi na Usalama Duniani
(i)           Barani Afrika
18.    Mheshimiwa Spika, hali ya Ulinzi na Usalama barani Afrika imeendelea kuimarika kutokana na juhudi mbalimbali za usuluhishi na upatanishi zinazoendelea kufanywa na Jumuiya ya Kimataifa. Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja dunia imeshuhudia kupungua kwa mashambulizi yanayotekelezwa na makundi ya waasi, upinzani na magaidi katika nchi za Somalia, Afrika ya Kati na Nigeria. Vilevile, hatua za upatanishi katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho na Sudan Kusini zinaelekea kuzaa matunda kutokana na maendeleo mazuri ya  majadiliano baina ya pande zinazohasimiana. Kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Asasi ya SADC ya Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama, Tanzania imepewa jukumu la kusimamia utatuzi wa migogoro ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Lesotho. Aidha, kupitia Chama Tawala cha CCM kwa kushirikiana na Chama cha ANC cha Afrika Kusini, Tanzania imechangia katika kutafuta suluhu kwenye mgogoro wa Sudan Kusini.
(ii)          Barani Asia
19.       Mheshimiwa Spika, hali ya usalama katika Rasi ya Korea imeendelea kutetereka kutokana na vitendo vya pande mbili hasimu ambazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea kwa upande mmoja na Jamhuri ya Korea na Marekani kwa upande mwingine. Hali ya kushutumiana kwa pande hizi inatokana na kila upande kuhofia juu ya uwezekano wa uvamizi kutoka upande mwingine. Mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia pamoja na majaribio ya makombora ya masafa marefu yanayofanywa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea kwa upande mmoja na mazoezi ya kijeshi ya pamoja yanayofanywa na Jamhuri ya Korea  na Marekani kwa upande mwingine, vimezidisha hofu katika rasi hiyo na ukanda mzima. Endapo vita itatokea baina ya pande hizi mbili italeta madhara makubwa si tu katika ukanda huo bali pia eneo lote la Asia, Pasifiki na dunia kwa ujumla.
20.       Mheshimiwa Spika, Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na mshirika wa Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia na kuhimiza matumizi salama ya teknolojia hiyo. Hivyo, tutaendelea kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika kusuluhisha mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo ili kuhakikisha hali ya amani na usalama inaendelea kudumishwa duniani.
(iii)       Barani Ulaya
21 Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama katika eneo la Umoja wa Ulaya imekumbwa na changamoto ya vitendo vyenye viashiria vya ugaidi pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamaji haramu. Mashambulio ya kutumia milipuko ya mabomu katika miji ya London, Manchester, Paris, Brussels, Berlin na Stockholm yamezua hofu na taharuki kubwa miongoni mwa wananchi wa nchi hizo. Mataifa hayo ya Umoja wa Ulaya pia, yameendelea kushuhudia ongezeko kubwa la Wakimbizi kutokana na migogoro ya kivita inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati hususan nchi za Syria na Iraq. Vilevile, idadi ya Wahamaji haramu wengi wao wakitokea mataifa ya Afrika Magharibi na kuingia mataifa ya Umoja wa Ulaya nayo imeendelea kuongezeka. Hali hiyo ya wasiwasi imesababisha kuibuka kwa vyama na vikundi vyenye siasa kali ya ubaguzi katika Bara la Ulaya. Chaguzi za hivi karibuni huko Ufaransa na Uholanzi zimefanikiwa kuleta ushirikiano kwa vyama vya wastani lakini tatizo bado lipo.
(iv)        Amerika ya Kusini na Kaskazini
22.    Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama katika eneo la Amerika ya Kusini na Kaskazini imeendelea kuwa shwari ikishuhudiwa kupungua kwa mapambano baina ya majeshi ya Serikali na makundi yanayojihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika nchi kama vile Mexico. Aidha, jitihada za upatanishi katika nchi ya Colombia zimechangia kwa kiasi kikubwa kusitisha mapambano ya kivita kati ya Serikali ya nchi hiyo na kundi la uasi lijulikanalo kama FARC. Vilevile, katika nchi ya Venezuela, Serikali yenye mrengo wa kushoto inakabiliwa na upinzani mkubwa na kusababisha hali nchini humo kuendelea kuwa tete. Katika kunusuru hali hiyo, Papa Francis anajaribu kupatanisha.


Hali ya Uchumi Duniani
i).   Barani Afrika
23.      Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Benki ya Dunia, uchumi wa Bara la Afrika kwa mwaka 2016 ulishuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2015. Sababu za kushuka kwa ukuaji wa uchumi ni pamoja na kuporomoka kwa bei ya mafuta katika mataifa yanayozalisha na kuuza bidhaa hiyo kama vile Angola na Nigeria. Halikadhalika, kushuka kwa bei ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika kwenye Soko la Dunia hususan malighafi pia kumechangia kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Bara hili. Hata hivyo, kwa mwaka 2017 uchumi wa Bara hili unatarajiwa kukua japo kwa kiasi kidogo kutokana na kuimarika kwa bei ya mafuta na bei ya bidhaa katika soko la Dunia.
ii).  Barani Asia
24. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Bara la Asia ambao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukikua kwa kasi kubwa kwa wastani ukilinganishwa na ukuaji wa uchumi katika maeneo mengine duniani, ulidorora kwa kiasi hasa kutokana na kupungua  kwa ukuaji wa uchumi wa nchi kama vile China uliosababishwa na kupungua kwa mauzo ya bidhaa za nchi hiyo duniani. Hali hii, inafanya nchi kama China, Japan, India na Korea Kusini kurekebisha kwa kiwango fulani cha misaada ya uwekezaji na biashara na nchi zinazoendelea kama za Afrika.
iii).     Barani Ulaya na Amerika
25.       Mheshimiwa Spika, katika eneo la Ulaya na Amerika uchumi umedorora hata hivyo kuna dalili za kuanza kuimarika japo kwa kasi ndogo huku kukiwa na ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira kutokana na kupungua kwa biashara na uwekezaji pamoja na mzigo wa madeni unaoendelea kuathiri uchumi wa baadhi ya nchi katika Umoja wa Ulaya. Kudorora kwa uchumi wa nchi hizi kubwa kumeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
26.       Mheshimiwa Spika, katika medani za siasa, kumekuwa na chaguzi katika nchi kadhaa kama vile Marekani, Ufaransa, Uholanzi na Austria ambapo katika chaguzi zote hizo dunia imeshuhudia ongezeko kubwa la wafuasi wa siasa zenye mrengo wa kulia. Inatazamiwa kuwa Serikali mpya zilizoingia madarakani na zinazofuata mrengo huo zitajikita zaidi katika kuhamasisha maendeleo ya ndani na kupunguza kasi ya ukuaji wa biashara na uchumi wa dunia kwa ujumla. Aidha, uamuzi wa kujitoa kwa Taifa la Uingereza katika Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ni kielelezo cha siasa zenye mrengo huo. Serikali mpya ya Marekani haijafafanua siasa yake ya uhusiano na Afrika. Matamshi ya Rais wa Marekani kuhusu Afrika yamekuwa yakitofautiana na tawala zilizopita. Hata hivyo, Serikali ya Marekani imeendeleza msaada kwa Tanzania katika kupambana na maambukizi ya UKIMWI.
Mikakati ya kukabiliana na athari za kuyumba kwa uchumi
27.    Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya kuyumba kwa hali ya uchumi duniani, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kutekeleza yafuatayo:-
a)   Kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha za umma ili kuendelea kupunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo;
b)   Kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia Sera ya Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi ya mwaka 2009 na Sheria ya Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi ya mwaka 2010. Mkakati huu unasaidia kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha za kugharamia miradi ya maendeleo;
c)    Kuendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuwekeza zaidi hapa nchini. Jitihada hizi zinaenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kufanya biashara nchini na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji;
d)   Kuendelea kutafuta fursa za masoko ya bidhaa zetu, kukuza utalii wa ndani na kushawishi  watalii kutoka mataifa mengine kutembelea nchi yetu ili kupanua wigo wa mapato na kupunguza athari inayoweza kusababishwa na kuyumba kwa biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine; na
e)    Kuendelea kuhamasisha ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo itazalisha bidhaa na ajira kwa wingi na kuongeza mapato yatokanayo na kodi.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017

28.    Mheshimiwa Spika, kabla ya kueleza utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2016/2017, naomba uniruhusu niainishe kwa ufupi majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-
         i.    Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje;
       ii.    Kusimamia na Kuratibu Masuala ya Uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali;
      iii.    Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa;
      iv.    Kusimamia masuala yanayohusu Kinga na Haki za wanadiplomasia waliopo nchini;
        v.    Kusimamia na kuratibu masuala ya Itifaki na Uwakilishi;
      vi.    Kuanzisha na Kusimamia Huduma za Kikonseli;
    vii.    Kuratibu Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa;
   viii.    Kuratibu na Kusimamia Masuala ya Watanzania Waishio Ughaibuni;
      ix.    Kuratibu na Kusimamia Utekelezaji wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
       x.    Kuratibu na Kusimamia Miradi ya Maendeleo na Taasisi zilizo chini ya Wizara; na
      xi.    Kusimamia utawala na Maendeleo ya Utumishi Wizarani na kwenye Balozi zetu.

29.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu hayo kwa mwaka 2016/2017, Wizara yangu ilitengewa kiasi cha Shilingi 162,109,416,709.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 154,109,416,709.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Katika fedha zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida, Shilingi 143,768,662,709.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na  Shilingi 10,340,754,000.00 ni kwa ajili ya mishahara.
30.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017 Wizara ilitarajia kukusanya maduhuli kiasi cha Shilingi 24,001,150,000.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 19,773,333,502.00 sawa na asilimia 83 ya makusanyo yote ya maduhuli. Ni matarajio ya Wizara kuwa itafikia malengo yake ya kukusanya maduhuli yaliyokadiriwa.
31.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2017 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 95,037,516,058.00 sawa na asilimia 59 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Kati ya fedha hizo Shilingi 83,039,138,698.00 ni kwa ajili ya bajeti ya Matumizi Mengineyo; Shilingi 8,509,062,360.00 ni kwa ajili ya mishahara; na Shilingi 3,489,315,000.00 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
32.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa licha ya changamoto mbalimbali za kibajeti. Katika kipindi hiki, Wizara imeendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya fedha za umma katika kudhibiti matumizi na mapato ambapo kwa kudhihirisha hilo, Wizara pamoja na Balozi zote isipokuwa Ubalozi mmoja   zimepata Hati Safi ya Ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2015/16. Nachukua fursa hii kuwashukuru Watendaji wa Wizara na kuwahimiza waendelee kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya matumizi ya fedha za umma wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
33.      Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitumie fursa hii kueleza kwa kifupi jinsi Wizara ilivyotekeleza majukumu yake katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017:-

 

KUBUNI NA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA SERA YA NCHI YA MAMBO YA NJE

34.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na Sekta binafsi iliratibu na kufanikisha ziara za viongozi wanaokuja nchini, mikutano ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano, masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na nchi rafiki, mikutano ya Bara la Afrika na nchi nyingine pamoja na makongamano ya biashara yaliyofanyika ndani na nje ya nchi kama ifuatavyo:

