Follow by Email

Sunday, July 10, 2016

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ampokea Waziri Mkuu wa India

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli akimpokea Waziri Mkuu wa India Mhe.  Narendra Modi mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Ikulu Jiji Dar es Salaam. Mhe. Modi yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili inayotarajiwa kumalizika leo.


Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi akikabidhiwa maua na mtoto Elizabeth Jackson mara baada ya kupokelewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amesimama na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi wakati nyimbo za Taifa zikipigwa mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu.
Mhe. Modi akikagua gwaride la heshima mara baada ya kumalizika kupigwa nyimbo za Taifa.
Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi akisalimiana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Mgeni wake Mhe. Modi wakipunga mkono kuwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki mgeni katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli na mgeni wake Mhe. Modi wakipiga ngoma kuashiria furaha, mshikamano na ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya mataifa yao.
Rais Mhe. Dkt John Pombe Magufuli akiongoza kikao kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam akiwa pamoja na mgeni wake Waziri Mkuu wa India na viongozi waandamizi wa Serikali za pande zote mbili. 
Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi akiongea katika Kikao na Waandishi wa habari ambapo alieleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na India na pia aliahidi Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano katika sekta ya Afya, Elimu, Maji na Teknolojia ya Habari, pamoja na kuzidi kuibua maeneo mapya ya ushirikiano. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dktr. John Pombe Magufuli akiongea katika kikao na Waandishi wa Habari, ambapo alisema Serikali ya Tanzania itazidi kuimarisha ushirikiano na Serikali ya India hasa katika masuala ya kiuchumi ili kuweza kuboresha maisha ya wananchi wa mataifa yao.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mhe. Modi mara baada ya kumaliza vikao na mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ziara ya Waziri Mkuu wa India nchini Tanzania


Serikali ya India imeahidi kuipatia Tanzania msaada wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020. 

Hayo yameelezwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mara baaada ya kufanya mazungumzo na mgeni wake, Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi. Mhe. Modi aliwasili nchini jana kwa ziara ya Kitaifa ya Siku mbili.


Rais Magufuli alieleza kuwa Tanzania na India zina uhusiano mzuri wa kihistoria ambao umekuwa na faida za kijamii na kiuchumi kwa pande zote mbili. Alitoa mfano namna India ilivyofadhili ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 178. 

Aidha, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya India kwa kuridhia kutoa kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 92 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kisiwani Zanzibar.  Rais Magufuli alielezea pia kuridhishwa na kiwango cha biashara kati ya Tanzania na India ambacho kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.

 Alisema kwa mwaka 2009, Tanzania iliiuzia India bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 187, kiwango hicho kimeongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.29 mwaka 2015.


Viongozi hao wakiwa katika mazungumzo rasmi, walikubaliana kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, viwanda, afya, nishati na madini.


Kwa upande wa Kilimo, Rais Magufuli alitoa wito kwa wakulima wa Kitanzania kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde hususan dengu kwa kuwa yana soko kubwa nchini India. Alisema India ni soko kubwa la  mazao hayo na imeahidi kusaidia pembejeo za kilimo ili kuongeza kiwango cha uzalishaji.


Kwa upande wa viwanda, mashirika ya viwanda vidogo ya India na Tanzania yamewekeana saini mkataba ambapo mashirika hayo yatafanya tathmini nchi nzima ya kubaini rasilimali zilizopo katika maeneo mbalimbali na aina ya viwanda vidogo vinavyoweza kuanzishwa kwenye maeneo hayo. Baada ya tathmini hiyo, Serikali ya India itatoa mkopo nafuu kwa ajili ya kujenga antamizi (incubators) za viwanda vidogo nchi nzima. Kupitia antamizi hizo, wananchi watapatiwa mafunzo maalum ya uzalishaji wa bidhaa, biashara na usimamizi wa fedha na baadaye kupewa mitaji kwa ajili ya kuanza shughuli za biashara.


Kwa upande wa sekta ya Afya, Rais Magufuli alimuomba Waziri Mkuu wa India kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza nchini katika uzalishaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba. “Nimemuomba Mhe. Modi na amekubali kuleta wawekezaji kuzalisha madawa na vifaa tiba hapa nchini. Hiyo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa matumizi ya fedha za kigeni kutokana na uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi. 

Sambamba na hilo, Rais Magufuli ameshukuru Serikali ya India kwa kuipatia Hospitali ya Bugando mashine maalum kwa ajili ya kupima ugonjwa saratani. Mashine hiyo inatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia sasa.


Kuhusu sekta ya nishati na madini, viongozi hao walikubaliana kushirikiana katika kuendeleza sekta hiyo hapa nchini. Tanzania ina utajiri mkubwa wa gesi asilia  ikiwemo Helium na madini. Hivyo ni vizuri tukishirikiana na wenzetu kuendeleza sekta hiyo.  


Rais Magufuli alihitimisha taarifa yake kwa kueleza kuwa wameazimia kushirikiana na India katika ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine, mabadiliko ya mfumo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanafanyika ili liwe na uwiano mzuri wa uwakilishi. Aidha, wameahidi kusaidiana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo ni tishio kubwa kwa maendeleo endelevu ya dunia ya sasa.


Waziri Mkuu wa India alikuwa katika ziara yake ya pili barani Afrika tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2014 ambapo alitembelea nchi za Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na atahitimisha ziara yake nchini Kenya.  


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Dar es Salaam, 10 Julai 2016.No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.