Follow by Email

Tuesday, June 21, 2016

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India akutuna na Waziri Mahiga.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) kulia akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa India, Bw. Amar Sinha alipokuja kumtembelea Ofisini kwake na Kufanya naye Mazungumzo kuhusu umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na India.
Mhe. Waziri akiwa katika mazungumzo na mgeni wake ambapo walijadili namna Tanzania na India zitakavyoweza kushirikiana katika sekta mbalimbali kama vile uwekezaji, elimu, afya, TEHAMA na ufundi.
Bw. Sinha akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo.
Mhe. Waziri akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India zawadi yenye picha za wanyama mbalimbali wanaopatikana katika hifadhi za taifa hapa nchini.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India akutuna na Waziri Mahiga.

Tanzania imetakiwa kujifunza kutoka India kufuatia maendeleo makubwa yaliyofikiwa na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali za viwanda,  teknolojia, TEHAMA, kilimo, usalama na afya. Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Bw. Amar Sinha ofisini kwake

Waziri Mahiga alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa ushirikiano wa Tanzania na India katika sekta ya uchumi unahitajika kwa kiasi kikubwa ili Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iweze kufikia malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025.

Alisema kuna umuhimu wa Tanzania na India kushirikiana kwa pamoja katika sekta za teknolojia, elimu, afya, elimu ya ufundi na TEHAMA ili kuiongezea uwezo Serikali iweze kufikia malengo yake yaliyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.

Mhe. Waziri aliishukuru Serikali ya India kwa misaada ya miradi ya maendeleo inayotoa kwa Tanzania. Misaada hiyo ni pamoja na ununuzi wa matrekta kwa ajili ya kuboresha kilimo wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 40 unaosimamiwa na SUMA-JKT.

Msaada mwingine ni ujenzi wa miundombinu ya maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam uliogharimu Dola za Marekani milioni 178.125. Aidha, India imekubali kusaidia ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika mikoa ya Shinyanga na Tabora utakaogharimu Dola za Marekani milioni 268.35 pamoja na mradi mwingine wa maji utakaogharimu Dola za Marekani milioni 92 utakaojengwa visiwani Zanzibar.

Awali, Bw. Sinha alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima. Wawili hao walisisitiza umuhimu wa nchi hizi mbili kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kwa ajili ya faida ya wananchi wa pande zote mbili. Maeneo waliyoyainisha ni pamoja na kilimo, mafuta na gesi, madawa, afya, madini na uchumi wa bahari (Blue economy).

Kuhusu uchumi wa Bahari, Balozi Mlima alieleza kuwa hilo ni suala ambalo Mhe. Rais Magufuli analisisitiza kila siku katika vikao mbalimbali. Alimuomba Katibu Mkuu huyo kuangalia uwezekano wa kusaidia kutafuta wawekezaji wa uvuvi kwenye Bahari Kuu nchini ambayo kwa kauli ya Rais bado haijafanyiwa kazi ipasavyo.

Kwa upande wake, Bw.Amar Sinha alisema kuwa ziara yake imelenga kuimarisha mahusiano ya kihistoria yaliyopo kati ya Tanzania na India pamoja na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano. Alisema India itaendelea kushirikiana na Tanzania na inafurahishwa na mchango inaotoa ambao unasaidia katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia 7 kila mwaka.   


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Juni 2016.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.