India
35.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya kitaifa ya Mhe. Nerendra Modi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya India iliyofanyika nchini mwezi Julai 2016. Pamoja na mambo mengine, Serikali za Tanzania na India zilisaini Mkataba wa Mkopo wa Dola za Marekani milioni 92 kwa ajili ya mradi wa maji wa Zanzibar ambao umeanza kutekelezwa. Aidha, utekelezaji wa makubaliano ya kuondoa hitajio la viza kwa raia wa India na Tanzania wenye Pasi za Kidiplomasia na Pasi za Huduma umeanza tangu mwezi Desemba 2016.
36.      Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali ya India iliahidi kutoa mkopo wenye riba nafuu wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza maji katika miji 17 ya Kasulu, Ludewa, Manyoni, Mugumu, Chunya, Sikonge, Makonde, Handeni, Makambako, Wanging’ombe, Kayanga, Songea, Zanzibar, Geita, Kilwa Masoko na Njombe. Mnamo mwezi Machi 2017, Serikali hiyo iliwasilisha rasmi uamuzi wake wa kutoa mkopo huo ambao utatolewa na Benki ya Exim ya India kwa riba ya asilimia 1.5 na utalipwa kwa kipindi cha miaka 25. Tayari benki hiyo imewasilisha nyaraka za masharti ya mkopo huo na Serikali inaendelea na taratibu za uchambuzi.
China
37.    Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Waratibu wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Beijing, China mwezi Julai 2016. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kufuatilia utekelezaji wa Mpango Kazi uliopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za China na Afrika uliofanyika Johannesburg, Afrika Kusini mwezi Desemba 2015. Miradi inayopewa kipaumbele katika mpango kazi huo inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya reli, bandari, nishati, viwanja vya ndege, barabara, maji, mawasiliano, maeneo ya viwanda pamoja na vyuo vya ufundi. Katika kufanikisha azma hiyo, China imeelekeza majimbo yake tajiri kuhamishia viwanda vyake barani Afrika katika nchi zilizochaguliwa. Kwa upande wa Tanzania, jimbo la Jiangsu limeshaanza uwekezaji kwenye viwanda vya nguo vilivyopo Dar es Salaam na Shinyanga na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 1,630. Aidha, kampuni ya Tianhe Shiye kutoka jimbo hilo inatarajia kufanya uwekezaji katika ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda utakaogharimu Dola za Marekani bilioni mbili.
38.    Mheshimiwa Spika, kupitia ushawishi wetu wa kidiplomasia, China iliichagua Tanzania kuwa nchi ya kuzindulia mpango wake wa Diplomasia ya Umma kati yake na Bara la Afrika. Wizara iliratibu uzinduzi wa Kongamano la kwanza chini ya mpango huo, lililofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti 2016. Manufaa yaliyopatikana katika kongamano hilo ni pamoja na kukuza mahusiano na mawasiliano kati ya China na Tanzania kuanzia ngazi za Viongozi wa Serikali, wataalam, wafanyabiashara, wawekezaji, wanamichezo na baina ya watu na watu. Aidha, wasemaji wa Serikali na Taasisi zake walijengewa uwezo wa kutoa habari za nchi kwa wakati bila kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kusimamia vyombo vya habari kutopotosha umma kwa kutoa taarifa zinazopinga maendeleo ya nchi au kupotosha utendaji wa Serikali.
39.    Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Tano wa Kamati ya Pamoja ya Ushirikiano katika masuala ya Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na China ulifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba 2016. Mafanikio ya mkutano huo ni kuimarika kwa mahusiano kati ya nchi hizi mbili katika sekta za biashara, uchumi na ufundi ambapo Serikali ya China ilikubali kuipa Serikali ya Tanzania msaada wa kiasi cha RMB Yuan milioni 300 sawa na Shilingi bilioni 97. Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayokubaliwa na pande zote mbili ikiwemo mradi wa vifaa vya ukaguzi na usalama kwa ajili ya viwanja vya ndege.
40.    Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mhe. Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania iliyofanyika mwezi Januari 2017. Kufuatia ziara hiyo, Serikali zote mbili zilikubaliana kuimarisha na kukuza uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni na kijeshi pamoja na kuimarisha ushirikiano uliopo katika masuala ya kimataifa kwa manufaa ya nchi zote mbili. Aidha, Wizara imesaini Mkataba wa msaada wa fedha za China Yuan 2,000,000, sawa na Shilingi milioni 633 kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya wageni mashuhuri Chamwino, Dodoma. Kukamilika kwa ujenzi wa makazi hayo kutatoa fursa kwa Wageni hao mashuhuri kupata mahali pa kufikia panapoendana na hadhi ya nyadhifa zao. Aidha, kutokana na hatua ya Serikali kuhamishia makao yake Dodoma, ujenzi huo utapunguza gharama ya malazi ya viongozi kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja nchini kwa ziara rasmi au za kikazi. 
Kuwait                         
41.      Mheshimiwa Spika, uhusiano kati ya nchi yetu na Kuwait unazidi kuwa mzuri. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Wizara iliratibu na kufanikisha ziara ya ujumbe wa Wataalam wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait uliokuja nchini mwezi Desemba 2016, kwa lengo la kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Mfuko huo pamoja na kupokea maombi ya miradi mipya iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania. Miradi mipya iliyojadiliwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahua, mkoani Tabora na mradi wa ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.
42.    Mheshimiwa Spika, kufuatia ziara hiyo pamoja na majadiliano ya wataalam, Bodi ya Mfuko wa Kuwait kwenye kikao chake cha mwezi Februari 2017, imeidhinisha fedha za Kuwait kiasi cha Dinar 15,000,000 sawa na Shilingi bilioni 110 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Barabara ya Chaya-Nyahua yenye urefu wa kilometa 85.4. Mkataba wa mkopo huo ulisainiwa mwezi Machi 2017, Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Dkt. Philip Isidory Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango alisaini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
43.    Mheshimiwa Spika,  vilevile, Ubalozi wa Kuwait kwa kushirikiana na Wizara yangu umeanzisha kampeni ijulikanayo kama “Maabara kwa Shule za Sekondari na Kisima kwa shule za Msingi”. Miradi hii inalenga kusaidia kuwepo kwa maabara kwa shule za Sekondari na Kisima kwa shule za msingi ambapo Ubalozi huo kupitia Taasisi mbalimbali zisizo za Kiserikali za nchini Kuwait zitakuwa zinafadhili miradi hiyo. Hadi sasa shule 27 zilizopo katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga zimenufaika na programu hiyo ambayo ni endelevu.
Umoja wa Falme za Kiarabu
44.       Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushawishi wadau mbalimbali wa maendeleo hususan nchi marafiki kuchangia utoaji wa huduma za kijamii. Kufuatia mazungumzo ya Wizara yangu na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Desemba 2016, Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Programu ijulikanayo kama Zayed Giving Initiative imetoa Zahanati mbili zinazotembea ambazo zitatoa huduma bure ya kupima na kutibu magonjwa yasiyoambukiza katika mikoa yote nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja. Zahanati hizo zilitoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam mwezi Februari na Machi 2017 na sasa zipo Zanzibar tangu mwezi Aprili 2017 kabla ya kwenda mikoa mingine.
45.       Mheshimiwa Spika, Vilevile, Wizara iliratibu ziara ya Ujumbe Maalum wa Kiuchumi wa Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi ambaye ni Kaimu Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu iliyofanyika mwezi Oktoba 2016. Pamoja na mambo mengine, Ujumbe huo ulipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa Serikali.
46.       Mheshimiwa Spika, wakati wa ziara hiyo, Tanzania iliwasilisha miradi mikubwa ya sekta ya Miundombinu ya barabara, bandari, reli na viwanja vya ndege inayohitaji ufadhili kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi ambao upo chini ya Mrithi huyo wa Mfalme. Mfuko huo tayari umeidhinisha kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa Dola za Marekani milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Malagarasi hadi Uvinza mkoani Kigoma yenye urefu wa kilometa 51. Aidha, Mheshimiwa Rais amemualika Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi kufanya ziara rasmi nchini mwaka huu ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizi mbili.
47.       Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu uliofanyika Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi Desemba 2016. Katika mkutano huo, masuala yaliyojadiliwa na kuwekewa maazimio ni pamoja na kuboresha uwekezaji na biashara, nishati, ulinzi na usalama, usafiri wa anga, kuendeleza miundombinu, elimu (kupatiwa nafasi za mafunzo) pamoja na kilimo na mazingira. Wakati wa Mkutano huo,Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini mikataba miwili ya Ushirikiano katika Sekta ya Anga; na Ushirikiano katika Sekta ya Utalii.
48.       Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu ni moja kati ya nchi muhimu za kimkakati katika biashara. Ili kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili, Wizara yangu inaendelea kuratibu majadiliano ya Mkataba wa Kutotoza Kodi mara Mbili na Kukwepa kulipa Kodi (Avoidance of Double Taxation and Tax Avoidance Agreement) na Mkataba wa Kuendeleza na Kulinda Uwekezaji baina ya nchi hizi mbili (Agreement on Promotion and Protection of Investments).
49.       Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha biashara baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu, Tanzania imealikwa kushiriki kwenye maonesho makubwa ya kibiashara yatakayofanyika Dubai mwaka 2020 (Dubai Expo 2020). Naomba kutumia fursa hii, kuwashauri wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa hiyo kwa kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo.
Qatar
50.    Mheshimiwa Spika, uhusiano kati ya Tanzania na Qatar umeendelea kuwa mzuri. Kupitia uhusiano huo, Wizara imefanikiwa kupata msaada wa magari 10 ya wagonjwa kutoka Ubalozi wa Qatar uliopo nchini.  Magari hayo yalikabidhiwa kwa Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mwezi Desemba 2016. Magari hayo yamekuwa ya msaada mkubwa katika kutoa huduma za afya.
51.    Mheshimiwa Spika, Qatar ni miongoni mwa nchi zenye uzoefu mkubwa katika sekta ya gesi na mafuta. Kwa kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na gesi na mafuta, tumeona ni vyema tukafungua ubalozi Doha ili kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya nchi hizi hususan diplomasia yetu ya uchumi.
Iran
52.       Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba 2016, Wizara iliratibu ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya Afrika. Kufuatia ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, Serikali ya Iran ilikabidhi msaada wa vifaa kwa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkokotoni, Zanzibar wenye thamani ya Dola za Marekani 500,000. Aidha, Serikali ya Iran ilitoa ahadi ya kujenga vyuo vya ufundi stadi vingine zaidi Unguja na Pemba pamoja na kutoa fursa za Mafunzo kwa Watanzania katika sekta za Nishati ya Mafuta na Gesi.
53.       Mheshimiwa Spika, pia napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, Iran imeonesha utayari wa kuifutia nchi yetu madeni yaliyolimbikizwa tangu miaka ya 1970 na kuwekeza hapa nchini katika viwanda vikubwa na vidogo.
Israel
54.    Mheshimiwa Spika, uhusiano kati ya Tanzania na Israel umeendelea kuimarika. Kufuatia kuimarika kwa uhusiano huo, Serikali ya Israel imeahidi kutoa msaada wa kujenga chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma ambacho ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
55.    Mheshimiwa Spika, kupitia mradi wa Save the Child Heart unaotekelezwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Mrisho Kikwete, Serikali ya Israel imejitolea kufadhili mafunzo ya tiba ya moyo kwa madaktari wa Taasisi hiyo ili kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa nje ya nchi. Hivi sasa, Taasisi hiyo inatoa huduma kwa Watanzania na vilevile inapokea wagonjwa kutoka nchi za nje zilizo jirani. Kadhalika, Serikali ya Israel imetoa msaada wa mchoro wa kituo cha maafa kinachotegemewa kujengwa eneo la Msalato hapa Dodoma. Wataalam kutoka Israel wanategemewa kuja nchini mnamo mwezi Juni 2017 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utakaowezesha kuchora mchoro huo. Kujengwa kwa kituo hicho kinachotarajiwa kuwa na kiwango cha kimataifa kitaongeza uwezo wa Dodoma kukabiliana na maafa ikizingatiwa kuwa Dodoma inatarajia kupokea wageni wengi kutokana na azma ya Serikali kuhamia Dodoma.
56.    Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza tangu Taifa letu lipate uhuru, Tanzania inafungua ubalozi Tel Aviv mwaka huu. Kwa kufungua Ubalozi huo, Tanzania itanufaika kwa kushirikiana na Israel katika kupata utaalam wa kilimo cha umwagiliaji, TEHAMA, ulinzi na utalii.
57.    Mheshimiwa Spika, Tanzania itaendelea kushiriki katika mijadala ya kimataifa kuhusu suala la haki za Wapalestina.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
58.               Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Joseph Kabange Kabila, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alifanya ziara ya Kitaifa nchini mwezi Oktoba 2016. Kufuatia ziara hiyo, nchi hizi mbili zilisaini Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi ambayo yatawezesha kushirikiana katika kufanya utafiti wa mafuta na gesi katika Ziwa Tanganyika. Aidha, makubaliano yamefikiwa juu ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yao. Hatua hii itaongeza mapato katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha mizigo.
Morocco
59.        Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2016, Mfalme Mohamed VI wa Morocco alifanya ziara ya Kitaifa nchini. Morocco ni nchi ya tano barani Afrika yenye uchumi mkubwa. Hivyo, katika kutekeleza diplomasia yetu ya uchumi, hatuna budi kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi hiyo.
60.                Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu litakumbuka kuwa, wakati wa ziara ya Mfalme wa Morocco, wafanyabiashara wapatao elfu moja waliambatana na kiongozi huyo hatua ambayo ilitoa fursa kwa wafanyabiashara wetu hapa nchini kukutana na wafanyabiashara hao kwa lengo la kuanzisha mahusiano ya kibiashara. Kutokana na ziara hiyo, nchi hizi mbili zilisaini jumla ya Mikataba 23 ya Ushirikiano katika sekta za kilimo, uvuvi, usafiri wa anga, nishati, utalii, viwanda, fedha na bima. Pia, wakati wa ziara hiyo, Mfalme wa Morocco alitoa ahadi ya kujenga uwanja mkubwa wa kisasa wa mpira wa miguu hapa mjini Dodoma. Hadi hivi sasa eneo utakapojengwa uwanja huo limeshapatikana na timu ya wataalam kutoka nchini Morocco imeshafika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ujenzi wa uwanja huo.
Zambia
61.    Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya Kitaifa ya Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu, Rais wa Jamhuri ya Zambia iliyofanyika hapa nchini mwezi Novemba 2016. Wakati wa ziara hiyo, nchi hizi zilikubaliana kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na uchumi hususan kuongeza ufanisi wa utendaji wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia na bomba la mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia. Kufuatia ziara hiyo, Wakuu wa Nchi hizi mbili waliagiza sheria inayounda Mamlaka ya TAZARA ifanyiwe mapitio na pande zote kwa ajili ya kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo. Kufuatia agizo hilo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mheshimiwa George Mcheche Masatu, Mwansheria Mkuu wa Serikali ulifanya ziara nchini Zambia na kufanya mazungumzo na wenzao nchini humo. Katika muendelezo wa mazungumzo hayo, mnamo Mwezi Februari 2017 ujumbe wa Zambia ulifanya ziara nchini kama sehemu ya kuendeleza majadiliano ya namna ya kuboresha Sheria ya Mamlaka ya TAZARA na hivi sasa majadiliano bado yanaendelea kwa kuwahusisha wadau wengine. Aidha, Mheshimiwa Lungu alipata fursa ya kujionea maboresho yaliyofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kuahidi kushawishi wafanyabiashara nchini mwake kuendelea kutumia Bandari hiyo.
Kenya
62.    Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016. Katika mkutano huo, masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, siasa, usalama na biashara yalijadiliwa. Mkutano huo ulizidi kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya.
Malawi
63.    Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi ulifanyika Lilongwe, Malawi mwezi Februari 2017. Katika mkutano huo masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, siasa, usalama, usafirishaji, nishati, uendelezaji wa Bonde la Mto Songwe na biashara yalijadiliwa na makubaliano kufikiwa. Tanzania na Malawi zilifanikiwa kutia saini mikataba miwili ya Huduma za Anga na Mashauriano ya Kidiplomasia. Mkutano huu ulizidi kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Malawi. Aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba, mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa mpaka katika ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi chini ya usuluhishi wa Mhe. Joaquim Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jukwaa la Viongozi na Wakuu wa Nchi Wastaafu wa Umoja wa Afrika,  akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Mhe. Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini yanatarajiwa kuanza tena wakati wowote hivi karibuni. Wizara inasubiri kupata tarehe rasmi ya kuanza kwa mazungumzo hayo kutoka Ofisi ya Rais Mstaafu Mhe. Chissano.
Uganda
64.    Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda alifanya ziara ya Kitaifa nchini mwezi Februari 2017. Kufuatia ziara hiyo, nchi hizi mbili zilitia saini hati ya kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kisiasa. Halikadhalika, zilikubaliana kuimarisha mahusiano katika sekta ya biashara na uwekezaji; uchukuzi; mafuta na nishati. Viongozi wa nchi hizi mbili waliagiza kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano ifikapo mwezi Aprili 2017.
65.       Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda ulifanyika Jijini Arusha mwezi Aprili 2017. Katika mkutano huo, masuala mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja za uchumi, siasa, usalama, usafirishaji, nishati na biashara yalijadiliwa na makubaliano kufikiwa. Aidha, Mkataba wa Ubia wa Mradi wa Umeme wa Murongo - Kikagati ulisainiwa na Mawaziri wa Nishati wa pande zote mbili kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa mitambo ya kufua umeme. Vilevile, Tanzania na Uganda zilitia saini Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga.
Ethiopia
66.    Mheshishimiwa Spika, ziara ya kitaifa ya Mheshimiwa Hailemariam Dessalegn, Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia la Jamhuri ya Ethiopia ilifanyika nchini mwezi Machi 2017. Ziara hiyo imeimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi zetu mbili katika nyanja za kidiplomasia, kiuchumi na kijamii. Tanzania na Ethiopia zilikubaliana kushirikiana katika maeneo 15 ambayo ni kufungua kituo kikubwa cha kuhifadhi mizigo cha bandari kavu; Ushirikiano katika Sekta ya Anga; Ushirikiano wa Kijeshi; Matumizi ya maji ya Mto Nile; Ushirikano katika Sekta ya Nishati; na Ushirikiano katika Sekta ya Mifugo na bidhaa za Ngozi. Maeneo mengine ni Kuondolewa kwa hitajio la Visa Rejea kwa raia wa Ethiopia; Ethiopia kufungua Ubalozi wake Tanzania; Ushirikiano katika sekta ya madini; Kuendeleza lugha ya Kiswahili; Ushirikiano katika Sekta ya Utalii; Ushirikiano katika Sekta ya Michezo; Ushirikiano kwenye Sekta ya Fedha; na Ushirikiano katika Sekta ya Mawasiliano.
67.    Mheshimiwa Spika, Wizara yangu itashirikiana na Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali pamoja na sekta binafsi katika kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo.
Afrika Kusini
68.    Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa Zuma, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini alifanya Ziara ya Kitaifa nchini mwezi Mei 2017. Ziara hiyo imetoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa. Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Zuma aliambatana na ujumbe wa wafanyabiashara zaidi ya 80 hatua ambayo ilitoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kubadilishana nao uzoefu. Kwa kipindi kirefu, Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana katika sekta za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kupitia ziara hiyo, mikataba ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, sayansi, teknolojia, uwekezaji, utamaduni na kilimo ilisainiwa.


Cuba
69.    Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2016, Mheshimiwa Salvador Antonio Valdés Mesa, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba alifanya ziara nchini. Mheshimiwa Mesa akiwa nchini alifanya mazungumzo na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; na viongozi wengine wa Serikali. Kufuatia mazungumzo hayo, Serikali ya Cuba iliahidi kuendelea kuleta madaktari wa binadamu hapa nchini ili kuwajengea uwezo wataalam wetu wa Sekta ya Afya.  Kwa sasa kuna madaktari 24 kutoka Cuba ambao wanatoa huduma za kitabibu na mafunzo katika hospitali na vyuo vya afya vilivyopo nchini. Madaktari hao wamesambazwa Zanzibar na katika Mikoa ya Dar es Salaam, Ruvuma, Pwani na Mbeya.
Czech
70.       Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya Mhe. Ivan Jancarek, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech hapa nchini mwezi Septemba 2016. Wakati wa ziara hiyo Tanzania na Czech zilikubaliana kuimarisha ushirikiano uliopo na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano, katika sekta za elimu, biashara na uwekezaji. Aidha, Serikali ya Czech iliahidi kufadhili wanafunzi wa Kitanzania kusoma katika vyuo vikuu vya nchi hiyo na kujenga kiwanda cha kuzalisha viuatilifu vya wadudu wanaoshambulia mazao ya mihogo na migomba. Vilevile, Serikali hiyo iliahidi kujenga kiwanda cha kutengeneza viatu na samani ambacho kitaendeshwa kwa ubia kati yake na Jeshi la Magereza.
Finland
71.    Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya Mhe. Kai Mykkänen, Waziri wa Biashara za Kimataifa na Maendeleo wa Jamhuri ya Finland iliyofanyika nchini mwezi Novemba 2016. Pamoja na mambo mengine, Mhe. Mykkänen alishiriki katika uzinduzi wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme jijini Dar es salaam. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Finland kwa gharama ya Shilingi bilioni 74.6. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 63.56 zimetolewa na Serikali ya Finland na Shilingi bilioni 11.03 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Uswisi
72.       Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya Balozi Manuel Sager, Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Uswisi iliyofanyika mwezi Februari, 2017. Balozi huyo, alitembelea hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Francis iliyopo Ifakara na kuzindua Jengo la Wagonjwa wa Nje ambalo limejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uswisi. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuongeza ubora wa huduma za afya na kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.
Canada
73.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha uliopita, majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Canada kuhusu uhuishwaji wa msaada wa Serikali ya Canada katika Mfuko wa Afya yalikamilika. Serikali ya Canada iliridhia kuendelea kuisaidia Tanzania kupitia Mfuko huo ambapo itachangia kiasi cha Dola za Canada milioni 87.3 sawa na Shilingi bilioni 141.9 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2020. Hadi kufikia mwezi Aprili 2017, Serikali hiyo ilikuwa imetoa kiasi cha Dola za Canada milioni 19, sawa na Shilingi bilioni 30.9 kuchangia mfuko huo.
Uturuki
74.    Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Racep Tayyip Erdogan, Rais wa Jamhuri ya Uturuki alifanya ziara ya kitaifa nchini mwezi Januari 2017. Kufuatia ziara hiyo, masuala mbalimbali yalijadiliwa kati ya Tanzania na Uturuki. Miongoni mwa masuala hayo ni mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa uliozinduliwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Aprili 2017. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu itahusisha ujenzi wa kipande cha reli kuanzia Dar-es-Salaam hadi Morogoro kwa kutumia fedha za ndani. Mradi huo unatekelezwa kwa ubia kati ya Kampuni ya YAPI Merkez ya Uturuki na MOTA-ENGEL AFRIKA ya Ureno. Kwa kutambua kuwa gharama za kutekeleza mradi huo ni kubwa, Wizara inaendelea kuratibu upatikanaji wa fedha kutoka kwenye mashirika ya kimataifa, taasisi za fedha na nchi rafiki kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa awamu nyingine za mradi huo. Awamu hizo zitajumuisha kipande cha kutoka Morogoro kwenda Dodoma na baadae Mwanza na Kigoma na hatimaye kuunganisha na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kukamilika kwa mradi huu kutakuza biashara, uwekezaji, ajira na kuongeza pato la taifa.
Japan
75.       Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Japan uliofanyika Jijini Dar es salaam mwezi Agosti 2016. Lengo la mkutano huo lilikuwa kupitisha miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya Japan katika mwaka 2016 hadi 2017. Jumla ya miradi 18 kutoka sekta za nishati, ujenzi wa barabara na maboresho ya bandari iliwasilishwa kwa Serikali ya Japan ili kuombewa ufadhili. Hadi kufikia mwezi Mei 2017, jumla ya miradi mitano (5) ilikuwa imekubaliwa wakati miradi 13 majadiliano bado yanaendelea. Miradi iliyokubaliwa ni: Mradi wa kuimarisha uwezo katika upangaji na utekelezaji wa programu ya kuendeleza kilimo wilayani; Mradi wa kutoa ushauri elekezi kuhusu uendelezaji wa sekta ya viwanda; Mradi wa kutoa ushauri elekezi kuhusu uendelezaji wa kongani za viwanda; Mradi wa usimamizi wa rasilimali ya maji yaliyo chini ya ardhi Zanzibar; na Mradi wa kutoa ushauri elekezi kuhusu maji kwa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar.
76.       Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika uliofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika nchini Kenya mwezi Agosti 2016. Nchi 48 za Afrika zilishiriki katika Mkutano huo. Matokeo ya mkutano huo ni pamoja na azma ya Serikali ya Japan:
             i.          Kutoa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 30 kwa Bara la Afrika ambazo zitatolewa kwa njia ya misaada, mikopo na uwekezaji katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Kati ya kiasi kilichoahidiwa, Dola za Marekani bilioni 10 zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika. Miundombinu hii ni pamoja na barabara, umeme na mipango miji;
           ii.          Kutoa mafunzo kwa vijana takribani 30,000 katika fani mbalimbali kama vile uendeshaji na usimamizi wa viwanda, ufundi, shughuli za kiuchumi na elimu ya biashara;
          iii.          Kutoa walimu wa kujitolea wapatao 20,000 kwa ajili ya kufundisha masomo ya hisabati na sayansi ili kuwajengea uwezo wanafunzi katika masomo hayo;
          iv.          Kuongeza Dola za Marekani bilioni 2 kwenye Mfuko wa Kukuza Biashara na Uwekezaji; na
            v.          Kuanzisha Japan - Africa Public-Private Economic Forum ili kukuza majadiliano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma kati ya Afrika na Japan.

