Follow by Email

Saturday, November 26, 2016

Makamu wa Rais Mhe. Samia Hassan azindua majengo ya Umoja wa Mataifa (MICT)


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Taasisi mpya ya kimataifa MICT(Mechanism for International Criminal Tribunals) ambayo imechukua majukumu ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR). 

 Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 25 Novemba, 2016 katika eneo la Lakilaki nje kidogo ya Jiji la Arusha na kuhudhuriwa na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, Viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwa upande wa Jiji la Arusha  pamoja na sehemu ya wakazi wa Arusha.
Rais wa Taasisi ya MICT (Mechanism for International Criminal Tribunal), Jaji Theodor Meron akihutubia wageni waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya Kisasa ya MICT.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt. Augustine Mahiga (Mb), akiwasalimia wageni waalikwa pamoja na kumkaribisha rasmi Makamu wa Rais Mhe. Mama Samia ili aweze kuhutubia wageni waalikwa. Pamoja na salamu Mhe. Waziri alieleza eneo lililotengwa na Serikali kwaajili ya Taasisi za Kimataifa lina ukubwa wa ekari 430 ambapo ekari 16 zimegaiwa kwa MICT na mpaka sasa zimeshatumika ekari tano tu katika ujenzi wa majengo ambayo yalifanyiwa uzinduzi.
Mhe. Makamu wa Rais akizindua rasmi majengo ya MICT tayari kwa kuanza kutumika. Walioko nyuma kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt. Augustine Mahiga na  Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sheria Bw. Miguel de Serpa Soares .
Mhe. Makamu wa Rais akizungumza wa wakandarasi wa kitanzania ambao walishinda zabuni ya kujenga majengo ya kisasa ya MICT.
Mhe. Mama Samia akitembelea jengo la kuhifadhia nyaraka ambalo litakuwa na huduma tatu ambazo ni pamoja na Maktaba ya sheria; chumba cha kuhifadhia nyaraka kinachoonekana katika picha kinahudumu katika nyuzi joto 24 lilonashauriwa kitaalamu kuhifadhi nyaraka hizo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt Aziz Mlima akipokea ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Celestine Mushy walipotembelea jengo la Mahakama.

Msajili wa MICT, Bw. John Hocking akitoa maelezo kwa Mhe. Makamu wa Rais alipotembelea katika jengo la Mahakama na kupewa ufafanuzi juu ya mpangilio wa kukaa mahakamani hapo wakati kesi zitakapoanza kusikilizwa.
Mhe. Makamu wa Rais akipanda mti katika eneo la majengo ya MICT katika kuhifadhi mazingira.

Mhe. Waziri Mahiga akipanda mti mbele ya jengo la utawala, pembeni yake ni Msaidizi wake Bw. Gerald Mbwafu na Afisa wa MICT.


Mhe. Mama Samia akimkabidhi zawadi Bw. Hocking ikiwa ni pongezi kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kusimamia ujenzi huo. Pia Bw. Hocking amemaliza muda wake wa kuhudumu MICT nchini.

Wazee wa kimila kutoka kabila la Wamasai, wenyeji wanaoishi jirani na Taasisi ya MICT katika vilima vya Lakilaki wakiombea baraka eneo la MICT kabla ya zoezi rasmi la uzinduzi.
Kutoka kulia ni Katibu Mkuu, Balozi Dkt. Aziz Mlima, Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Tuvako Manongi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mushy wakifuatilia hotuba ya Mhe. Makamu wa Rais.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Baraka Luvanda akifuatilia hotuba.


Wa pili kulia ni Bw. Gerald Mbwafu, Bi. Blandina Kasagama na Bi. Sekela Mwambegele maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya uzinduzi.

Picha ya pamoja ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais wa MICT, Mabalozi kutoka Wizarani na viongozi wengine wa MICT pamoja na Mkandarasi wa majengo ya MICT.

Makamu wa Rais akiwa katika picha ya pamoja meza kuu, kutoka kushoto ni John Kocking (Msajili MICT), Theodor Meron (Rais wa MICT), Miguel de Serpa Soares (Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sheria), kulia ni Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ( Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Mhe. Mrisho Gambo (Mkuu wa Mkoa wa Arusha), Serge Brammertz (Mwendesha Mashitaka MICT) na Jaji Mohamed Chande Othman (Jaji Mkuu).

