Follow by Email

Thursday, April 13, 2017

Balozi Asha-Rose Migiro awasilisha hati za utambulisho kwa Rais Michael D. Higgins wa Ireland

 Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dkt Asha-Rose Migiro mapema mwezi huu aliwasilisha hati za utambulisho (letter of credence) kwa Rais wa Ireland, Mhe. Michael D. Higgins.

Akiwasilisha hati hizo katika Ikulu ya Ireland, Balozi Migiro alimfikishia Rais Higgins salamu za Mhe. Rais John Magufuli na wananchi wa Tanzania pamoja na kumuahidi kufanya kazi itakayoimarisha uhusiano wa kihistoria baina ya Serikali za Tanzania na Ireland pamoja na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dkt Asha-Rose Migiro  akimkabidhi Rais Michael D. Higgins hati ya utambulisho kutoka kwa Mhe.Rais John Pombe Magufuli. 
Mhe. Balozi Migiro akikagua gwaride rasmi lililoandaliwa na kikosi cha Jeshi la Anga la nchi hiyo.
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na Ireland, Dkt. Asha-Rose Migiro  akiagana na Rais Higgins.
Mhe. Migiro  alitumia fursa hiyo pia kukutana na kuzungumza na wanadiaspora wa Tanzania waishio katika miji mbalimbali ya Ireland ambapo waliweza kujadili masuala mbalimbali kwa ajili ya ujenzi na maendeleo ya Taifa, hususan masuala ya uwekezaji na kutumia nafasi walizopata kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza fursa zilizopo nchini sambamba na kudumisha utumaduni wetu.Pia Balozi Migiro aliwasihi wanadiaspora kushikamana, kuwa wamoja na kuunda Jumuiya ya Watanzania waishio Ireland akiwakumbusha kauli ya wahenga isimayo kuwa 'Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu'.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.