Follow by Email

Saturday, February 25, 2017

Rais Museveni awasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili


Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli akimkaribisha nchini Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa cha Julius Nyerere tayari kwa kuanza ziara ya siku mbili hapa. Katika ziara hiyo Mhe. Museveni anatarajiwa kufanya mzungumzona mwenyeji wake Magufuli pamoja na kutembelea Kiwanda cha Azam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kushoto) akiwa  na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Kassim Majaliwa (katikati) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) wakati wa mapokezi ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Museveni
Rais Museveni pamoja na mwenyeji wake Rais Dkt. Magufuli wakisikiliza nyimbo za mataifa yao
Makamu wa Rais akiwa uwanja wa ndege na Viongozi mbalimbali wa ngazi za juu Serikalini wakati wa mapokezi ya Rais Museveni.
Rais Museveni pamoja na Rais Magufuli wakitizama moja ya kikundi cha ngoma kilichokuwa kikitoa burudani uwanjani hapo.
Rais Yoweri Kaguta Museveni pamoja na Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakizungumza jambo.
===================================================
 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 


Tanzania na Uganda sio nchi rafiki tu bali ni ndugu wa kweli lakini Kiwango cha biashara kati ya nchi hizo hakitafsri ipasavyo ukubwa wa udugu na urafiki uliopo kati ya yao. 

Hayo yalibainishwa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam akiwa na Mgeni wake Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni. 

Rais Museveni yupo nchini Tanzania kwa ziara ya Kiserikali ya Siku mbili kuanzia tarehe 25 hadi 26 Februari 2017.

“Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Shilingi bilioni 126.744 mwaka 2016 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya Shilingi bilioni 99.882 zilizouzwa mwaka 2015”. “Hiki ni kiwango kidogo sana ukilinganisha na udugu mkubwa tulionao kati ya nchi zetu mbili”alisema Dkt. Magufuli.

Rais Magufuli alieleza kuwa ili kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili, Serikali yake imeanza mkakati wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam-Mwanza-Isaka hadi Burundi na Rwanda. Rais Magufuli alisema pia kuwa Serikali itajenga Bandari Kavu jijini Mwanza ili kuwarahisishia wafanyabiashara wa Uganda kuchukulia bidhaa zao Mwanza badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam. 

Sanjari na hayo Serikali itaboresha bandari ya Bell na itapunguza vizuizi vya barabarani na kubaki vitatu ili kupunguza muda mwingi unaopotezwa na malori ya mizigo kwenye vizuizi hivyo.

Kuhusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima hadi Bandari ya Tanga, Rais Magufuli alisema Serikali yake ilishafanyia kazi vikwazo vyote saba vilivyowasilishwa ikiwemo kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kutoa mwito kwa mwekezaji kuanza ujenzi wa bomba hilo haraka kwani hakuna kisingizio kingine. Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa kupanga tarehe ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa bomba hilo  na kwamba yupo tayari kusafiri kwenda nchini Uganda kama itakubalika jiwe hilo kuwekwa nchini humo. 

Aidha, Rais Magufuli alizungumzia jitihada za Serikali yake kufufua Shirika la Ndege la ATCL kwa kununua ndege sita kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga nchini na nchi jirani. Alimuomba Rais Museveni muda utakapofika ndege hizo ziweze kwenda Uganda jambo ambalo liliafikiwa.

Akizungumzia Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Umoja wa Ulaya (EPA), Rais Magufuli aliuona mkataba huo kama kikwazo katika juhudi za Serikali za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020. Hivyo alimuomba Rais Museveni kumuunga mkono kuepuka mkataba huo kwa manufaa ya wananchi wa EAC.

“Rais Museveni alibebwa na Tanzania wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo namuomba Rais Museveni naye anibebe katika suala hili la EPA kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu na Jumuiya yetu” alisisitiza Rais Magufuli. 

Kwa upande wake, Rais Museveni alibainisha kuwa, hadi leo tatizo kubwa kwa Bara la Afrika lililopelekea hadi kutawaliwa na wakoloni huko nyuma ni ukosefu wa umoja na msimamo wa pamoja.  Alisema amekuja Tanzania kujadiliana na Rais Magufuli ili kupata msimamo wa pamoja kuhusu Mkataba wa EPA wenye manufaa kwa wananchi kwani undugu na umoja  uliopo kati ya nchi hizi mbili ni zaidi ya mkataba huo.

Kuhusu mpango wa Tanzania kujenga reli ya kiwango cha kimataifa, Rais Museveni aliupongeza mpango huu na kuutaja kama mchango wa pili wa Tanzania katika ukombozi wa Uganda. Alisema reli hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa uchumi wa Uganda kwa kuwa utakuwa ni usafiri wa haraka na gharama nafuu.

Rais Museveni kabla ya kuondoka nchini kesho tarehe 26 Februari 2017 atatembelea kiwanda cha AZAM kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam. AZAM pia imefanya uwekezaji nchini Uganda.  


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam, 25 Februari, 2017
No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.