Jamhuri ya Korea
77.       Mheshimiwa Spika, mwezi Julai 2016 Wizara iliratibu mkutano kati ya Ujumbe kutoka Jamhuri ya Korea ulioongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya Exim ya Korea na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkutano huo, Serikali ya Jamhuri ya Korea iliahidi kuipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2020. Aidha, nchi hiyo iliichagua Tanzania kuwa moja ya nchi za kipaumbele katika ushirikiano wake na nchi za Afrika.Vilevile, kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, Wizara iliratibu programu maalum ya upatikanaji wa walimu wa kujitolea wa masomo ya Sayansi na Hisabati kutoka nchi hiyo kwa ajili ya kuja kufundisha nchini. Mwezi Agosti 2016 Wizara iliwapokea walimu 10 ambao wamepangwa kufundisha katika shule za Sekondari za Zanaki, Benjamin William Mkapa na Jangwani zilizopo Dar es Salaam.
78.       Mheshimiwa Spika, mwezi Agosti 2016 Wizara iliratibu ziara ya Wabunge kutoka Jamhuri ya Korea waliofika nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Dkt. Tulia Ackson (Mb), Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Madhumuni ya ziara hii yalikuwa ni kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Jamhuri ya Korea.
79.       Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia, Serikali ya Jamhuri ya Korea imeifahamisha Wizara yangu kuwa inawasiliana na Bunge la nchi yao ili kuikaribisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kutembelea Bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kubadilishana uzoefu.
80.       Mheshimiwa Spika, halikadhalika mwezi Septemba 2016, Wizara iliratibu ziara ya ujumbe kutoka Taasisi ya Ushirikiano katika masuala ya Kilimo kati ya Jamhuri ya Korea na Afrika iliyoanzishwa mwaka 2010. Taasisi hiyo inajishughulisha na utafiti wa mazao ya kilimo na dawa za kuua wadudu wanaoshambulia mazao. Tafiti za Taasisi hiyo hufanyika kwa kushirikiana na maafisa ugani wa nchi husika kwenye mazao mbalimbali kama vile mpunga, mihogo, nyanya na mengineyo. Nchi wanachama hupata fursa za kupata mafunzo, kubadilishana uzoefu na utafiti kupitia mikutano na makongamano mbalimbali yanayoandaliwa kila mwaka na taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.
81.       Mheshimiwa Spika, miongoni mwa miradi inayotekelezwa na taasisi hiyo ni Africa Rice ambao ni mradi mkubwa wa utafiti katika zao la mpunga wenye lengo la kukuza teknolojia katika uzalishaji wa zao hilo ili kupunguza umaskini na kuhakikisha usalama wa chakula. Kutokana na ziara hiyo Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeanza hatua za awali za kujiunga na Taasisi hiyo ili kupata utaalam zaidi utakaowezesha kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.
82.       Mheshimiwa Spika, vilevile,Wizara iliratibu ziara ya wajumbe kutoka Jamhuri ya Korea kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa Maji Taka katika Jiji la Dar es Salaam mwezi Septemba 2016. Wajumbe hao walikutana na kufanya mazungumzo na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam. Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kufadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa Dola za Marekani milioni 9.9. Kukamilika kwa mradi huo kutapunguza adha ya maji taka na kuhakikisha usalama wa afya kwa wakazi katika Jiji la Dar es Salaam.
83.        Mheshimiwa Spika, mwezi Aprili 2017 nilifanya ziara ya kikazi ya kwanza Barani Asia kwa kutembelea Jamhuri ya Korea nikiwa kama Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wakati wa ziara yangu nilifanya mkutano na mwenyeji wangu Mhe. Yun Byung-se, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na tulizungumzia masuala mbalimbali yenye maslahi kwa nchi zetu, ikiwemo hali ya sasa ya ushirikiano wa kiuchumi na miradi ya maendeleo. Aidha, tulijadili kuhusu hali ya Rasi ya Korea ambapo Tanzania tuliendelea kusisitiza msimamo wetu wa kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Kimataifa katika kuhakikisha amani na usalama katika Rasi hiyo inapatikana. Nilifanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea mwaka 1992.
84.       Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka 25, Serikali ya Korea imeisaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo Ujenzi wa Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi unaojumuisha madaraja matatu yenye jumla ya urefu wa mita 275  pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 48; na Ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 600. Vilevile, Serikali ya Korea imefadhili ujenzi wa Hospitali ya mama na mtoto iliyopo Chanika, Dar es Salaam yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 160 ambayo inatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni. Aidha, Watanzania zaidi ya 1,000 wamenufaika kwa kupata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali nchini Korea.
85.       Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, Jamhuri ya Korea imefadhili ujenzi wa shule ya Sekondari ya Tumaini iliyopo Kwarara, Unguja. Aidha, Jamhuri ya Korea imekubali kuisaidia Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar vitendea kazi kwa lengo la kuijengea uwezo mamlaka hiyo. Vilevile, Serikali ya nchi hiyo kupitia shirika lake la Maendeleo la KOICA inatarajia kutekeleza mradi wa kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji Pemba na Unguja  wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 50.
86.       Mheshimiwa Spika, katika ziara yangu nilipata pia fursa ya kukutana na Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Korea  kwa lengo la kuwasilisha ombi la kujengewa uwezo Serikali yetu katika masuala mbalimbali ya kiutendaji. Aidha, nilitumia nafasi hiyo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini kwa baadhi ya Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Korea. Vilevile, nilitembelea Chuo cha Taifa cha Diplomasia cha Jamhuri ya Korea kwa ajili ya kujifunza uendeshaji wa Chuo hicho pamoja na kuimarisha ushirikiano wakidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.
87.       Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine Jamhuri ya Korea imeahidi kuendelea kuisadia nchi yetu katika maeneo mbalimbali itakayohitaji kujengewa uwezo, kuhamasisha wafanyabiashara kuwekeza nchini na kuimarisha ushirikiano wa vyuo vyetu vya diplomasia.
Ushiriki wa Tanzania katika Makongamano ya Biashara
88.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Taasisi ya Sekta Binafsi katika kuratibu maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya kibiashara na uwekezaji ya kimataifa. Faida za majukwaa hayo ni kufungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara wa kitanzania na kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kuvutia uwekezaji nchini hususan katika sekta ya viwanda.
89.    Mheshimiwa Spika, hadi sasa, majukwaa ambayo Wizara imeyafanikisha kwa kushirikiana na wadau hao ni Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na India lililofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Julai 2016; Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Rwanda lililofanyika Kigali mwezi Septemba 2016; Kongamano la Pili la Biashara kati ya Tanzania na Misri lililofanyika Cairo mwezi Septemba 2016; Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  lililofanyika Lubumbashi mwezi Septemba 2016; Kongamano la Pili la Biashara kati ya Tanzania na Comoro lililofanyika Zanzibar mwezi Oktoba 2016; Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Israel lililofanyika Tel Aviv mwezi Novemba 2016; Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Zambia lililofanyika Lusaka mwezi Machi 2017; Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Mauritius lililofanyika Port Louis mwezi Machi 2017; Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Czech lililofanyika Prague mwezi Mei 2017; na Kongamano la Biashata kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Rome mwezi Mei 2017.
Mapitio ya Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001
90.       Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imeanza zoezi la kupitia Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 ili iweze kuendana na mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo yametokea ndani na nje ya nchi. Ili kuwa na Sera inayokidhi mahitaji ya sasa na baadae, Wizara imeunda Timu ya Wataalam inayojumuisha Wanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo cha Diplomasia; Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali; pamoja na Sekta Binafsi. Timu hiyo imeanza kufanya tathmini ya Sera hiyo kwa lengo la kupima mafanikio yaliyopatikana; kubaini mapungufu; changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake; na kuainisha namna ya kuzitatua.
91.    Mheshimiwa Spika, Sera nzuri na inayotekelezeka kwa kiasi kikubwa inategemea ushiriki wa wadau mbalimbali wakati wa uandaaji wake. Kwa kutambua umuhimu huo, Timu hiyo imekusanya maoni kutoka pande zote za Muungano kwa kuzingatia uwakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii wakiwemo Viongozi Wakuu Wastaafu; Mawaziri; wanadiplomasia; wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama; wafanyabiashara mashuhuri; wajasiriamali wadogo; watoa huduma; Asasi Zisizo za Kiserikali na wananchi kwa ujumla. Maoni hayo yalipatikana kutoka Zanzibar na mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Ruvuma, Mbeya, Kigoma na Kagera.
92.    Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa tathmini hiyo kutawezesha kuandaliwa kwa rasimu ya Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje ambayo itazingatia maoni ya wadau. Naomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine kutoa ushirikiano kila wakati Timu ya Wataalam itakapohitaji kuwaona kwa ajili ya kupata maoni yenu katika hatua inayofuata ya kuandaa rasimu ya Sera hiyo.

 

KUSIMAMIA MIKATABA NA MAKUBALIANO YA KIMATAIFA

93.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara iliratibu na kusimamia kusainiwa kwa Mikataba 12 na Hati za Makubaliano 28 baina ya Tanzania na nchi mbalimbali. Mikataba na Makubaliano hayo ni kiashiria kikubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi yetu na nchi nyingine, mashirika ya Kikanda na Kimataifa katika kuongeza kasi ya kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kutangaza utalii. Wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo kwa kuzingatia maslahi ya nchi yetu.
94.    Mheshimiwa Spika, orodha ya Mikataba na hati za Makubaliano zilizosainiwa katika kipindi hicho ni kama inavyooneshwa kwenye Kiambatisho Na. 1.

KUSIMAMIA MASUALA YANAYOHUSU KINGA NA HAKI ZA WANADIPLOMASIA WALIOPO NCHINI

95.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa jamii za kibalozi zinazowakilisha nchi zao na mashirika ya kimataifa hapa nchini, zinapata haki zao kama ilivyoainishwa katika Sheria za Kimataifa hususan Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka 1961. Aidha, Serikali inaendelea kutoa wito kwa Mabalozi, Wanadiplomasia, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa na wafanyakazi wote wenye kinga kuendelea kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na Mkataba wa Vienna.

 

KUSIMAMIA NA KURATIBU MASUALA YA ITIFAKI NA UWAKILISHI

96.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu ziara za viongozi mbalimbali wa kitaifa kwenda nje na masuala ya itifaki na uwakilishi kwa mabalozi na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
97.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu ziara za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Baadhi ya ziara za viongozi hao zilifanywa katika nchi za China, Djibout, Ethiopia, Indonesia, India, Jordan, Kenya, Mauritius, Swaziland na Umoja wa Falme za Kiarabu. Ziara hizi zimeendelea kuwa na mafanikio makubwa siyo tu katika kukuza na kuimarisha mahusiano baina yetu na nchi hizo pamoja na mashirika ya kimataifa bali zimeendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha fursa za kiuchumi pamoja na kuisaidia kupata ufadhili katika miradi mikubwa ya maendeleo.
98.    Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Wizara imeendelea kuandaa na kuratibu sherehe za kuwasilisha hati za utambulisho za Mabalozi wa nchi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini. Miongoni mwao ni Mabalozi wa nchi za Italy, Saudi Arabia, Morocco, Zambia, Cuba, Iran, Burundi, Jamhuri ya Korea, Somalia, Ireland, Canada, Thailand, Austria, Uingereza, Sudan, Slovakia, Ukraine, Ghana, Hungary, Belarus, Guinea, Botswana, Niger, Mauritius, Cyprus, Bangladesh, Nepal, Gabon, Ecuador, New Zealand na Congo Brazaville.

 

KUANZISHA NA KUSIMAMIA HUDUMA ZA KIKONSELI

99.       Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za kikonseli kwenye balozi zetu nje na kutoa viza kwa raia wa kigeni wanaotembelea nchini; kurahisisha upatikanaji wa viza kwa maafisa na watendaji wa Serikali, Vyama vya Siasa na Taasisi nyingine zinazostahili huduma hiyo; Kushirikiana na mamlaka nyingine kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania waishio nje ya nchi; na kutatua matatizo na kulinda maslahi ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye Balozi mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa hapa nchini.