Picha ya Pamoja meza kuu na wawakilishi kutoka Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa.

Majengo yaliyozinduliwa, kutoka kushoto ni Mahakama, Jengo la Utawala na kulia ni jengo la kuhifadhia nyaraka ambalo ndani yake lina maktaba.
Mti wa asili unaowakilisha amani (Christmas Tree) ambao ulikuwa umekauka  katika eneo la mradi umefanyiwa jitihada za makusudi za kuhudumiwa ili uweze kuota tena.
==========================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia     Suluhu Hassan amezindua majengo  ya Taasisi mpya ya Kimataifa MICT ambayo inachukua majukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR). Uzinduzi huo umefanyika tarehe 25 Novemba, 2016 katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha. 

Taasisi hiyo mpya ijulikanayo kama Mfumo wa Kimataifa wa kumalizia Mashauri Masali (international Residual Mechanism for Criminal Tribunal)  ya iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR)  imejengwa katika eneo la Lakilaki  nje Kidogo ya Jiji la Arusha.

Pamoja na kuendesha Mashauri Masalia ambayo hayakukamilika baada ya Mahakama ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda kumaliza muda wake,  pia taasisi hiyo itahifadhi nyaraka pamoja na kutoa huduma ya maktaba bure kwa umma hususan katika taaluma ya Sheria ambapo imefanikisha kuanzisha makataba kubwa ya Mfano ya Sheria za Kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mhe. Samia alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) katika kuhakikisha Taasisi hiyo mpya inafanya kazi zake kwa tija ikiwa pamoja na kusimamia Haki za Binadamu, Utawala wa Sheria pamoja na usawa wa jinsia katika nafasi zote unapewa kipaumbele nchini.

“Aidha napenda nimshukuru Msajili wa Taasisi ya MICT,  Bw. John Hocking ambaye siku zote ameendelea kujitoa kwa hali na mali katika kusimamia ujenzi wa mradi huu na kuhakikisha unakamilika na kuanza kazi kwa wakati, pamoja na wafanyakazi wote wa MICT” alisema Mhe. Samia.

Aidha, Rais wa MICT Jaji Theodor Meron aliishukuru Serikali ya Tanzania hususan Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao walikuwa waratibu wakuu katika ufuatiliaji na usimamizi wa mradi sambamba na Taasisi nyingine za Umma kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Jiji la Arusha kwa ujumla, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Shirika la Simu Tanzania (TTCL).

Halikadharika alitoa shukrani za pekee kwa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu  Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa ushirikiano waliotoa katika kufanikisha kukamilika kwa mradi.
 
Jaji Theodor pia alieleza majengo ya Taasisi ya MICT yamejengwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 8.78 fedha za nchi wanachama za Umoja wa Mataifa na kwamba ardhi kwaajili ya ujenzi ilitolea bure na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na huduma nyingine zilizokuwa zikiambana na ujezi huo kama maji, umeme, matengenezo ya barabara katika kiwango cha lami ambayo imeitwa "barabara ya haki", huduma ya mtandao na vifaa vya kujengea ambavyo ni rasilimali ya Tanzania na pia ujenzi huo umetumia mkandarasi mzawa kutoka nchini Tanzania. 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga ameshukuru Shirika la umoja wa Mataifa kwa maamuzi yake mazuri ya kuipa Tanzania heshima ya kuwa mwenyeji wa Taasisi hiyo na akasema Serikali ya Tanzania itahakikisha haki inasimamiwa katika kesi za kimataifa na akakaribisha mashirika mengine ya Kimataifa kuja kujengwa nchini Tanzania. Pia kwa wale wanaofanya tafiti kuhusiana na Taasisi nyingine za kimataifa ni mahali sahihi kwaajili ya kufanikisha tafiti zao.

Mwaka 2010 Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha Azimio nambari 1966 la kuanzisha Mfumo wa Kimataifa utakaomalizia mashauri ya Masalia kwa iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) yaliyotokea mwaka 1994 na Mauaji ya Halaiki yaliyotokea katika iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani (ICTY).  Katika azimio hilo Baraza kuu lilibainisha wazi kwamba Arusha itakuwa makao  makuu ya Tawi hilo jipya la MICT na The Hague kuwa makao makuu ya Tawi Jingine.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.