Follow by Email

Friday, March 31, 2017

Tanzania na Ethiopia zakubaliana kukuza ushirikiano

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa Mkutano wa Pamoja kati yake na Waziri Mkuu wa Shirikisho la Kidemokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn (aliyeketi kulia) na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya ushirikiano kati yao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Susan Kolimba (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Mhe. Workneh Gebeyehu wakisaini Mkataba wa Ushirikiano na ule wa kuanzisha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
==================================================== 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameeleza kuwa ziara ya siku mbili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Hailemariam Dessalegn nchini Tanzania ni ya mafanikio makubwa kwa nchi zote mbili.
Rais Magufuli amesema kuwa amejadiliana mambo mengi yenye faida kubwa na mgeni wake huyo walipokuwa katika mazungumzo ya faragha na rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
“Tumezungumza na kukubaliana takriban masuala 13 ambayo yatakapotekelezwa yatakuwa na faida kubwa kwa pande zote mbili.” Rais Magufuli alisema.
Masuala hayo ni pamoja na ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ambapo  Shirika la Ndege la Ethiopia litashirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo na matengenezo ya ndege.
Shirika hilo la Ethiopia ambalo kwa sasa lina ndege takriban 96 zinazofanya kazi na nyingine 42 zipo katika mchakato wa ununuzi limepanga pia kufungua kituo kikubwa kuliko vyote Barani Afrika cha kuhifadhi mizigo hapa nchini. Mizigo hiyo ambayo itapokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam na kusambazwa nchi husika kupitia Shirika la Ndege la Ethiopia.  
Masuala mengine yaliyoafikiwa ni pamoja na kushirikiana katika uwekezaji wa viwanda vya ngozi, nyama, na maziwa kwa kuwa Tanzania na Ethiopia ni moja ya nchi zenye mifugo mingi Barani Afrika.
Viongozi hao pia walizungumzia matumizi ya maji ya Mto Nile na kusisitiza kuwa matumizi ya maji hayo lazima yanufaishe nchi zote. Kwa kuzingatia hilo Tanzania imeipongeza Ethiopia kwa kujenga Bwawa la Gilgel Gibe la kuzalisha umeme wa MW 1870 pamoja na bwawa kubwa kabisa Barani Afrika la The Grand Ethiopian Renaissance ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha MW 6400 litakapokamilika.
Ethiopia imeahidi kuiuizia Tanzania MW 400 kwa bei nafuu kabisa. Rais Magufuli alisema mpango huo utakapokamilika utatoa ushindani kwa TANESCO kwa kuwa bei za umeme wa shirika hilo zipo juu kidogo. Kwa sasa umeme unaozalishwa Tanzania hauzidi MW 1500.
Aidha, Mhe. Dessalegn ameahidi kutuma wataalamu wake nchini kuja kufanya utafiti wa maeneo ambayo Tanzania inaweza kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme kama huo.
Ili kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, Serikali ya Ethiopia imepanga kufungua Ubalozi hivi karibuni mjini Dodoma ambapo Rais Magufuli ameahidi kutoa eneo bure kwa ajili ya ujenzi. 
Sanjari na hayo, Mhe. Dessalegn ameahidi kukiendeleza Kiswahili ambapo atachagua chuo kikuu kimoja nchini Ethiopia kifundishe somo hilo. Kwa upande wake Rais Magufuli ameahidi kutoa walimu wa kufundisha somo la Kiswahili katika chuo kitakachochaguliwa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia alieleza kuwa Tanzania na Ethiopia zina uzoefu wa kutosha, hivyo zikishirikiana katika uzoefu huo zitaendelea kiuchumi bila ya kuzishirikisha nchi nyingine. 
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza sekta zitakazotoa ajira kwa wingi kwa vijana ambao ni takriban asilimia 70 ya watu wote. Alitoa mfano wa sekta hizo kuwa ni pamoja na kilimo ambayo ikiendelezwa vizuri itapunguza umaskini kwa kiasi kikubwa kwa wananchi.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
31 Machi, 2017


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.