 

KURATIBU MASUALA YA USHIRIKIANO WA KIKANDA NA KIMATAIFA

A.  Ushirikiano wa Kikanda
Umoja wa Afrika
100.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi Januari 2017. Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkutano huo, Wakuu wa Nchi na Serikali walijadili na kupitisha maazimio kadhaa. Miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa ni:-
i.     Umoja wa Afrika kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya amani na usalama katika nchi mbalimbali zenye migogoro barani Afrika zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Libya, Burundi na Sudan Kusini;
ii.   Nchi ambazo hazijaanza kutekeleza Makubaliano ya kutumia asilimia 0.2 ya ushuru wa forodha kwa bidhaa zote zinazoingizwa kutoka nje ya Afrika kwa ajili ya Kuchangia Umoja wa Afrika, zilipewa muda wa kujipanga hadi mwaka 2018;
iii.  Nchi wanachama zitafute fedha kwa ajili ya kutekeleza uondoshwaji wa vikwazo visivyo vya kibiashara barani Afrika; na
iv.  Ombi la nchi ya Morocco kujiunga na Umoja huo.
101.      Mheshimiwa Spika, pembezoni mwa Mkutano huo, Mheshimiwa Rais alikabidhi zawadi ya kinyago chenye kuashiria Umoja kilichowekwa katika Jengo la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lililopewa jina la Julius Nyerere Peace and Security Building. Jengo hilo lilizinduliwa mwezi Oktoba 2016 na kupewa jina hilo kutokana na mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika masuala ya amani na usalama barani Afrika.
102.      Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huo, Mheshimiwa Rais pia alipata fursa ya kukutana na viongozi mbalimbali na kujadili masuala yanayohusu mahusiano ya nchi yetu na ya Kimataifa.  Viongozi aliokutana nao ni pamoja na Mheshimiwa Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia; Mheshimiwa Prof. Arthur Peter Mutharika, Rais wa Malawi; Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda; Mhe. Abdel Fattah el-Sisi, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri; Mheshimiwa Danny Antoine Rollen Faure, Rais wa Jamhuri ya Shelisheli; na Mheshimiwa Antonio Gutteres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Mazungumzo yake na viongozi hao yalilenga katika kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kufungua fursa katika nyanja za uwekezaji, biashara na utalii.
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
103.      Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kushiriki kikamilifu katika mikutano na majukwaa mbalimbali ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Wizara iliratibu ushiriki wa nchi yetu katika masuala ya  siasa, ulinzi, usalama na utangamano wa Jumuiya hiyo kama ifuatavyo:-
Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
104.      Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika mwezi Agosti 2016 Mbabane, Swaziland, Tanzania ilikabidhiwa nafasi ya Uenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ijulikanayo kama Organ Troika kwa kipindi cha Agosti 2016 hadi Agosti 2017. Hii ni mara ya tatu kwa nchi yetu kupewa jukumu hilo adhimu kutokana na imani waliyonayo nchi wanachama kwa nchi yetu na uzoefu wetu katika utatuzi wa changamoto za kisiasa, kiulinzi na kiusalama katika Ukanda huo. Kutokana na nafasi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Wizara imeratibu na kuongoza ushiriki wa Viongozi na Wajumbe mbalimbali kwenye utatuzi wa migogoro ndani ya Ukanda huu ikiwemo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Falme ya Lesotho na Madagascar kama ifuatavyo:-
i.    Ujumbe wa Mawaziri wa Asasi ya Utatu ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
105.      Mheshimiwa Spika, kufuatia kutetereka kwa hali ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Septemba 2016 na kutokana na Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, nilipewa jukumu na Mheshimiwa Rais, kuongoza Ujumbe Maalum wa Mawaziri wa Utatu wa Asasi hiyo nchini DRC. Ziara ya kwanza ya Ujumbe wa Mawaziri ilifanyika mwezi Oktoba 2016, ambapo ujumbe ulikutana na wadau mbalimbali wa kisiasa nchini humo na kusisitiza umuhimu wa kutafuta makubaliano kwa njia ya majadiliano. Aidha, ujumbe huo  uliunga mkono Majadiliano ya Kitaifa yaliyokuwa yakiendelea nchini humo, yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika chini ya uwezeshaji wa Mhe. Edem Kodjo, Waziri Mkuu Mstaafu wa Togo. Majadiliano haya ndiyo yaliyofanikisha kufikiwa  Makubaliano ya wadau wa siasa nchini DRC ya mwezi Oktoba 2016.
106.      Mheshimiwa Spika, kwa kuwa makubaliano ya mwezi Oktoba 2016 hayakuhusisha vyama vyote vya upinzani nchini humo, juhudi za kushirikisha wadau wengine ambao hawakutia saini makubaliano hayo ziliendelea chini ya usimamizi wa Kanisa Katoliki ambapo mwezi Desemba 2016 wadau wa siasa nchini humo walitia saini Makubaliano mapya. Makubaliano hayo yanatoa mwongozo wa kuundwa kwa Serikali shirikishi ya Mpito ambayo itaongoza nchini humo hadi Uchaguzi Mkuu utakapofanyika mwezi Desemba 2017. Katika kutekeleza makubaliano hayo, mwezi Aprili 2017, Mheshimiwa Rais Kabila alimteua Bw. Bruno Tshibala, kutoka chama cha Upinzani cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS) kuwa Waziri Mkuu na mwanzoni mwa mwezi Mei 2017, Baraza Jipya la Mawaziri lilitangazwa.
107.      Mheshimiwa Spika, kufuatia maendeleo haya chanya, niliongoza ziara ya pili ya Ujumbe wa Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama nchini DRC mwezi Aprili 2017. Katika ziara hiyo, tumeweza kuona jitihada anazozifanya Mheshimiwa Rais Kabila katika kipindi hiki cha kuelekea maandalizi ya Uchaguzi Mkuu nchini humo. Hivi sasa, zoezi la uandikishaji wapiga kura linaendelea na jumla ya wananchi milioni 23 wamekwishaandikishwa kati ya milioni 40 wanaotarajiwa kuandikishwa.
108.      Mheshimiwa Spika, kwa nafasi yetu ya Uenyekiti wa SADC tuna wajibu wa kuendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha amani na usalama vinatawala nchini DRC.
ii.  Kamati ya Uangalizi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika nchini Lesotho
109.      Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimteua Mhe. Jaji Mstaafu Frederick Werema, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uangalizi ya SADC nchini Lesotho. Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka nchi za Double Troika ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Msumbiji, Swaziland na Tanzania, ilipewa jukumu la kufuatilia utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya Wakuu wa Nchi na Serikali yanayolenga kurejesha amani ya kudumu nchini humo.
110.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Kamati imefanya ziara tatu nchini Lesotho, ambapo pamoja na mambo mengine, imebaini kwamba maagizo yanayotolewa na Wakuu wa Nchi na Serikali kwa Serikali ya Lesotho hayajatekelezwa ipasavyo huku hali ya kisiasa nchini humo ikiendelea kutetereka. Itakumbukwa kuwa, Mfalme wa Lesotho alifikia uamuzi wa kuvunja Bunge la nchi hiyo baada ya Wabunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Serikali. Kwa muktadha huo, Kamati ya Uangalizi ya SADC nchini Lesotho imetoa pendekezo la kupeleka Waangalizi nchini Lesotho ili kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mageuzi na hatua za kuiwezesha nchi hiyo kurudi katika hali ya utulivu na amani huku ikijiandaa kufanya Uchaguzi Mkuu mwezi Juni 2017.
iii.   Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Zambia na Jamhuri ya Shelisheli
111.      Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kudumisha misingi ya demokrasia na amani katika Kanda, Wizara iliratibu na kuongoza Timu ya SADC ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu katika nchi za Zambia na Shelisheli.
112.      Mheshimiwa Spika, Uchaguzi Mkuu nchini Zambia uliofanyika mwezi Agosti 2016, ulihusisha vyama tisa vilivyotoa wagombea wa Urais. Uchaguzi huo uliendeshwa kulingana na Katiba ya Zambia ya mwaka 2016 ambapo Mheshimiwa Edgar Lungu alitangazwa mshindi na kuapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo tarehe 16 Agosti 2016. Timu ya waangalizi ilielezea kuridhika kwake na uchaguzi huo na kuwa ulikidhi vigezo vilivyowekwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika vya kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
113.      Mheshimiwa Spika, nilipewa heshima ya kuongoza Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika Uchaguzi Mkuu wa Wabunge wa Jamhuri ya Shelisheli uliofanyika mwezi Septemba 2016. Katika uchaguzi huo wagombea kutoka vyama vitatu vya siasa na wagombea huru watatu walishiriki kugombea majimbo 25 ya uchaguzi katika nchi hiyo. Chama Tawala cha Parti Lepep kilipata majimbo 10 na muungano wa vyama vya upinzani wa LDS ulipata majimbo 15.  Uchaguzi huo uliokuwa huru na wa haki, ulifanyika kwa amani na utulivu na ulikidhi vigezo vilivyowekwa na Jumuiya. Kutokana na chama tawala kupata ushindi mdogo katika uchaguzi huo, mwezi Oktoba 2016 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Shelisheli Mheshimiwa James Alix Mitchel, alitangaza kujiuzulu wadhifa wake na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Mheshimiwa Danny Faure. Mheshimiwa Faure aliapishwa tarehe 16 Oktoba 2016 kuwa Rais wa nchi hiyo.
iv. Mkutano wa Kamati Ndogo ya Mawaziri wa Siasa na Diplomasia
114.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki Mkutano wa Kamati Ndogo ya Mawaziri wa Siasa na Diplomasia uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Februari 2017. Katika Mkutano huo, Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Mambo ya Nje, Diplomasia na Siasa walipokea na kujadili taarifa za masuala ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Falme ya Lesotho. Vilevile, Mawaziri walipokea na kujadili taarifa za tathmini za maombi ya Burundi na Comoro kujiunga katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambapo Mawaziri walikubaliana kwamba kwa kuwa Comoro imekidhi vigezo karibu vyote vilivyowekwa na SADC, inaweza kujiunga isipokuwa kwa Burundi inayohitaji kufanyiwa uchambuzi na mjadala wa kina.
v.   Mafunzo ya Raia kuhusu Usuluhishi wa Migogoro
115.      Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maazimio ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ni kuanzisha program za kuwajengea uwezo watumishi katika masuala ya usuluhishi na upatanishi wa migogoro. Kutokana na azimio hilo, Wizara iliratibu na kushiriki katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi katika masuala ya utatuzi na usuluhishi wa migogoro yaliyoandaliwa na SADC. Jumla ya watumishi 30 kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali walishiriki mafunzo hayo. Hatua hiyo imewezesha nchi yetu kuongeza idadi ya wataalam wa masuala ya usuluhishi na upatanishi wa migogoro kwa njia ya amani.
vi.    Kuendeleza Viwanda katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
116.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa viwanda, Wizara imeratibu ushiriki wa Tanzania katika uandaaji wa Mkakati wa Jumuiya wa Kuendeleza Viwanda 2016 – 2063 na Mpango Kazi wa utekelezaji wake. Mkakati huo unalenga kuziwezesha nchi wanachama ikiwemo Tanzania, kuweka nguvu ya pamoja katika kukuza viwanda hivyo na kuziwezesha nchi kushiriki zaidi katika mnyororo wa thamani kikanda na kimataifa. Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mkakati huo uliidhinishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali katika Mkutano wa Dharura uliofanyika Mbabane Swaziland mwezi Machi 2017 ambapo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliongoza ujumbe wa Tanzania kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
vii.  Ajira kwa Watanzania katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
117.      Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Watanzania wanapata nafasi za ajira katika Sekretariati ya SADC, Wizara ilifanikiwa kuzishawishi nchi Wanachama kuongeza muda wa mkataba wa Dkt. Stergomena Laurent Tax, mtanzania ambaye kwa sasa ndiye Katibu Mtendaji wa Jumuiya. Wakuu wa Nchi na Serikali waliridhia nyongeza ya mkataba wake kwa kipindi cha pili na cha mwisho katika mkutano wao uliofanyika Mbabane, Swaziland mwezi Machi 2017. Aidha, katika mkutano huo, Mhe. Jaji Mstaafu Regina Rweyemamu aliteuliwa kuwa kati ya Majaji saba wanaounda timu ya Majaji wa kuhudumia Mahakama ya Masuala ya Kiutumishi ya Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Agosti 2017. Kufuatia ajira ya Mheshimiwa Jaji Mstaafu Rweyemamu, idadi ya Watanzania walioajiriwa katika Sekretariati ya Jumuiya imefikia 18.
Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi
118.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa kwanza wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na bahari ya Hindi uliofanyika mjini Jakarta, Indonesia mwezi Machi 2017. Mkutano huo umefanyika wakati Jumuiya ikiadhimisha miaka 20 ya kuanzishwa kwake. Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Mkutano huo, Wakuu wa Nchi na Serikali walisaini Makubaliano ya Jakarta ambayo yamebainisha mikakati, mipango na maazimio yanayolenga kuongeza kasi ya maendeleo kwa nchi wanachama kwa kuanisha mafanikio na changamoto za Jumuiya. Mkutano huo pia uliidhinisha Mpango Kazi wa utekelezaji wa Makubaliano hayo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2021.
119.      Mheshimiwa Spika, Mpango Kazi huo umejumuisha maeneo ya vipaumbele vya Jumuiya ambavyo ni Biashara na Uwekezaji, Usafiri wa Bahari, Uvuvi, Menejimenti ya Udhibiti wa Majanga, Taaluma, Sayansi na Teknolojia, Utalii na Utamaduni, Uchumi Bahari na masuala ya Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Kila Nchi mwanachama inatakiwa kuchagua eneo moja au zaidi ambalo itatoa uongozi katika utekelezaji wake. Wakati wa Mkutano huo, Tanzania ilionesha nia ya kutoa uongozi katika eneo la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Hata hivyo, taarifa rasmi za uchaguzi wa maeneo hayo zitawasilishwa na kujadiliwa katika Mkutano wa Maafisa Waandamizi utakaofanyika nchini Indonesia, mwezi Julai 2017.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
119.   Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ina dhamana ya kuratibu na kusimamia shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki  kwa mujibu wa Ibara ya 8 Ibara ndogo ya 3 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 1999. Kwa mantiki hiyo, Wizara imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania kwa kutekeleza kikamilifu majukumu mbalimbali kwa lengo la kusimamia maslahi mapana ya kitaifa katika Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-


a.   Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha
i.    Biashara na Uwekezaji katika Jumuiya ya  Afrika Mashariki
120. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika kuandaa Taarifa ya Mwenendo wa Biashara na Uwekezaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2015 ikiwa na lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Ripoti hiyo inabainisha kuwa, utekelezaji wa Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umekuwa na mafanikio katika kukuza biashara ya bidhaa na uwekezaji miongoni mwa Nchi wanachama.
121. Mheshimiwa Spika, biashara ya bidhaa miongoni mwa Nchi Wanachama imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 4,483.6 mwaka  2011 hadi kufika Dola za Marekani milioni 5,069.7 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 13. Kwa upande wa Tanzania biashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 787.1 mwaka 2011 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 1,203.6 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 53.
122. Mheshimiwa Spika, mauzo ya Tanzania kwenye Soko la Afrika Mashariki yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutoka Dola za Marekani milioni 409.0 mwaka 2011 hadi Dola za Marekani milioni 924.9 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 126 wakati manunuzi yalipungua kutoka Dola za Marekani milioni 378.1 mwaka 2011 hadi Dola za Marekani milioni 278.1 mwaka 2015 sawa na punguzo la asilimia 26.5. Bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni pamoja na visimbuzi, kamba za katani, mbogamboga, matunda, tangawizi, chai, karatasi, vyakula vya mifugo na sabuni.
123. Mheshimiwa Spika, malengo ya Umoja wa Forodha ni pamoja na kukuza biashara ya bidhaa na kuchochea uwekezaji miongoni mwa Nchi Wanachama, na ndio maana tuna kampuni kutoka nchi wanachama zilizowekeza Tanzania na kampuni za Tanzania zilizowekeza kwenye Nchi nyingine Wanachama. Baadhi ya kampuni kutoka Tanzania ni Bakhresa, Mount Meru, Benki ya CRDB na Bank M. Aidha, kampuni zilizowekeza hapa kwetu ni pamoja na Benki ya KCB na NAKUMAT. Uwekezaji unaovuka mipaka unachangia kukuza biashara na ajira miongoni mwa nchi wanachama. Katika mwaka 2016, Tanzania iliandikisha Jumla ya miradi 6 kutoka nchi za Kenya, Uganda na Rwanda yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 2.5.

ii.  Uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha
124.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha kwa lengo la kukuza biashara baina ya Nchi Wanachama na kupunguza gharama za kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika barabara Kuu ya Kati, Tanzania imeendelea kutumia vituo vitatu katika  kupima uzito wa malori yanayotumia barabara hiyo vilivyopo Vigwaza, Nyuki na Nyakahura.
125. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki, jumla ya Vikwazo Visivyokuwa vya Kiforodha 116 katika Jumuiya viliondolewa. Kati ya hivyo, vikwazo vinavyoihusu Tanzania vilivyoondolewa ni:- Kodi ya asilimia 1.5 kwa ajili ya maendeleo ya reli kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka Nchi Wanachama; kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya taratibu za uingizaji na uuzaji wa bidhaa; kodi kwa bidhaa za maonesho ya 40 ya Sabasaba kutoka kwenye Nchi Wanachama; na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kufunga ofisi mapema (saa 9 Alasiri) na hivyo kukwamisha ukaguzi wa mizigo katika bandari kavu.
126. Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa kwa upande wa Tanzania pekee ni pamoja na kuimarisha uwezo wa Kamati ya Kitaifa ya Uondoaji Vikwazo visivyo vya forodha na kuiwezesha kufanya vikao kila mwezi badala ya kila robo ya mwaka kama ilivyokuwa awali hivyo kupunguza malalamiko ya vikwazo hivyo kukaa muda mrefu bila kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
iii.   Mapitio ya Wigo wa Pamoja wa Ushuru wa Forodha na Sheria ya Uasilia wa Bidhaa

127.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kusimamia mapitio ya Wigo wa Pamoja wa Ushuru wa Forodha na Sheria ya Uasilia wa Bidhaa.  Katika kukamilisha azma hiyo, Nchi Wanachama zimekamilisha Hadidu za Rejea, kupendekeza vigezo vitakavyotumika katika kuweka kiwango cha ushuru wa forodha katika bidhaa zinazotoka nje ya Jumuiya na kuandaa Mpango Kazi wa kukamilisha kazi hiyo.
128.   Mheshimiwa Spika, Wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki katika zoezi hilo wanatoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania. Zoezi hili ni muhimu na linagusa mustakabali wa nchi yetu katika kuendeleza viwanda, uwekezaji na kukuza biashara. Hivyo, natoa wito kwa sekta binafsi kushirikiana kikamilifu na kikosi kazi hiki, ili kutoa taarifa zitakazowezesha mapitio yatakayofanyika kuwa na tija kwa ustawi wa taifa letu.
b.   Utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja
129.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kushiriki kwenye utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Mafanikio ya utekelezaji wa Itifaki hiyo kwa upande wa Tanzania ni pamoja na kuandaa na kuanza kutumia Kanuni Mpya za Uhamiaji za mwaka 2016; utaratibu wa ushirikiano kati ya taasisi zinazotoa huduma mipakani na Sheria ya Ajira za Kigeni ya mwaka 2015 ambayo imezingatia matakwa ya Itifaki ya Soko la Pamoja.

