Follow by Email

Thursday, February 23, 2017

Rais wa Uganda kufanya ziara ya siku mbili nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu ziara ya siku mbili ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni atakayoifanya hapa nchini tarehe 25 na 26 Februari, 2017.Kulia ni Balozi Innocent Shiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na kushoto ni Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizarani.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Suleimani Seleh (wa kwanza kushoto) akifuatilia kwa makini mkutano wa waandishi wa habari na Waziri Mahiga.Kulia ni sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo.
Juu na chini ni sehemu ya waandishi wa habari wakiendelea kumsikiliza Waziri Mahiga (hayupo pichani) .
Mkutano na Waandishi wa habari ukiendelea 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 


Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Uganda nchini


Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kufanya ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini tarehe 25 na 26 Februari 2017 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. 

Mhe. Rais Museveni anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 25 Februari, 2017 majira ya asubuhi  na atapokelewa na Mhe. Dkt Magufuli pamoja na Viongozi wengine wa Serikali. 

Madhumuni ya  ziara hiyo ni kukuza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Uganda na Tanzania pamoja ‎na kujadili masuala mbalimbali ya kikanda, kimataifa na maeneo ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili hususan katika maeneo ya Biashara, Nishati, Uchukuzi na yale yanayohusu ujirani mwema.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Museveni  atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mazungumzo ya faragha yatakayofuatiwa  na mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili. 

Pia, Mhe. Rais Museveni na ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mhe. Rais Magufuli.
Siku ya pili, tarehe 26 Februari, 2017, Mhe. Rais Museveni atatembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Viwanda vya Kampuni ya Said Salim Bakhresa ambaye amewekeza pia nchini Uganda na baadaye Bandari ya Dar es Salaam.

Mahusiano ya Uganda na Tanzania

Mahusiano ya Tanzania na Uganda ni mazuri na yamekuwa yakiimarika kila mara. Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa ukaribu sana katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisisasa, kiusalama, kijamii na kikanda hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia kumekuwepo ziara za mara kwa mara za viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi hizi mbili ikiwemo ziara ya Rais Uganda, Mhe. Museveni ambaye alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Rais Magufuli zilizofanyika mwezi Novemba, 2015. Aidha, Rais Magufuli pia alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Rais Museveni mwezi Mei, 2016.

Mahusiano katika Sekta ya Biashara

Mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Uganda yameendelea kuimarika katika miaka ya hivi karibuni. Katika kipindi cha mwaka 2016 yalikuwa ni mazuri ambapo Tanzania iliweza kufanya mauzo (exports) ya kiasi cha Shilingi bilioni 126.744 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 99.882 mwaka 2015. Mauzo ya Uganda nchini Tanzania (imports) kwa mwaka 2016 yalikuwa ni Shilingi bilioni 66.849 bilioni ikilinganishwa na Shilingi 78.31 mwaka 2015.

Aidha, nchi ya Uganda ina umuhimu mkubwa kwa Tanzania kutokana na jiografia yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwa nchi jirani tunayopakana nayo. Uganda ni nchi isiyokuwa na bandari (landlinked country) hivyo inaitegemea Tanzania kwa ajili ya kupitisha mizigo yake. 

Nchi hiyo imezidi kuwa na umuhimu kufuatia uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta nchini Tanzania, kutoka Kabaale-Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga. Bomba hili litakuwa na urefu wa kilomita 1443 na kipenyo cha inchi 24. Mradi wa ujenzi wa Bomba hili unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2020.

Utekelezaji wa mradi huu unategemewa kuwa na faida nyingi kwa taifa ikiwemo kufungua fursa za ajira kwa Watanzania, kuchochea shughuli za kiuchumi kwa mikoa bomba hilo litakapopita,  kufungua ukanda wa biashara wa kaskazini mwa Tanzania na Uganda  na kuimarisha uhusiano katika soko la Afrika Masahariki.

 Ushirikiano kupitia Tume ya pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Uganda

Mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda ulisainiwa Kampala, Uganda tarehe 13 Machi, 2007. Mkataba huo unaainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano ambayo yalipaswa kutekelezwa kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC). Maeneo yaliyoainishwa ni pamoja na Miundombinu, Viwanda, Biashara, uwekezaji, Nishati, Utalii, Kilimo, Uvuvi, Mazingira, Ulinzi na Usalama.

Ushirikiano katika jitihada za usuluhishi wa Mgogoro wa Burundi

Jitihada za usuluhishi wa mgogoro nchini Burundi zinaendelea vizuri. Mhe. Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa usuluhishi wa mgogoro huo kwa kushirikiana na Rais Msataafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni Mwezeshaji wa mazungumzo ya upatanishi wamekuwa wakifanya jitihada za dhati za kurejesha amani nchini Burundi. 

Mhe. Rais Museveni na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini tarehe 26 Februari, 2017.

-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 23 Februari, 2017
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.