Follow by Email

Tuesday, March 22, 2016

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje afanya ziara Chuo cha Diplomasia

Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe.  Dkt. Susan Kolimba (Mb.) , akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Chuo cha Diplomasia wakati wa ziara yake Chuoni hapo. Chuo hicho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Balozi  Dkt. Mohammed Maundi (katikati) na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Taaluma Chuoni  hapo, Dkt. Wetengere Kitojo

Naibu Waziri akiangalia vitabu vilivyopo kwenye Maktaba ya Chuo hicho

Naibu Waziri akiwaeleza jambo uongozi wa chuo hicho.
Naibu Waziri akikagua Darasa la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Chuo cha Diplomasia
Dkt. Suzana Kolimba akizungumza na uongozi wa Chuo cha Diplomasia mara baada ya kumaliza kuzungukia eneo la Chuo cha Diplomasia
Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia naye akizungumza wakati Naibu Waziri alipotembelea Chuo hicho
Naye Mkurugenzi wa Taaluma, Dkt. Watengere Kitojo akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri
Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu Chuoni hapo Dkt. Charles Bekon akionesha  Mpango Mkakati wa Chuo cha Diplomasia ikiwemo mfano wa  michoro ya majengo ya Chuo.
 Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba akitazama sampuli ya michoro ya majengo yanayotarajiwa kujengwa Chuoni hapo
Dkt. Susan akisalimiana na Wakufunzi wa Chuo cha Diplomasia mara baada ya kuwasili Chuoni hapo.
Naibu Wizara Dkt. Suzan Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Chuo cha Diplomasia, wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia Dkt. Mohammed Maundi, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha Dkt. Achiula (wa pili kutoka kulia), Mkurugenzi wa Taaluma wa Chuo cha Diplomasia Dkt. Watengere Kitojo (wa kwanza kulia) na Mhasibu Mkuu Dkt. Charles Bekon. 


Picha na Reginald Philip

=========================================================================================================


Naibu Waziri Dkt. Kolimba aeleza nia ya Wizara katika kuendeleza Chuo cha Diplomasia 

Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa imejipanga kuhakikisha Chuo cha Diplomasia kinaboresha huduma zake za utoaji elimu na mafunzo ya masuala ya Diplomasia ili kukidhi mahitaji ya Watanzania katika taaluma hiyo.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alipofanya ziara katika Chuo hicho kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Mhe. Kolimba alisema kwamba Chuo cha Diplomasia ambacho kilianzishwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji ni miongoni mwa vyuo vilivyojipatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi kwa kutoa  mafunzo katika masuala ya Diplomasia na hivyo Wizara haina budi kuhakikisha inaendelea kukiboresha ili kuhakikisha kinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Mhe. Dkt. Susan alisema kuwa, miongoni mwa masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika maboresho hayo ni pamoja na miundombinu ya Chuo kwa maana ya kuongeza majengo, vifaa vya kisasa vya kufundishia, maabara za kisasa za lugha, maktaba na kuongeza Wakufunzi.

Aidha, Mhe. Kolimba aliueleza Uongozi wa Chuo hicho kuwa ni vema vipaumbele katika kukiletea chuo maendeleo vikaainishwa ikiwa ni pamoja na kuonyesha mikakati ya kila changamoto ili kupata suluhisho la haraka la changamoto hizo.

“Ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya na tunaahidi kuwa pamoja nanyi wakati wote ili kuhakikisha Chuo chetu kinafikia viwango vinavyostahili” alisema Mhe. Kolimba.

Vilevile alieleza kuwa ni vema Chuo kikaimarisha ushirikiano na Vyuo vingine vya ndani na nje kwa kuainisha maeneo muhimu ya ushirikiano yenye faida kwa pande zote. Pia alikitaka Chuo kuwa na mikakati itakayokiwezesha Chuo hicho kuweza kujiendesha kibiashara  kama vyuo vingine nchini na kuacha utegemezi mkubwa katika bajeti ya Serikali.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri Chuoni hapo, Mkurugenzi wa Chuo hicho, Balozi Mohammed Maundi alisema kuwa Chuo hicho kinaendelea kuboresha maeneo mbalimbali ya Chuo hicho ikiwemo kuanzishwa kwa Kozi ya Shahada mwaka 2015 na tayari chuo kimepata michoro ya majengo kwa Chuo kipya wanachotarajia kukijenga na sasa kinachohitajika ni fedha ili kukamilisha mpango huo ambao kwa kiasi kikubwa utamaliza changamoto zinazokikabili Chuo.

Chuo cha Diplomasia (CFR) ni chuo kilichoanzishwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji mwaka 1978. Chuo kimekuwa kikitoa elimu katika ngazi ya Cheti, Diploma, Shahada na Shahada ya Juu. 

-Mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.