c.   Utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha
130.   Mheshimiwa Spika, Nchi Wanachama zimekamilisha Sera ya Mikataba ya Kodi ambayo itatumika kuandaa Modeli ya Mikataba ya Kodi itakayotumiwa na kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika majadiliano yanayohusu kodi na nchi nyingine. Hii itawezesha kuleta uwiano wa viwango vya kodi vinavyotozwa na nchi wanachama kwa wawekezaji kutoka nje ya Jumuiya.
d.   Ushirikiano Baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kanda Nyingine
131. Mheshimiwa Spika, Mkutano 17 wa Dharura wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Jijini Dar es Salaam mwezi Septemba 2016 ulipokea na kujadili suala la Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Ulaya (EAC-EU Economic Partnership Agreement –EPA). Baada ya majadiliano ya kina, Viongozi Wakuu wa Nchi walikubaliana kuendelea na mashauriano ili kutafuta ufumbuzi wa changamoto za EPA zilizokuwa zimebainishwa. Katika kutekeleza makubaliano ya Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu EPA, Wizara ilishirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kufanya uchambuzi wa ndani wa kina na kuandaa mapendekezo ya msimamo wa nchi. Uchambuzi uliofanyika ulionesha kuwa Mkataba huo siyo rafiki kwa ustawi wa Taifa letu hasa katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa Viwanda.
132. Mheshimiwa Spika, kufuatia maombi ya Bunge lako Tukufu, Serikali iliwasilisha Mkataba huo Bungeni. Baada ya majadiliano, Bunge lilitoa Azimio la kuishauri Serikali isisaini Mkataba huo.
133. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa 18 wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Dar es salaam mwezi Mei 2017, suala la Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki lilijadiliwa. Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kuwa Rais wa Jamhuri ya Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya kuongoza ujumbe kwenda Umoja wa Ulaya kwa lengo la kutafuta muafaka wa namna ya kuondoa changamoto zilizopo katika Mkataba huo. Aidha, ujumbe huo unalenga kushawishi Umoja wa Ulaya kutoiadhibu Kenya wakati majadiliano ya kutafuta muafaka yakiendelea.
134. Mheshimiwa Spika, Viongozi hao pia walikubaliana kuwa, endapo Juhudi za kupata muafaka kuhusu changamoto za Mkataba wa EPA kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya hazitazaa matunda ndani ya kipindi cha miezi sita, utaangaliwa uwezekano wa nchi zitakazokuwa tayari kuendelea na Mkataba wa EPA kwa mujibu wa ibara 7(e) ya Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inayohusu kanuni ya ‘‘Variable Geometry’’.
135. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri wa Eneo Huru la Biashara la Utatu wa COMESA-EAC-SADC uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Oktoba 2016. Mkutano huo ulipokea na kujadili taarifa ya maeneo yaliyosalia katika majadiliano ya awamu ya kwanza ambayo ni Uondoaji wa Ushuru wa Forodha; Uasilia wa Bidhaa; na Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara. Vilevile, Mkutano ulipokea na kuridhia baadhi ya viambatisho vya Mkataba huo vinavyohusu Vikwazo Visivyo vya Kiforodha; Ushirikiano katika Masuala ya Forodha; Uwezeshaji Biashara; Biashara ya Bidhaa zinazopita kwenda nchi nyingine; Vikwazo vya Kiufundi vya Kibiashara na Afya ya Wanyama na Mimea. Baraza la Mawaziri pia lilipokea taarifa ya utiaji saini Mkataba huo ambapo jumla ya nchi 18 tayari zilikuwa zimesaini. Kufuatia hatua hiyo, Baraza la Mawaziri liliagiza nchi ambazo hazijasaini kufanya hivyo na zile ambazo zimesaini ziendelee na taratibu za kuridhia. Tanzania imeshasaini Mkataba huo na taratibu za kuridhiwa zinaendelea.
136. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki Kongamano la 14 la AGOA lililofanyika Washington DC, Marekani mwezi Septemba 2016. Kaulimbiu ya Kongamano hilo ilikuwa ni “Kuimarisha Ushirikiano wa Kibiashara na Uwekezaji kati ya Marekani na Afrika”. Masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na: Biashara na masuala ya wafanyakazi; Tathmini ya Utekelezaji wa Mpango wa AGOA; Namna ya kugharamia miradi mikubwa ya miundombinu; Kuvutia uwekezaji ili kuhakikisha Mpango wa AGOA unatumika ipasavyo; Uwiano wa usalama na biashara kimataifa; Mkataba wa urahisishaji biashara; Uwezeshwaji wa upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati; na Mikakati ya kunufaika na mpango wa AGOA.
137. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika Majadiliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Afrika.  Hadi sasa nchi za Umoja wa Afrika zimepitisha kanuni za kuendesha majadiliano, hadidu za rejea za vikundi kazi vitakavyoshiriki katika majadiliano ya maeneo yenye utaalam mahsusi, pamoja na kupitisha mpango kazi wa namna ya kukamilisha majadiliano ya uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.
e.      Sekta za Uzalishaji
138. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika majadiliano ya Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Afya ya Wanyama na Mimea wa Jumuiya yaliyofanyika Nairobi, Kenya mwezi Novemba 2016. Muswada huo unalenga kuwa na sheria itakayoziwezesha nchi wanachama kutekeleza sera, taratibu na mikakati iliyobainishwa kwenye Itifaki ya Afya ya Wanyama na Mimea ya Jumuiya, kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa chakula cha Binadamu na Wanyama.
139.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika majadiliano ya Rasimu ya Mkataba wa kukuza na kuinua Viwanda Vidogo na vya Kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mkataba huo utatoa fursa kwa nchi wanachama kutatua  changamoto na kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati katika  Jumuiya. Miongoni mwa masuala ambayo yamepewa kipaumbele katika kuinua  Sekta hii muhimu ni:- mazingira rafiki ya ulipaji kodi; uwezeshaji wa wafanyabiashara wadogo kwa kurasimisha biashara zisizo rasmi; utoaji wa mikopo kwa riba nafuu; na kuanzisha vituo vya  kuwajengea uwezo wajasiriamali. Aidha, katika hatua ya utekelezaji wa Sera na Mkakati wa kuendeleza Viwanda  wa Afrika Mashariki, nchi wanachama zinaendelea na majadiliano ya Rasimu ya  muswada wa Uendelezaji wa Viwanda katika Jumuiya.
140.   Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu na kushiriki katika Maonesho ya 17 ya Juakali/Nguvukazi kwa mwaka 2016 yaliyofanyika Kampala, Uganda mwezi Desemba 2016. Maonesho haya yalijumuisha wajasiriamali zaidi ya mia saba kutoka nchi wanachama na yalikuwa na kaulimbiu isemayo “Nunua bidhaa za Afrika Mashariki, Jenga Uchumi wa Afrika Mashariki”.
141.   Mheshimiwa Spika, Jumla ya Wajasiriamali 138 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walishiriki maonesho hayo ambapo Tanzania ilifanikiwa kutoa washindi watatu ambao ni Bi. Margareth Kiondo katika bidhaa za vinyago; Tegoe’s Honey Group katika bidhaa za asali; na katika bidhaa za nguo mshindi alikuwa Bi. Fridah Tarimo. Washindi hao wote walitunukiwa vyeti vya ubora wa bidhaa katika maonesho hayo.
142.   Mheshimiwa Spika, Wajasiriamali wengi walitumia fursa hiyo kutangaza, na kuuza bidhaa zao, kubadilishana ujuzi, teknolojia na uzoefu katika fani mbalimbali za uzalishaji wa bidhaa pamoja na utafutaji wa masoko na pia kujenga mahusiano ya kibiashara baina yao.
      
f.    Utekelezaji wa Programu na Miradi ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii
143.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika utekelezaji wa miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki za Uendelezaji wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii kama ifuatavyo:
i.    Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani
144.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kushiriki katika ujenzi na uendeshaji wa  Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani. Katika Kituo cha Rusumo kilichopo mpakani mwa Tanzania na Rwanda limefunguliwa Tawi la Benki ya NMB ndani ya jengo la Kituo hicho lililoanza kutoa huduma mwezi Julai 2016. Kufunguliwa kwa Tawi hilo kumeongeza ufanisi katika kutoa huduma kituoni hapo. Aidha, mnamo mwezi Februari 2017 ulifanyika utafiti wa kuangalia matokeo ya kuanzisha Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Huduma kwenye Kituo hicho. Matokeo ya awali ya Utafiti huo uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan yanaonesha kuwa muda wa kukamilisha taratibu kwa malori ya mizigo yanayovuka mpaka kupitia Kituo hicho umepungua kutoka wastani wa siku moja hadi saa moja na nusu. Kwa sasa malori zaidi ya 200 yanavuka mpaka kupitia Kituo hicho kwa siku ikilinganishwa na wastani wa malori 90 kabla ya utaratibu wa Mfumo huo kuanza kutumika mwezi Machi 2016.
145.   Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa msaada wa Dola za Marekani 525,120 kwa lengo la kuwezesha uendeshaji wa Kituo cha Namanga kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya. Fedha hizo ni kwa ajili ya ununuzi wa samani na vifaa vya TEHAMA; kuwajengea uwezo wa utekelezaji wa Mfumo huo Watalaam wa Taasisi zinazotoa huduma mpakani; na kutoa elimu kwa wananchi na watumiaji wa Kituo hicho.  Mwezi Novemba 2016, Wizara iliratibu makabidhiano ya vifaa vya TEHAMA vilivyonunuliwa kupitia msaada huo. Vifaa hivyo ni pamoja na  komputa 80, swichi 8, printa 32 na scanner 20.
146. Mheshimiwa Spika, vilevile, kuhusu Kituo cha Tunduma kilichopo mpakani mwa Tanzania na Zambia, Mkataba wa Ujenzi kati ya Mkandarasi Kampuni ya Nadhra Engineering Construction Company Limited na taasisi ya Trade Mark East Africa (TMEA), ambayo ni mfadhili wa ujenzi wa Kituo hicho ulisainiwa mwezi Oktoba 2016. Ujenzi wa Kituo hicho ulianza mwezi Novemba 2016 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2018.
ii.  Uendelezaji wa Mtandao wa Barabara
147.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Kamati ya Makatibu Wakuu ya Usimamizi wa Miradi ya Barabara za Afrika Mashariki uliofanyika Mombasa, Kenya mwezi Desemba 2016. Pamoja na mambo mengine, nchi wanachama zilionesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili/Taveta – Voi, ikiwemo sehemu ya Sakina - Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 ambayo ujenzi wake utakuwa wa kipindi cha miaka miwili na nusu kuanzia mwezi Februari 2016.
148.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Wataalam wa Kikanda inayosimamia utekelezaji wa Mradi wa kuwezesha Sekta ya Uchukuzi na Biashara kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba 2016. Katika Mkutano huo, Tanzania iliwasilisha miradi ya kipaumbele katika sekta za Bandari, Nishati, Reli, Barabara na Anga ili ijumuishwe katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo. Aidha, nchi wanachama zinaendelea na majadiliano ya Rasimu ya Mfumo wa Sheria wa Matumizi ya Mtaala wa Mafunzo ya Madereva wa Magari ya Biashara katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
149.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kushiriki majadiliano ya Mpango wa Miaka 5 wa Kuwezesha Sekta ya Uchukuzi na Biashara kwa Njia ya Barabara kwenye eneo huru la biashara la utatu wa COMESA – EAC – SADC uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwezi Novemba 2016. Mpango huo unalenga kuwianisha sera, sheria, kanuni na mifumo ya kitaasisi kwenye sekta ya uchukuzi kwa njia ya barabara kwenye nchi zote 19 Wanachama wa Utatu huo.
iii.   Sekta ya Mawasiliano
150.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kushiriki katika kuandaa Rasimu ya Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Posta kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mkakati huo una lengo la kuboresha Huduma za Mawasiliano zinazotolewa kwa njia ya Posta kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia kwenye sekta hiyo. Majadiliano kuhusiana na mkakati huo yanaendelea kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.
151.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Ziara ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Februari 2017. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufuatilia hatua zilizofikiwa kuhusiana na uwianishaji wa gharama za maunganisho ya simu za mkononi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kamati hiyo ilikutana na Wataalam wa Sekta ya Mawasiliano hapa nchini. Aidha, ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa Mpango huo, wadau wa mawasiliano walipendekeza Nchi Wanachama kuweka Mitambo ya kufuatilia na kupambana na uhalifu wa kimtandao na Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya utafiti wa kubainisha faida na changamoto za mfumo huo.
iv.  Sekta ya Elimu
152.   Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wao wa 18 uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Mei 2017 walitoa Tamko la  Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa Eneo Moja la Elimu ya Juu (Declaration on the Establishment of the East African Community Common Higher Education Area).Tamko hilo lina lengo la kuhakikisha mafanikio ambayo hadi sasa yamepatikana katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye elimu ya juu yanawianishwa ili kuwa na mfumo mmoja wenye kuwezesha utolewaji wa elimu na mafunzo yenye viwango bora vitakavyotambulika baina ya Nchi Wanachama. Wakuu wa Nchi wameliagiza Baraza la Mawaziri la Jumuiya kufanya mageuzi yanayohitajika katika Elimu na Mafunzo ili kufikia lengo hili.
153.   Mheshimiwa Spika, kila mwaka Wanafunzi wa Sekondari wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huandaliwa shindano la kuandika Insha na washindi watano hutunukiwa vyeti pamoja na zawadi na Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mada ambayo wanafunzi huandikia Insha hulenga kuwajengea uelewa wa Mtangamano wa Afrika Mashariki. Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wao wa 18 uliofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Mei 2017 walitoa vyeti pamoja na zawadi kwa washindi wa Shindano la Insha la Jumuiya la mwaka 2016.  Kwa upande wa Tanzania mshindi alikuwa ni Alex Mbogo kutoka Shule ya Sekondari Kibaha, Mkoa wa Pwani.
154.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Elimu, Sayansi na Teknolojia, Utamaduni na Michezo uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Oktoba 2016. Katika Mkutano huo Nchi Wanachama ziliidhinisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Majukumu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la Mpango Mkakati huo ni kuratibu na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuzijengea uwezo taasisi zinazojihusisha na utafiti wa Kiswahili.
v.   Sekta ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii
155.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Kongamano la Pili la Watoto la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofanyika Nairobi, Kenya mwezi Agosti 2016. Lengo la Kongamano hilo lilikuwa ni kuwakutanisha pamoja Watoto wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuwapa fursa ya kushiriki katika shughuli zinazowahusu na kuwajengea uwezo wa kutambua haki zao. Katika Kongamano hilo, Sera ya Mtoto ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inalenga kulinda haki za watoto ilizinduliwa rasmi. Katika Kongamano hilo, watoto wawili na mwangalizi wao mmoja kutoka Tanzania walishiriki. 
vi.     Sekta ya Kazi na Ajira
156.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu Mkutano wa kuandaa Mpango wa Pamoja wa Kubadilishana Wafanyakazi Vijana miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Novemba 2016. Mpango huo unalenga kutekeleza Ibara ya 10 ibara ndogo ya 8 ya Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika mpango huo, nchi Wanachama zinajadili mpango wa kubadilishana vijana waajiriwa katika nchi za Jumuiya hiyo. Kukamilika kwa Mpango huo kutatoa fursa kwa vijana wetu kujijengea uwezo na kupata uzoefu katika fani mbalimbali.
vii.    Sekta ya Afya
157. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea na uratibu wa  ukamilishwaji wa Sera ya Afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sera hii iliidhinishwa na Mkutano wa 35 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika Arusha mwezi Aprili 2017. Msingi Mkuu wa Sera hii ni kutoa mwongozo katika kukabiliana na changamoto katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa hasa katika upatikanaji wa dawa zenye ubora, kuhimiza utoaji huduma za afya kwa kuzingatia misingi ya maadili, sheria na kujali utu. Aidha, Sera hii inatoa mwongozo wa kuandaa mikakati ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ya binadamu na wanyama. Vilevile, itachochea ukuaji wa ubunifu na tafiti za kisayansi na pia kuzalisha  wataalam wenye uwezo na weledi katika masuala ya Afya.
viii.  Miradi na Programu za Mazingira
158.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 17 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria pamoja na Maadhimisho ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria yaliyofanyika Kisumu, Kenya mwezi Novemba 2016. Katika Mkutano huo, Nchi Wanachama zilizindua Mpango Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Dhana ya Idadi ya Watu, Afya, na Mazingira wa mwaka 2016 – 2021. Mpango Mkakati huo utaongoza Asasi za Kiraia, Washirika wa Maendeleo na Sekta binafsi katika kuhuisha na kuratibu utekelezaji wa dhana hiyo wakati wa utekelezaji wa miradi yao.
159.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Kongamano la Utafiti wa Kisayansi na Mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria lililofanyika Jijini Mwanza mwezi Februari 2017. Kongamano hilo lilifunguliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na maazimio mengine, Kongamano hilo liliazimia Jumuiya ya Afrika Mashariki iendelee na maandalizi ya awamu ya tatu ya Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria kwa kuanza kutafuta rasilimali fedha.
g.   Utekelezaji wa Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama
160.   Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Mei 2017, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhi Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda. Hii ni kufuatia Tanzania kushika nafasi hiyo kwa vipindi viwili mfululizo. Katika kipindi cha Uenyekiti wa Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipiga hatua kubwa katika utekelezaji wa programu na miradi yake mbalimbali.
161.   Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuanza kwa utekelezaji wa Himaya Moja ya Forodha ikiwa ni utekelezaji wa Itifaki ya Jumuiya ya Umoja wa Forodha. Utekelezaji wa Himaya Moja ya Forodha umewezesha kupunguza muda wa kusafirisha mizigo na abiria baada ya vituo 11 kati ya 15 vya kutoa huduma kwa pamoja kujengwa. Kwa upande wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli zinazounganisha mataifa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ujenzi wa barabara ya Arusha – Holili – Taveta - Voi kati ya Tanzania na Kenya unaendelea ambapo kipande cha kutoka Sakina hadi Tengeru ujenzi wake unaendelea. Ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam – Tabora – Mwanza na Tabora – Kigoma – Keza – Msongati itakayounganisha Tanzania na nchi za Burundi na Rwanda umeanza. Aidha, katika kipindi hicho Jamhuri ya Sudan Kusini ilikamilisha taratibu za kisheria zilizoiwezesha kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya Hati za Kuridhia Mkataba wa Kujiunga na Jumuiya hiyo mwezi Septemba 2016.
162.   Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeainisha Shirikisho la Kisiasa kuwa ni hatua ya mwisho ya mtangamno wa Afrika Mashariki na unatekelezwa hatua kwa hatua kuanzia Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja kisha Umoja wa Fedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa. Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya katika Mkutano wao wa Kawaida wa 18 wameidhinisha Jumuiya kuanza na mfumo wa Confederation kama hatua ya kipindi cha Mpito cha kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki. Aidha, wameagiza Baraza la Mawaziri kuunda timu ya wataalam wa masuala ya katiba ili kuandaa Rasimu ya Katiba itakayoiwezesha Jumuiya kuanza kutekeleza mfumo huo.
163.   Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa kipindi cha utumishi cha Dkt. Enos Steven Bukuku, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mipango na Miundombinu, Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi Wanachama ulimteua na kumuapisha Injinia Stephen Daud Malekela Mlote kutoka Tanzania kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo. Vilevile, mkutano huo ulimteua Jaji Dkt. Charles Oyo Nyawello kutoka Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki katika Mahakama ya Awali.
164.   Mheshimiwa Spika, jitihada za usuluhishi wa Mgogoro wa Kisiasa Nchini Burundi zinaendelea chini ya Mwezeshaji Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kukamilika awamu ya mashauriano na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Burundi, Mwezeshaji ameainisha maeneo kadhaa ya msingi ambayo yatakuwa sehemu ya majadiliano.
165.   Mheshimiwa Spika, maeneo hayo ni usalama na kumaliza vitendo vya uvunjifu wa amani; utawala wa sheria na kumaliza ukiukwaji wa haki za binadamu;  hali ya utekelezaji wa Mkataba wa Amani wa Arusha wa Mwaka 2000; masuala ya demokrasia; masuala ya kijamii na binadamu, madhara ya uchumi yaliyosababishwa na mgogoro huo; uhusiano wa nchi hiyo na majirani zake pamoja na Jumuiya za Kimataifa; na utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano Maalum kuhusu Burundi wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya Kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Maeneo hayo yatawasilishwa katika awamu ya kwanza ya majadiliano ambayo inahusisha viongozi na wadau muhimu kisiasa nchini Burundi ili kuainisha yale ambayo wanakubaliana. Wadau wengine kama asasi za kijamii, viongozi wa kidini, makundi ya wanawake na vijana watashirikishwa katika awamu ya pili ya usuluhishi ili kujadili maeneno ambayo yatakosa muafaka katika awamu ya kwanza.
166.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika  Mkutano wa 7 wa Dunia wa Masuala ya Uchaguzi sanjari na Programu ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016 uliofanyika katika majimbo ya Washington DC, Maryland na Virginia mwezi Novemba 2016. Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kujenga uelewa na kuimarisha usimamizi/uendeshaji na uangalizi wa uchaguzi kwenye Kanda mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, Mkutano huo ulikuwa ni fursa kwa wajumbe na Jumuiya ya Afrika Mashariki kujifunza na kubadilishana uzoefu na Kanda nyingine kuhusu namna ya kuendesha chaguzi za kidemokrasia na kuimarisha amani na usalama wakati wa uchaguzi.
h.  Uwianishaji wa Vibali vya Kazi na Ukaazi katika Nchi Wanachama
167. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika majadiliano ya uwianishwaji wa madaraja ya vibali vya kazi/ukaazi na ada ya vibali kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kuzingatia kuwa suala la vibali vya kazi Tanzania Bara  na Zanzibar linashughulikiwa na Wizara tofauti, Tanzania imepewa muda hadi kufikia  mwezi Septemba 2017 kuwianisha Sheria na Kanuni zinazohusiana na utoaji wa vibali vya kazi na tozo za ada kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kabla ya kukamilisha majadiliano hayo katika ngazi ya Jumuiya. Wizara inaendelea kuratibu majadiliano ya ndani kuhusu suala hili.
i.    Maandalizi ya Pasi Mpya ya Kusafiria ya Kimataifa ya Afrika Mashariki
168. Mheshimiwa Spika Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Uhamiaji kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mjini Moshi mwezi Novemba 2016. Mkutano huo ulifanya tathmini ya hatua iliyofikiwa na Nchi Wanachama katika kukamilisha maandalizi ya kuanza matumizi ya Pasi Mpya ya Kusafiria ya Kimataifa ya Afrika Mashariki ifikapo mwezi Aprili 2017.
169.   Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huo ilibainika kuwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zipo katika hatua tofauti za maandalizi ya kutoa Pasi hizo. Nchi za Burundi na Kenya zimekamilisha maandalizi ya kutoa pasi hizo, wakati Tanzania, Uganda na Rwanda zinaendelea kukamilisha taratibu za utekelezaji. Hivyo, ilipendekezwa muda wa kuanza kutoa Pasi hizo usogezwe mbele kutoka mwezi Aprili 2017 hadi mwezi Desemba 2017.

