Follow by Email

Thursday, May 26, 2016

Tanzania na China kuendelea kuimarisha ushirikiano

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akiwaonyesha waandishi wa habari  kitabu kinachoelezea Historia ya Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye Mkutano na vyombo vya habari  uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano ambao  Bi. Kasiga aliwaelezea mafanikio ya ziara iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Aziz Mlima nchini China  ambapo  pamoja na kufadhili shughuli mbalimbali za kiuchumi, nchi hiyo pia imekubali kutoa ufadhili wa nafasi kumi za masomo ya kidiplomasia ambapo itatoa nafasi tano za  mafunzo ya muda mrefu na tano za muda mfupi kwa kila mwaka
Mkutano ukiendelea
==================================================================TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Kikazi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki nchini China

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Aziz Mlima alifanya ziara ya kikazi nchini China kuanzia tarehe 15 – 19 Mei 2016 kufuatia mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na China katika nyanja za siasa, uchumi na utamaduni.

Akiwa nchini China, Dkt. Mlima pamoja na mambo mengine alipata fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Makampuni makubwa ya China ambayo baadhi yao yameshawekeza nchini na mengine yameonesha dhamira ya kuwekeza.

Wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Zhang Ming, masuala mbalimbali yalijitokeza ikiwa ni pamoja na China kusisitiza dhamira yake ya dhati ya kukuza ushirikiano na Tanzania katika nyanja ya uchumi kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu. China imeweka kipaumbele cha juu katika miradi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo na eneo la viwanda pamoja na maboresho ya Reli ya TAZARA na ipo tayari kuanza upembuzi yakinifu wa Reli ya Kati. 

Kwa upande wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Kampuni ya China ya Merchant Holding International (CMHI) ambayo imeingia ubia na Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Oman kujenga bandari hiyo, wapo katika hatua nzuri ya kukamilisha mazungumzo ya ubia wao ili waanze awamu ya kwanza ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ndani ya mwaka huu wa 2016.
Kwa suala la ujenzi wa eneo la viwanda, Serikali ya China imebainisha kuwa ikwishatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu wezeshi (barabara, nishati ya umeme, maji, TEHAMA).

Kuhusu Reli ya TAZARA, China imeahidi kuwa itaendelea kuipa kipaumbele cha juu reli hiyo kwa sababu inabeba historia ya mahusiano yake na Afrika. China imeridhishwa na mazungumzo ya wataalamu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kuahidi kufanyia kazi yaliyokubalika ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kupitia Itifaki ya 16 kwa ajili ya maboresho makubwa ya miundombinu ya TAZARA pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye mikutano itakayofuata kuangalia namna bora ya kuendesha reli hiyo kwa ushirikiano na Tanzania na Zambia. 

Mkutano na Mamlaka ya Tumbaku

Katibu Mkuu alikutana na Kamishna wa State Tobacco Monopology, Bw. Lin Chengxing ambapo pamoja na mambo mengine walizungumzia utekelezaji wa Mkataba wa Kuruhusu Tumbaku ya Tanzania kuingia soko la China uliosainiwa mwaka 2013 wakati Rais wa nchi hiyo, Mhe. Xi Jinping alipofanya ziara nchini. Bw. Lin alijulisha kwamba makampuni mawili ya China-Hunan Industries na Shandong Industries yamepewa jukumu la kuinunua tumbaku ya Tanzania kwa ajili ya kufanya majaribio. 

Hadi hivi sasa wameshanunua tani 1500 ambazo zinahifadhiwa kwa kati ya miezi 24 hadi 30 (fermentation) kabla ya kutumika kuzalisha sigara. Matarajio yao ni kwamba sigara zitakazozalishwa na tumbaku ya Tanzania itaingia soko la China mwaka ujao. Endapo soko la China litapendelea sigara hizo, mahitaji ya tumbaku ya Tanzania katika soko la China yataongezeka kwa kiasi kikubwa. 

Mkutano na Chuo Kikuu cha Mambo ya Nje

Dkt. Mlima alikutana na Rais wa Chuo Kikuu cha Mambo ya Nje cha China, Prof. Qin Yaqing ambapo walijadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya chuo hicho na Chuo cha Diplomasia cha hapa nchini. Katika majadiliano hayo,  walikubaliana kushirikiana katika tafiti na utoaji wa mihadhara.  Aidha, Chuo hicho kimeahidi kutoa nafasi za masomo tano za muda mfupi na tano za muda mrefu kila mwaka kwa Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje. Chuo hicho kilianzishwa mahsusi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China na baadaye kilianzisha programu mbalimbali na kuchukua wanafunzi kutoka nje ya nchi. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 26 Mei 2016.
 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.