Follow by Email

Thursday, December 1, 2016

Mkutano wa ushirikiano kati ya Afrika na Jamhuri ya Korea kufanyika Addis Ababa

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari. Katika mkutano huo Bi. Kasiga aliwaeleza Waandishi wa Habari kuhusu Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa nchi za Afrika na Korea utakaofanyika Mjini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba, 2016. Mkutano huo utajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Afrika na Korea pamoja na maeneo mapya ya mashirikiano.
Afisa Mambo ya Nje, Bi. Bertha Makilagi akifuatilia mkutano kati ya Bi. Kasiga na Waandishi wa Habari. Wengine ni Waandishi wa Habari waliohudhuria mkutano huo.
Sehemu ya Waandishi wa Habari wakisikiliza na kunukuu kwa makini mkutano uliokua ukiendelea
Mkutano ukiendeleaTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Korea ujulikanao kama Korea-Africa Ministerial Forum unaotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza Barani Afrika, Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba, 2016. Mikutano mitatu ya kwanza ilifanyika Seoul, Korea mwaka 2006, 2009 na 2012.

Mkutano huu ambao umeandaliwa na Serikali ya Korea kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika una lenga kukuza ushirikiano pamoja na kuandaa maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Korea na mataifa ya Afrika katika miaka mitatu ijayo.

Tanzania ni moja ya nchi nne (4) za Afrika ambazo Korea imezichagua kuanzisha mahusiano ya kimkakati “strategic partnership” yatakayozifanya nchi hizo kupewa kipaumbele katika kupokea misaada na mikopo nafuu kutoka Korea katika kipindi cha miaka mitano ijayo kati ya 2016 hadi 2020.
Katika kipindi hicho, Tanzania itapokea kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 300 ikiwa ni asilimia 17.1 ya msaada utakaotolewa Barani Afrika, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza Barani Afrika kupokea misaada kutoka Jamhuri ya Korea. Nchi nyingine ni Msumbji, Ethiopia na Angola.
Msaada huo unategemea kufadhili miradi katika sekta za umeme, viwanda na TEHAMA. 

Sanjari na Mkutano huo, ujumbe wa Tanzania utafanya mkutano wa pande mbili na ujumbe wa Serikali ya Korea kuzungumzia masuala ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili. Tanzania itatumia fursa hiyo kuiomba Korea kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mipya ikiwemo mradi wa Daraja la Selander ambao unatarajiwa kuanza mwaka 2017 na kukamilika 2020.
Aidha, ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa Afrika na Korea ni fursa muhimu ya kukuza mahusiano baina ya nchi zetu mbili hususan katika Nyanja ya uchumi. Serikali ya Korea ilitoa ahadi ya kuongeza uwekezaji Barani Afrika hususan katika sekta za nishati, miundombinu na viwanda. 

 Miradi ambayo Tanzania imefaidika tokea kuanzishwa mikutano hii mwaka 2006 ni pamoja na mradi wa kuendeleza kilimo cha Mwani Zanzibar wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.6 na Awamu ya Pili ya Mradi wa Huduma ya Uchunguzi wa Afya ya Uzazi Jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni nne (4).

Miradi mingine ambayo Jamhuri ya Korea imeshirikiana na inaazimia kushirikiana na Tanzania ni:-
·        Ujenzi wa Mradi wa Daraja la Kikwete kwenye Mto Malagarasi Mkoani Kigoma ambao umekamilika; Ujenzi wa Hospitali ya Kimataifa iliyopo eneo la Mloganzila; Dar es Salaam   na Hospitali ya Mama na Mtoto iliyopo Chanika, Dar es Salaam.

·        Kadhalika, hivi karibuniTanzania imesaini
o   Makubaliano ya kupanua miundombinu ya Majitaka jijini Dar es Salaam; na
o   Makubaliano ya kutekeleza miradi utakaofadhiliwa kwa pamoja na benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Jamhuri ya Korea.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 01 Desemba, 2016.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.