j.    Mapambano Dhidi ya Ugaidi, Uharamia, Biashara Haramu ya Binadamu na Dawa za Kulevya
170. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Kupambana na Ugaidi uliofanyika Entebbe, Uganda mwezi Novemba 2016. Katika Mkutano huo, Nchi Wanachama zilibadilishana uzoefu kuhusiana na mapambano dhidi ya ugaidi, kuweka mfumo mmoja wa kurekodi na kubadilishana taarifa na mienendo ya ugaidi. Aidha, nchi wanachama zilikubaliana kuhuisha sheria za kupambana na ugaidi katika Jumuiya kwa lengo la kuwa na tafsiri moja na kiwango sawa cha adhabu.
171.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mkakati wa Kikanda wa kupambana na uharamia katika Bahari ya Hindi ambao unahusisha pia Kanda za SADC, COMESA na IGAD. Majukumu ya utekelezaji wa Mkakati huo yamegawanywa kikanda ambapo Jumuiya ya Afrika Mashariki imepangiwa jukumu la kuhifadhi watuhumiwa wa uharamia watakaokamatwa, kuendesha mashtaka dhidi yao na kuwafunga watakaopatikana na hatia na kisha kuwarejesha nchini mwao mara baada ya kumaliza vifungo.
172.   Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hilo, Jumuiya ya Afrika Mashariki iliandaa mafunzo mwezi Aprili 2017 kwa ajili ya kuwajengea uwezo Waendesha Mashtaka na Wanasheria kuhusu namna ya kushughulikia kesi za uharamia na kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa uharamia.
173.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu utekelezaji wa Mkakati wa Kikanda wa Kupambana na Biashara haramu ya Binadamu. Nchi Wanachama zimebaini kuwa tatizo la biashara haramu ya binadamu katika Jumuiya limekuwa likiongezeka kila mwaka na kwamba wahanga wakubwa wa biashara hiyo ni wanawake na watoto huku chanzo kikuu kikitajwa kuwa ni umaskini. Nchi Wanachama zimekubaliana kuhuisha sheria za kupambana na biashara hiyo na kuimarisha mawasiliano kuhusiana na mienendo ya wahusika katika biashara hiyo.
174.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu utekelezaji wa Mkakati wa Kikanda wa Kupambana na dawa za kulevya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Nchi Wanachama zilibadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali. Maeneo hayo ni pamoja na njia na mbinu mpya za usafirishaji na uzalishaji wa dawa za kulevya; kubainisha maeneo ambayo ni kitovu cha uzalishaji wa dawa za kulevya hasa bangi; na kuainisha malighafi za viwanda zinazotumika kuzalisha dawa za kulevya. Aidha, Nchi Wanachama zimekubaliana kuhuisha sheria za kupambana na dawa za kulevya, kuanzisha kanzidata ya kutunza taarifa za watuhumiwa na kuandaa Mkakati wa kuelimisha umma juu ya madhara ya dawa hizo.
k.   Mafunzo kwa Maafisa Kadeti
175. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki Mkutano wa Wakufunzi wa Vyuo vya Maafisa Kadeti wa Majeshi ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Kigali, Rwanda mwezi Machi 2017. Mkutano huo, uliandaa na kuwianisha baadhi ya masomo ambayo yatatumika kama rejea kwa vyuo vyote vya Maafisa Kadeti kwenye Nchi Wanachama wa Jumuiya. Aidha, Wakuu wa Vyuo hivyo walikubaliana masuala yatakayofundishwa kwenye masomo ili kuleta ulinganifu katika mafunzo hayo.
l.    Zoezi la Pamoja la Kijeshi la Afrika Mashariki
176. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika maandalizi ya zoezi la Pamoja la Kijeshi la Afrika Mashariki la Kamandi ya pamoja ya kijeshi lililofanyika Bujumbura, Burundi mwezi Februari 2017. Zoezi hili pia limepangwa kufanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2017. Lengo la zoezi hilo ni kujenga uwezo wa majeshi yetu katika Operesheni za kulinda Amani, kupambana na Ugaidi, kukabiliana na Majanga na Uharamia.
177. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu ya awali ya majadiliano ya Uundaji wa Mkataba wa Pamoja wa Ulinzi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya Itifaki ya Ushirikiano katika Ulinzi ya Jumuiya ambapo Nchi Wanachama zinatakiwa kukamilisha majadiliano hayo ndani ya mwaka mmoja tangu kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo. Tayari, Baraza la Mawaziri la Jumuiya limeidhinisha Rasimu hiyo kama Mwongozo wa Majadiliano ya Mkataba huo.
Bunge la Afrika Mashariki
178. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kushiriki katika Mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki. Katika Mikutano hiyo, Bunge la Tatu la Afrika Mashariki lilipitisha Miswada minne ya Sheria. Miswada hiyo itawasilishwa kwa Wakuu wa Nchi Wanachama kwa hatua stahiki. Miswada hiyo ni:-
                i.        Muswada wa Sheria wa Afrika Mashariki wa Kukabiliana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu katika Jumuiya wa mwaka 2016;
              ii.        Muswada wa Sheria wa Afrika Mashariki wa Malipo/Maslahi kwa Viongozi Maalum wa Viungo/Taasisi za Jumuiya wa mwaka 2015;
            iii.        Muswada wa Sheria wa Afrika Mashariki wa Utawala wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2016; na
             iv.        Muswada wa Sheria wa Afrika Mashariki wa Usawa wa Kijinsia wa mwaka 2016.

B.  Ushirikiano wa Kimataifa
Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu
179. Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka jana, nililifahamisha Bunge lako Tukufu kuhusu Umoja wa Mataifa kupitisha Ajenda ya mwaka 2030 iliyobeba Malengo ya Maendeleo Endelevu. Utekelezaji wa malengo hayo Kimataifa ulianza rasmi mwezi Januari 2016 na yatafanyiwa tathmini kila baada ya miaka mitano na hatimaye tathmini ya mwisho mwaka 2030. 
180. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017,Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa hapa nchini imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya Serikali kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu. Lengo ni kuhakikisha kuwa umma na makundi yote kwenye jamii yanafahamu nafasi yao kwenye utekelezaji wa Malengo hayo. Hadi sasa Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini tumeweza kutoa elimu kwa wananchi kwenye mikoa ya Mbeya, Kagera, Kilimanjaro, Kigoma, Dar es Salaam na Dodoma. Aidha, elimu hiyo pia ilitolewa Zanzibar katika visiwa vya Pemba na Unguja. Zoezi hili ni endelevu kwa nchi nzima, hivyo litaendelea kufanyika ili kuhakikisha kila mdau anashiriki ipasavyo katika kutimiza malengo ya ajenda hii. Kwa upande wa Bunge, kama ambavyo tuliwahi kutoa elimu kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa mchakato wa kuundwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu mwezi Machi 2015, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wengine muhimu tutaendelea kutoa elimu kwa Wabunge kadri itakavyohitajika ili kufanikisha utekelezaji wake.
181. Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali imeendelea kuratibu na kushiriki katika Mikutano mbalimbali ya Kimataifa kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja na nchi na wadau wengine juu ya namna bora ya kushirikiana katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu. Baadhi ya Mikutano hiyo ni:- Jukwaa la Kisiasa la Ngazi za Juu kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu lililofanyika New York, Marekani mwezi Julai 2016; Mkutano wa Ngazi ya Juu wa “Global Partnership for Effective Development Cooperation – GPEDC” uliofanyika Nairobi, Kenya mwezi Novemba hadi Desemba 2016; Mkutano wa Kimataifa kuhusu Usafiri Endelevu uliofanyika Ashgabat, Turkmenistan mwezi Novemba, 2016. Mikutano mingine ni Mkutano wa Shirika la Posta Duniani uliofanyika Istanbul, Uturuki mwezi Septemba hadi Oktoba 2016; Mkutano wa Tatu wa Shirika la Makazi Duniani uliofanyika Quito, Equador mwezi Oktoba 2016; Mkutano wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa kuhusu Uendeshaji wa Shughuli za Kimaendeleo  uliofanyika New York, Marekani mwezi Februari hadi Machi 2017; na Mkutano wa 61 wa Umoja wa Mataifa wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani uliofanyika New York, Marekani mwezi Machi 2017.
182. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na mikutano hiyo ambayo imetoa fursa kwetu kusimamia kikamilifu maslahi mapana ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
183. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Msaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ambao unatekelezwa kuanzia mwezi Julai 2016 hadi mwezi Juni 2021. Katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo, Tanzania itafaidika na miradi yenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.3 ambapo asilimia 8 ya fedha hizo zitatumika kwa miradi ya Zanzibar. Utekelezaji wa mpango huo unawiana na vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016 - 2021); na Mpango wa Pili wa Kupunguza Umaskini Zanzibar wa mwaka 2016 – 2021; Ajenda ya Afrika ya 2063; na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030.
Kikao cha 71 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
184. Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Kikao cha 71 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika New York, Marekani kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba 2016. Tanzania ilitumia Kikao hicho kueleza misimamo yake kwenye masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa Saharawi Magharibi; kuwa na Taifa la Palestina sambamba na Israel salama; na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi. Aidha, kupitia kikao hicho tuliijulisha Jumuiya ya Kimataifa juu ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua migogoro ya kisiasa inayozikabili nchi jirani; kupambana na ugaidi pamoja na dawa za kulevya. Vilevile, tulitoa taarifa kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili nchi, Bara la Afrika na dunia kwa ujumla katika kutokomeza umaskini; kupambana na rushwa; na dawa za kulevya. Aidha, Tanzania ilisisitiza kuendelea kusimamia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kama sehemu ya mkakati endelevu wa kuheshimu na kulinda haki za binadamu kwa ujumla pamoja na haki za watoto na walemavu.
185.      Mheshimiwa Spika, wakati wa Kikao hicho, pia ulifanyika Mkutano maalum kuhusu masuala ya Wakimbizi na Wahamaji uliolenga kutafuta namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo. Tanzania ilitumia fursa hiyo kuieleza dunia changamoto zinazolikabili Taifa katika kuhifadhi wakimbizi na kuzishukuru nchi marafiki na mashirika ya kimataifa kwa ushirikiano katika kusaidia kutunza wakimbizi waliopo nchini. Pamoja na kwamba Tanzania inao wajibu wa  kutunza wakimbizi kama mshirika wa mikataba ya kimataifa na sera za wakimbizi, tulitumia Mkutano huo kuitaka Jumuiya ya Kimataifa nayo kuwajibika zaidi katika suala hili kwa kuendelea kushirikiana na nchi yetu pamoja na nchi nyingine za Afrika katika kuhudumia wakimbizi na jamii za Watanzania zinazozunguka kambi za wakimbizi. Kwa mara nyingine, Tanzania iliihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa itaendelea kuheshimu mikataba ya kimataifa na kikanda inayoipa nchi yetu wajibu wa kupokea na kuhifadhi wakimbizi.
186.      Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kutumia fursa hii kuzishukuru kwa dhati nchi marafiki na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa kwa kuendelea kutuunga mkono katika kuhifadhi wakimbizi. Nchi kama Marekani, Canada, Australia na Norway zimekuwa zikipokea wakimbizi wanaohifadhiwa nchini kwa ajili ya kuwapa uraia kwenye nchi zao kama njia mojawapo ya kuwasaidia wakimbizi, hivyo kusaidia kupunguza gharama za kuwahifadhi wakimbizi hao. Kwa sasa programu ya kuhamisha wakimbizi 50,000 wenye uraia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kupatiwa uraia wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2015 hadi 2025 inaendelea vizuri.
Ushiriki kwenye Operesheni za Kulinda Amani Duniani
187.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kufuatilia ushiriki wa Tanzania kwenye Operesheni za Kulinda Amani. Hadi sasa, Tanzania ina jumla ya walinda amani 2,279 kwenye Misheni sita za Umoja wa Mataifa ambazo ni: MONUSCO, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; UNAMID, Darfur; UNIFIL, Lebanon; UNMISS, Sudan Kusini; UNISFA, Abyei; na MINUSCA, Jamhuri ya Afrika ya Kati.
188.      Mheshimiwa Spika, katika ushiriki wetu kwenye operesheni hizi, Tanzania imeendelea kuaminika na kuheshimika katika Jumuiya ya Kimataifa. Kutokana na sifa hii, Watanzania wenye ujuzi waliteuliwa kwenye Kamandi za juu kwenye Misheni mbalimbali zikiwemo MONUSCO – FIB katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na UNAMID ya Darfur, Sudan. Ushiriki huo umezidi kuwajengea Wanajeshi wetu uzoefu katika medani za kimataifa na kuongeza maarifa na mbinu mbalimbali za kijeshi ikiwemo kujifunza matumizi ya vifaa vya kisasa vya kijeshi.
189.      Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuuhakikishia uongozi wa Umoja wa Mataifa kuwa, Tanzania itaendelea kuhakikisha kuwa askari wetu wanaheshimu sheria, kanuni, taratibu na maadili ya kulinda amani katika misheni hizo.
190.      Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Wizara iliratibu na kufuatilia ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya kuhifadhi masalia na kumbukumbu za kesi za mauaji ya kimbari ya Rwanda katika eneo la Laki Laki, Arusha. Kwa kutambua umuhimu wa suala hili, Serikali imechangia eneo lenye ukubwa wa ekari 16 kwa ajili ya shughuli za ujenzi na eneo la ekari tano kati ya hizo tayari limejengwa majengo matatu ambayo ni Jengo la Mahakama; Jengo la Kuhifadhi Kumbukumbu, Maktaba, Kantini; na Jengo la Utawala.
191.      Mheshimiwa Spika, Umoja wa Mataifa umechangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 8.8 ambazo zimetumika kugharamia ujenzi wa majengo hayo ambayo mojawapo linaongoza Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa na Maktaba kubwa na ya kisasa kuhusu masuala ya sheria hususan sheria za kimataifa kuhusu uhalifu. Napenda kutumia nafasi hii kuwakaribisha Wanazuoni kutoka ndani na nje ya nchi kutumia rasilimali zinazopatikana kwenye Maktaba hiyo ili kujijengea uwezo na kuelimisha umma juu ya athari za matukio ya uhalifu kupitia tasnia hii ya sheria. Idara za Sheria, Mahakama na Vitivo vya Sheria Vyuo Vikuu mnakaribishwa kutumia maktaba hii kwa shughuli mbalimbali hasa tafiti.
192.      Mheshimiwa Spika, nafurahi kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, majengo hayo ambayo yalizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba 2016, yalijengwa na Wakandarasi wa Tanzania baada ya kushindanishwa na Kampuni nyingine za Kimataifa.
193.      Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Kisiasa, Ulinzi na Usalama ilipewa jukumu la kuwasilisha ombi maalum kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuiongezea muda Misheni ya Kulinda Amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ijulikanayo kama MONUSCO - FIB. Maamuzi haya yalifikiwa kwa kuzingatia umuhimu wa vikosi hivyo katika kulinda amani na usalama nchini humo na kwa kuzingatia hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, inayochangiwa na kuongezeka kwa vikundi vya uasi pamoja na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2017.
194.      Mheshimiwa Spika, nilipewa jukumu na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongoza Ujumbe Maalum wa Tanzania kuwasilisha ombi hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hivyo, tarehe 28 Machi 2017, niliwasilisha ombi hilo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, New York, Marekani. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tarehe 31 Machi 2017, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha kwa kauli moja Azimio la kukiongezea muda kikosi cha kulinda Amani cha MONUSCO-FIB. Kwa namna ya kipekee kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kuzishukuru nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na nchi wanachama wa SADC kwa ujumla wake kwa imani walioionesha kwa Tanzania kwa kuipa jukumu la kusimamia suala hili na kusaidia kulifanikisha.
195.      Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa suala hili, sio tu Tanzania inakuwa imetekeleza majukumu yake kama Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Kisiasa, Ulinzi na Usalama, bali pia inatekeleza moja ya nguzo za Sera yake ya Mambo ya Nje inayosisitiza ujirani mwema
196.      Mheshimiwa Spika, kuongezewa muda kwa vikosi vya MONUSCO-FIB ni hatua muhimu kwa kuwa inatoa nafasi ya kutafuta suluhu ya hali ya kisiasa ili kurejesha amani na usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha, kuwepo kwa amani na usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutaongeza fursa za biashara na faida nyingine za kiuchumi na kijamii baina ya nchi hiyo na nchi za SADC na Maziwa Makuu, hivyo kuinua uchumi wa ukanda huu na ule wa nchi moja moja.
Misaada na Mikopo kutoka Mashirika ya Kimataifa
197.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi yetu na mashirika ya fedha ya kimataifa kwa lengo la kuendelea kunufaika na ushauri wao na mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, kipaumbele kikiwa katika miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara, reli, nishati na maji.
198.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha,Viongozi mbalimbali wa mashirika ya fedha walifanya ziara za kikazi hapa nchini. Viongozi hao ni Mhe. Dkt. Frannie Léautier, aliyekuwa Makamu wa Rais Mwandamizi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika; na Bw. Amadou Hott, Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshughulikia masuala ya nishati. Viongozi hao walifanya mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wengine wa Serikali kuhusu namna ya kusaidia kuendeleza Miundombinu ya barabara, reli na nishati. Ziara hizo zilifuatiwa na ziara ya Wakurugenzi nane (8) wa Idara mbalimbali za Benki hiyo waliyoifanya hapa nchini mwezi Februari hadi Machi 2017 kwa lengo la kujadiliana kwa kina na Serikali namna bora ya kutekeleza maboresho ya sekta ya miundombinu na nishati. Miongoni mwa miradi ambayo ilijadiliwa ni ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme Malagarasi na Kakonko huko Kigoma; pamoja na njia ya kusafirisha umeme kuunganisha Ukanda wa Kaskazini Magharibi kwenye Gridi ya Taifa.
199.      Mheshimiwa Spika, Wakurugenzi hao pia, walifanya mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na kufanya tathmini ya miradi ya ujenzi wa barabara za Mahonda – Mkokotoni (Kilomita 31); Fuoni-Kombeni (Kilomita 8.6); Pale – Kiongele (Kilomita 4.6); na Matemwe – Muyuni (Kilomita 7.6) zinazofadhiliwa na benki hiyo.
200.      Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2017, Mhe. Dkt. Jim Yong Kim, Rais wa Benki ya Dunia alifanya ziara ya kikazi nchini, ambapo pamoja na mambo mengine, alifanya mazungumzo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushiriki katika kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma katika eneo la Ubungo. Wakati wa uzinduzi wa mradi huo, mikataba mikubwa mitatu (3) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 780 ilisainiwa kati ya Benki ya Dunia na Serikali. Kiongozi huyo pia, aliahidi kuendelea kuisaidia Tanzania kupata mikopo ya riba nafuu kwenye sekta mbalimbali. Mikopo hiyo inatarajiwa kufikia kiasi cha Dola za Marekani kati ya bilioni tatu (3) na nne (4) katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ujio wa viongozi hao wa ngazi za juu wa mashirika ya fedha ni ishara ya ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na Mashirika hayo na pia ni ishara ya kukubalika kwa sera za kiuchumi zinazosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Tano. Hivyo, kuimarika kwa ushirikiano huo kunatuhakikishia kuendelea kupata fedha za kuendeleza miundombinu ambayo ni kichocheo kikubwa cha ustawi wa sekta nyingine za kiuchumi kama vile kilimo na biashara na hatimaye kusukuma azma ya kukuza viwanda na kuongeza ajira.  
201.      Mheshimiwa Spika, pamoja na kudumisha ushirikiano na mashirika ya fedha, Wizara yangu imeendelea pia kushirikiana na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yanayolenga kuboresha huduma za kijamii. Katika mwaka huu wa fedha, Viongozi Wakuu wa Umoja wa Mataifa na Mashirika yake walitembelea Tanzania. Viongozi hao ni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu; Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira; na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamaji. Kwa ujumla ziara hizo zilitoa nafasi kwa Tanzania kujadiliana na Viongozi hao namna wanavyoweza kuisaidia nchi kuendeleza na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta za Afya, Mazingira na Uhamaji. Mfano, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu limeipatia Tanzania msaada wenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 831,000 unaojumuisha magari manne (4) ya wagonjwa, magari mawili (2) ya huduma na vifaa tiba
202.      Mheshimiwa Spika, vilevile, kufuatia ombi la Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa njiani kuelekea New York, Marekani, alipita kwa muda mfupi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam tarehe 9 Machi 2017 na nilifanya naye mazungumzo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais.
203.      Mheshimiwa Spika, Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliipongeza Tanzania kwa uwezo wake wa kutekeleza kanuni za utawala bora ndani ya nchi na pia kudumisha amani Barani Afrika hususan katika Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Mheshimiwa Guterres alimpongeza Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwa jitihada zao katika kutatua migogoro ya kisiasa katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Aidha, alipongeza juhudi za Tanzania za kuendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka nchi hizo. Tanzania ingependa kuona hali ya amani na utulivu inaendelea kuwepo katika nchi zinazotuzunguka ili kuzuia kuongezeka kwa wakimbizi.
Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris
204.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 22 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 22) uliofanyika Marrakech, Morocco, mwezi Novemba 2016. Mkutano huo ulikuwa ni wa kwanza tangu kupitishwa kwa Makubaliano ya Paris mwezi Desemba 2015 na ulijikita katika kujadili utekelezaji wa Makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa mwezi Novemba 2016. Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoathirika na mabadiliko ya tabianchi, imesaini Makubaliano hayo yanayoweka mikakati ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuzijengea nchi uwezo wa kukabiliana na athari hizo. Kwa sasa, Tanzania ipo katika hatua za maandalizi ya kuridhia Makubaliano hayo.
205.      Mheshimiwa Spika, pamoja na masuala mengine, Mkutano wa COP 22 ulijadili umuhimu wa mifuko ya kimataifa inayofadhili miradi ya uhifadhi wa mazingira na ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi katika kutekeleza Makubaliano ya Paris. Mifuko hiyo ambayo Tanzania imekuwa ikinufaika nayo ni pamoja na Green Climate Fund (GCF), Global Environment Facility (GEF), Adaptation Fund (AF) na Least Developed Countries Fund (LDCF). Tunaishukuru Mifuko hii kwa misaada inayotoa kwa Tanzania, na tunazishukuru nchi zinazochangia fedha kwenye Mifuko hii. Tunaendelea kutoa wito kwa nchi zilizoendelea kuendelea kuongeza michango kwenye mifuko hiyo ili nchi maskini ambazo hazijasababisha tatizo hili ziweze kutekeleza mipango na miradi ya kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko hayo.
206.      Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, inaendelea kuhamasisha sekta ya umma na sekta binafsi kufuatilia kwa karibu ufadhili unaotolewa na mifuko hiyo kwenye miradi ya kupambana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uhifadhi wa mazingira ili kuiokoa nchi na rasilimali zake na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
207.      Mheshimiwa Spika, Tanzania itaendelea kushirikiana na vyombo vya kimataifa hususan vile vya Umoja wa Mataifa katika kulinda mazingira ya wanyamapori na misitu kwa ajili ya utalii hususan matumizi endelevu ya maji ya Mto Ruaha na Mto Mara.
Mfuko wa Dunia wa Masuala ya Afya
208.      Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilishiriki kwenye Mkutano wa Tano wa Mfuko wa Dunia wa Masuala ya Afya ujulikanao kama Global Fund uliofanyika Montreal, Canada mwezi Septemba 2016. Lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kuhamasisha nchi zilizoendelea na mashirika mbalimbali ya kimataifa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 13 kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu katika nchi zinazoendelea. Mkutano huo, ulifanikiwa kuchangisha  kiasi cha  Dola za Marekani bilioni 12.9, fedha ambazo zitatumika kusaidia nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, kupambana na magonjwa hayo katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.
209.      Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuzishukuru nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa kwa kuchangia mfuko huo ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kupambana na magonjwa hayo. Aidha, napenda kutoa wito kwa nchi na mashirika mengine kuiga mfano huo. Nichukue nafasi hii tena kuishukuru Serikali na watu wa Marekani kwa msaada wa hivi karibuni kwa Tanzania wa Dola za Marekani milioni 526 kwa ajili ya kuendelea kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

 

KURATIBU NA KUSIMAMIA MASUALA YA WATANZANIA WAISHIO UGHAIBUNI

210.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuwahamasisha na kuwashirikisha Watanzania waishio ughaibuni katika kuchangia maendeleo nchini. Katika kutekeleza azma hiyo, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliandaa Kongamano la Tatu la Diaspora lililofanyika Zanzibar mwezi Agosti 2016, ambapo Diaspora kutoka zaidi ya nchi 20 duniani walishiriki. Makongamano hayo yamekuwa yakileta hamasa kubwa kwa Diaspora kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo nchini kupitia uwekezaji katika sekta za elimu, afya, miundombinu, uchukuzi, utalii, nishati na madini. Vilevile, Wizara iliratibu ushiriki wa Taasisi za Umma na Binafsi kwenye Kongamano la kuadhimisha Siku ya Tanzania yenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji kwenye sekta ya maliasili na utalii, lililofanyika Texas, Marekani mwezi Mei 2017.
211.      Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea kukusanya na kutunza kumbukumbu za Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwahimiza kusajili Jumuiya zao katika Ofisi za Balozi zilizo karibu nao. Usajili huo utaiwezesha Serikali kukamilisha kanzidata itakayopatikana katika Tovuti maalum ya Diaspora, ili taarifa za Diaspora zenye kuonesha takwimu sahihi za idadi yao, elimu, ujuzi na maarifa waliyonayo zisaidie Serikali kuwashirikisha kikamilifu katika kuleta maendeleo nchini.
212.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kutoa elimu  kwa Watanzania waishio ughaibuni ili kuhakikisha wanazitambua haki na fursa zilizopo. Tunawakumbusha kila mara kuendelea kuijengea taswira nzuri nchi yetu kwa kuishi na kufuata sheria za nchi husika, tunawapa taarifa za fursa zilizopo kwa sasa ndani ya nchi yetu, changamoto na mafanikio pamoja na kuhamasisha uwekezaji. Halikadhalika, tunasikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa kushirikiana na Serikali za nchi walizopo pamoja na Wizara za sekta husika.
213.      Mheshimiwa Spika, mathalan katika eneo la umiliki ardhi, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitoa ufafanuzi kupitia Ofisi za Balozi zetu na maeneo ya uwakilishi kuhusiana na umiliki wa ardhi. Walifahamishwa kuwa, kulingana na Sheria ya uraia namba 6 ya mwaka 1995 na Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999, Mtanzania ambaye ameukana uraia wake anapoteza hadhi ya kuwa raia wa Tanzania na hivyo hataruhusiwa kumiliki ardhi nchini. Hata hivyo, kupitia Taasisi ya Uwekezaji, Watanzania hao bado wana fursa ya kuwekeza nchini kulingana na sheria na miongozo ya uwekezaji iliyopo nchini.

 

KUSIMAMIA UTAWALA NA MAENDELEO YA UTUMISHI WIZARANI NA KWENYE BALOZI ZETU

Uwezo uliopo katika Wizara
214.      Mheshimiwa Spika, Wizara ina jumla ya watumishi 487ambapo watumishi 107 wapo kwenye Balozi zetu na watumishi 380 wapo Makao Makuu.
Mafunzo
215.      Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuwajengea uwezo watumishi waliopo, Wizara kwa kushirikiana na wafadhili imeendelea kugharamia mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi ndani na nje ya nchi. Katika kipindi hiki, watumishi 77 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi na watumishi 14 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu katika shahada ya Umahiri.
Uteuzi
216.      Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na uwakilishi nje, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Mabalozi ili kujaza nafasi zilizo wazi katika vituo vya Beijing, Paris, Brussels, Muscat, Rome, New Delhi, Pretoria, Nairobi, Brasilia, Maputo, Kinshasa, Kampala, Abuja, Moroni na Geneva. Aidha, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa Mabalozi wa vituo vipya katika nchi za Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki.

 

KURATIBU NA KUSIMAMIA MIRADI YA MAENDELEO NA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA

Miradi ya Maendeleo ya Wizara
217.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara iliidhinishiwa bajeti ya maendeleo kiasi cha Shillingi bilioni 8. Miradi iliyopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara ambalo ni sehemu ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kiasi cha Shilingi bilioni 2.3; kukamilisha ukarabati jengo la ghorofa tisa litakalotumika kwa ajili ya ofisi na makazi katika Ubalozi wa Tanzania Maputo, Msumbiji kiasi cha Shilingi bilioni 1.3; kukarabati makazi ya Balozi na watumishi yaliyopo Stockholm, Sweden kiasi cha Shilingi bilioni 2.2; kukarabati majengo mawili yanayomilikiwa na Serikali yaliyopo Khartoum, Sudan kiasi cha Shilingi bilioni 1.8; na kuboresha mfumo wa mawasiliano kati ya Wizara na Balozi za Tanzania nje kiasi cha Shilingi milioni 321.5.
218.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Mei 2017, Wizara imepokea Shilingi bilioni 3.4 za bajeti ya maendeleo sawa na asilimia 43.6. Kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi bilioni 2.1 ni kwa ajili ya kukarabati makazi ya Balozi na watumishi yaliyopo Stockholm, Sweden na Shilingi bilioni 1.3 zimetumika kwa ajili ya kumlipa mkandarasi anayekamilisha kazi ya ukarabati wa jengo la Ofisi na makazi lililopo Maputo, Msumbiji. Wizara inaendelea kufuatilia fedha za maendeleo ziliozosalia ili kuweza kutekeleza  miradi iliyopangwa.

Taasisi Zilizo Chini ya Wizara
219.      Mheshimiwa Spika, kuna taasisi tatu ambazo Wizara yangu ina jukumu la kuzisimamia ambazo ni Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, ambacho pia kinasimamia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo Dar es Salaam. Naomba nichukue fursa hii kutoa taarifa ya taasisi hizo kama ifuatavyo:-
Chuo cha Diplomasia
220.      Mheshimiwa Spika, baada ya kupata ithibati na kutambuliwa rasmi na Baraza la Ithibati la Elimu ya Ufundi, Chuo sasa kimejikita katika kutoa Programu za Diplomasia ya Uchumi ili kwenda sambamba na Sera ya Taifa ya Mambo ya Nje na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda. Aidha, Chuo kimeanza kutoa kozi za muda mfupi na muda mrefu za utatuzi wa migogoro.
221.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mipango na malengo yake ya kujiimarisha na kujitanua ili kukipa uwezo na kujitegemea, Chuo kilijikita katika kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano 2012/2013 – 2016/2017. Kipaumbele cha Mpango Mkakati huo ni kuboresha miundombinu ya Chuo ili kwenda sambamba na utekelezaji wa matakwa ya Baraza la Ithibati la Elimu ya Ufundi. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Chuo hakikupewa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo lakini Wizara kwa kutambua hilo ilitumia mahusiano mazuri yaliyopo kati yake na wadau mbalimbali kukiwezesha Chuo hicho kupata misaada ya vitendea kazi. Kupitia juhudi hizo, nchi ya Jamhuri ya Korea ilikipatia  Chuo hicho msaada wa kompyuta 150. Vilevile, Ubalozi wa Kuwait nchini ulisaidia kufanya ukarabati wa Maktaba ya Chuo hicho.
222.      Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha mazingira ya Chuo yanaboreshwa, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara yangu imetenga fedha za bajeti ya maendeleo kwa ajili ya Chuo ili kuboresha miundombinu yake. Hatua hiyo itawezesha Chuo kuongeza program, udahili na uwezo wa kujitegemea.
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha
223.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia Machi 2017 Kituo kimeweza kuwa mwenyeji wa Mikutano 274 ambayo 54 ni ya kimataifa na 220 ya kitaifa. Aidha, katika kipindi hicho, Kituo kimefanikiwa kupata mapato kiasi cha Shilingi 10,155,779,694.00 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya mapato. Vilevile, naomba kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Kituo kimeendelea kupata hati safi ya ukaguzi.
224.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/2018, Kituo kimepanga kuingiza mapato kiasi cha Shilingi 16,920,100,686.00 kutokana na vyanzo vyake mbalimbali. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kinategemewa kuingiza kiasi cha Shilingi 4,047,100,000.00.
225.      Mheshimiwa Spika, ili kuongeza wigo wa utoaji huduma, AICC inategemea kukopa kiasi cha Shilingi bilioni 2.12 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa upanuzi wa Hospitali ya AICC baada ya kupata kibali cha Wizara ya Fedha na Mipango. Kituo pia kinaendelea kufanya taratibu za kuwezesha kujengwa Kituo mahsusi cha mikutano kitakachoitwa Mt. Kilimanjaro International Convention Centre (MK-ICC). Kituo hicho ndicho kitakuwa suluhisho sahihi la mahitaji ya mikutano ya kimataifa na maonesho hapa nchini. Vilevile, Kituo kinaendelea na mchakato wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha mikutano Dodoma.
226.      Mheshimiwa Spika, baada ya Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (UN-ICTR) kufunga shughuli zake na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuhamishia baadhi ya shughuli zake katika jengo lao jipya, kwa sasa Kituo cha AICC kina nafasi ya kutosha kuweza kupokea taasisi nyingine za Kitaifa na Kimataifa.  Hivyo, ninatumia nafasi hii kukaribisha taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zitakazopenda kuweka makao yao Jijini Arusha kutumia nafasi hizo za ofisi zilizo wazi.
Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika
227.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania (APRM Tanzania) kwa mujibu wa miongozo ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kama ifuatavyo:
             i.        Kushiriki katika Mkutano wa Bunge la Afrika uliojadili Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika uliofanyika Sharm el Sheikh, Misri mwezi Oktoba 2016.  Katika Mkutano huo, Wajumbe walieleza kuridhishwa kwao na hatua zilizofikiwa na Tanzania katika kudumisha amani na utulivu, kulinda haki za binadamu, kudumisha Muungano, maendeleo ya kiuchumi, matumizi ya lugha moja ya Kiswahili na utoaji wa huduma muhimu za kijamii. APRM Tanzania pia ilipata fursa ya kueleza hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zilizobainishwa kwenye ripoti hiyo;
           ii.        Kusimamia utekelezaji wa mpango wa kuondoa changamoto za utawala bora zinazoihusu nchi yetu zilizobainishwa kwenye Ripoti ya APRM. Mkazo umewekwa katika kukamilisha ripoti ya utekelezaji wa mpango huo kwa upande wa Zanzibar ili kupata ripoti moja ya nchi itakayowasilishwa kwenye Kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika;
          iii.        Kushiriki katika Mkutano wa kutafuta Wajumbe Wapya wa Jopo la Watu Mashuhuri la Mpango wa Afrika wa Kujitathmini katika Utawala Bora uliofanyika Cape Town, Afrika Kusini mwezi Novemba 2016. Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Balozi Ombeni Yohana Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu alichaguliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Jopo hilo.  Wajumbe wengine waliochaguliwa wanatoka katika nchi za Algeria, Misri, Nigeria na Msumbiji;
          iv.        Kutoa taarifa kwa wananchi  kuhusu matokeo ya tathmini ya utawala bora kwa nchi yetu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na pia kwa kutumia majukwaa mengineyo; na
            v.        Kuisaidia Serikali kuimarisha Mfumo wa Kujitathmini Kiutawala Bora.

 

CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017 NA NAMNA YA KUZIPATIA UFUMBUZI

228.      Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17, zipo changamoto mbalimbali ambazo Wizara imekabiliana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yake. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na kutumia fedha nyingi za bajeti kugharamia pango kwa ajili ya ofisi na makazi balozini; Kasi ndogo ya ubadilishaji wa Sheria za nchi ili kuendana na matakwa ya Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki; Kasi ndogo ya sekta binafsi kutumia fursa za biashara na uwekezaji zitokanazo na Mtangamano wa Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa; na uelewa mdogo wa Watanzania kuhusu masuala ya Mtangamano.
229.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizi Wizara inaendelea kutekeleza mpango wake wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi Balozini kwa kutumia fedha za bajeti ya maendeleo zinazotolewa na Serikali na kwa kushirikisha Mifuko ya Uwekezaji iliyopo nchini katika kutekeleza baadhi ya miradi yake ya maendeleo; kuruhusu kasi ya ubadilishaji sheria za nchi ili ziendane na matakwa ya Itifaki ya Soko la Pamoja; na kuzihimiza Taasisi za Serikali kutoa kipaumbele na kuongeza kasi ya ubadilishaji wa sheria zilizoainishwa ili kuwawezesha Watanzania kunufaika ipasavyo na fursa za Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda.
230.      Mheshimiwa Spika,kwa kutambua umuhimu wa kipekee wa kutoa  elimu kwa Umma wa Watanzania juu ya fursa zinazotokana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa ambazo Tanzania ni mwanachama, Wizara imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali za fursa zinazopatikana nje ya mipaka ya Tanzania. Kwa muktadha huu,Wizara imeendelea kutumia vyombo vya habari vya umma, binafsi na vya kimataifa kama vile TBC1, Capital,  Clouds, Radio One, BBC, CGTN, VoA, RFI, DW na Bloomberg kutoa Elimu kwa Umma kuhusu fursa zinazotokana na Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Aidha, Wizara imeendelea pia kutumia machapisho, Tovuti yake na Mitandao ya kijamii kama vile Tweeter na Blog ili kuweza kuwafikia wadau wengi zaidi.
231.      Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mawasiliano baina ya Wizara na wadau wake, Wizara ilianzisha utaratibu wa kuzungumza na Waandishi wa Habari kila wiki. Malengo  ya mikutano hii ni kuueleza umma masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Wizara ikiwemo maazimio yanayofikiwa kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa na kikanda, ziara za viongozi wanaotembelea nchini na pia kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu Wizara. Jumla ya mikutano 70 kati ya Wizara na Waandishi wa Habari kutoka vyombo vyote vya habari ilifanyika ndani ya mwaka huu wa fedha.
232.      Mheshimiwa Spika, ni matumaini yangu kuwa juhudi hizi zitapanua uelewa wa Wananchi kuhusu utendaji wa Wizara kwa ujumla pamoja na kuwahamasisha kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya mbalimbali za kikanda na Kimataifa.

 

MALENGO YA WIZARA KWA MWAKAWA FEDHA 2017/2018

233.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, pamoja na mambo mengine, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu yake kama ifuatavyo:
             i.        Kutangaza mazingira mazuri ya nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa;
           ii.        Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi wahisani, mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo;
          iii.        Kuendelea kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali katika kuvutia wawekezaji na watalii, kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko;
          iv.        Kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
            v.        Kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi mbalimbali wa kitaifa;
          vi.        Kuendelea kusimamia balozi zetu katika kutekeleza majukumu ya uratibu hasa kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu;
        vii.        Kuendelea kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo;
       viii.        Kuongeza uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Konseli Kuu na kuendelea kununua, kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya makazi na ofisi za Balozi kwa kadri hali ya fedha itakavyoruhusu;
          ix.        Kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi ya Taifa letu;
           x.        Kuendelea kutetea na kusimamia maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali zilizotoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini. Kwa mfano, ahadi za G8 na ile ahadi ya kila nchi tajiri kutoa asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kwa nchi zinazoendelea na kutoa asilimia 0.2 ya pato lake kwa nchi maskini sana duniani kama msaada;
          xi.        Kuendelea kutambua jumuiya za watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa;
        xii.        Kuratibu maandalizi na kushiriki kwenye majadiliano katika mikutano ya Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mikutano ya Vikundi Kazi na Wataalam;
      xiii.        Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Afrika Mashariki, miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki;
       xiv.        Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika kuelekea kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
        xv.        Kuratibu zoezi la mapitio ya Sheria za Tanzania ili kuwezesha Watanzania kunufaika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
       xvi.        Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na COMESA na SADC pamoja na Eneo Huru la Biashara la Afrika;
     xvii.        Kuratibu majadiliano kuhusu  maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi (reli, barabara, bandari, nishati, viwanja vya ndege na hali ya hewa) na kijamii (elimu, afya, mazingira, jinsia na watoto) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
   xviii.        Kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha katika biashara baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
      xix.        Kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki;
        xx.        Kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia mfumo wa Confederation;
      xxi.        Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Baraza la Usalama la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
     xxii.        Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa Afrika Mashariki;
   xxiii.        Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;
   xxiv.        Kutoa Elimu kwa Umma juu ya fursa zitokanazo na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
     xxv.        Kuratibu mapitio, utafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
   xxvi.        Kuratibu na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Taasisi ya TradeMark East Africa Wizarani, Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na sekta binafsi; na
  xxvii.        Kukamilisha kuandaa Sera Mpya ya Mambo ya Nje.

SHUKRANI

234.      Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru Mabalozi, Wawakilishi wa taasisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kupitia nchi zao katika kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
235.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kupata mafanikio makubwa kutokana na mchango wa wadau na washirika wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa, kikanda, kimataifa pamoja na sekta binafsi. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Algeria, Australia, Austria, Brazil, Canada, China, Cuba, Denmark, Finland, Hungary,  India, Italia, Ireland, Israel, Iran, Japan, Korea Kusini, Kuwait, Malaysia, Marekani, Malta, Misri, Morocco, New Zealand, Norway, Oman, Poland, Qatar, Saudi Arabia, Sweden, Singapore, Thailand, Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ureno, Urusi, Uswisi na Uturuki.
236.      Mheshimiwa Spika, vilevile, shukrani ziwaendee Umoja wa Ulaya, AfDB, African Capacity Building Facility, Benki ya Dunia, IAEA, IMF, Investment Climate Facility for Africa, UNDP na Mashirika mengine yote ya Umoja wa Mataifa, TradeMark East Africa, The Association of European Parliamentarians with Africa na WWF pamoja na Mifuko na Mashirika mbalimbali ya Misaada kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi.
237.      Mheshimiwa Spika, vilevile, tunapenda kutoa shukrani zetu kwa wadau mbalimbali ambao wameendelea kutujengea uwezo Wizarani ikiwemo kufanikisha uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Tunazishukuru Serikali za Kuwait na Oman kwa msaada wa magari; UNDP kwa vifaa vya mawasiliano; na Jamhuri ya Korea na Kuwait kwa msaada wa Kompyuta. Vilevile, Wizara inamshukuru Mheshimiwa Jasem Al-Najem Balozi wa Kuwait nchini, kwa utayari wake wa kuendelea kutusaidia katika maeneo mengine na Mheshimiwa Dkt. Lu Younqing Balozi wa China nchini kwa kuahidi kutoa fedha zitakazojenga nyumba ya Wageni Mashuhuri eneo la Chamwino hapa Dodoma.

 

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2017/2018

238.      Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu, kwa mwaka 2017/2018 Wizara imepangiwa bajeti ya kiasi cha Shilingi 150,845,419,000.00. Kati ya fedha hizo Shilingi 142,845,419,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
239.      Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Shilingi 133,424,290,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 9,421,129,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara. Kati ya fedha za Matumizi Mengineyo Shilingi 410,000,000.00 ni kwa ajili ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania, Shilingi 3,341,148,909.00 ni kwa ajili ya fedha za Mishahara na Matumizi Mengineyo ya Chuo cha Diplomasia na Shilingi 513,060,356.00 ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
240.      Mheshimiwa Spika, katika fedha za bajeti ya Maendeleo kiasi cha Shillingi 8,000,000,000.00 zilizopangwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Shilingi 1,815,527,215.00 zitatumika kukarabati jengo la ofisi na makazi ya watumishi, Ubalozi wa Tanzania Kampala; Shilingi 315,425,000.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya Balozi yaliyopo Kinshasa, DRC; Shilingi 477,293,775.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa ofisi ya Ubalozi na makazi ya watumishi, Ubalozi wa Tanzania Harare; Shilingi 373,320,000.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya Balozi, ubalozi wa Tanzania Beijing; Shilingi 534,682,500 ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi, Ubalozi wa Tanzania  Pretoria; Shilingi 593,300,000.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa nyumba za ubalozi zilizopo Ubalozi wa Tanzania  Lilongwe; Shilingi 508,420,000.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi Ubalozi wa Tanzania  Cairo; Shilingi 865,300,200.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini;   Shilingi 257,006,310.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la zamani la ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Washington DC, Shilingi 259,725,000.00 ni kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Balozi, ubalozi wa Tanzania Addis Ababa, Shilingi 195,943,440.00 ni kwa ajili ya ukarabati wa makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania Brussels; na Shilingi 1,804,056,560.00 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya ubalozi, Ubalozi wa Tanzania Muscat.
241.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara inatarajia kukusanya kiasi cha Shilingi 25,773,882,820.00 ikiwa ni maduhuli ya Serikali.

HITIMISHO

242.      Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu ya Wizara, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 150,845,419,000.00. Kati ya fedha hizo Shilingi 142,845,419,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.
243.      Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza.
244.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.