Follow by Email

Tuesday, February 23, 2016

Matangazo ya moja kwa moja kutokea Ngorongoro Crater yarushwa nchiniMarekani

Mwakilishi wa Serikali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika Wizara hiyo, Bw. Herman Keraryo akizungumza na  Waandishi wa Habari kuelezea umuhimu  wa matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa na Shirika la Utangazaji la ABC News la nchini Marekani kutokea Bonde la Ngorongoro katika kuitangaza Tanzania.  Shirika la ABC News kupitia kipindi chake mashuhuri cha Good Morning America kimerusha matangazo yake ya moja kwa moja kutokea Bonde la Ngorongoro tarehe 23 Februari, 2016.
Mkurugenzi  wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi Devotha Mdachi naye akifafanua jambo kwa waandishi

Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi naye akifafanua kwa waandishi wa habari namna Tanzania na Mamlaka hiyo itakavyofaidika na matangazo hayo ya moja kwa moja yaliyorushwa na ABC News.
Bi. Mindi Kasiga,  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa naye akizungumza na waandishi wa habari
Mhandisi Mkuu wa mawasiliano na matangazo  wa Shirika la  ABC News, Bi Farhoun akiwaeleza Wakurugenzi na Waandishi wa Habari namna matangazo hayo yatakavyorushwa kwa kutumia Teknolojia ya hali ya juu na kwamba wamejipanga kuwaonesha Wamarekani Wanyama  na  Jamii za Wamasai wanaoishi katika Bonde hilo. 
Bi. Farhoun akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa Wakurugenzi
Bi. Farhoun akielezea namna baadhi ya vifaa na mitambo inavyofanya kazi
Wakurugenzi na Waandishi wa Habari wakiangalia namna matangazo yanavyorushwa moja kwa moja. Picha ya chini anayeonekana kwa mbali kwenye screen za  televisheni ni mtangazaji mashuhuri wa kipindi cha Good Morning America, Bi. Amy Robach akizungumza wakati wa matangazo hayo
Wakurugenzi wakisalimiana na sehemu nyingine ya Wataalam wa matangazo (crew) waliokuwa wamepiga kambi katikati ya Ngorongoro.
Baadhi ya Wanyama walioonekana katika kipindi cha moja kwa moja cha "Good Morning America"
Bi. Kasiga na Bw. Asante Melita kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa katika picha ya pamoja na Mtangazaji maarufu wa kipindi cha Good Morning America Bi. Amy Robach.
 ===================================================


Shirika la Utangazaji la ABC News la nchini Marekani limefanikiwa kurusha matangazo yake ya  moja kwa moja (live) kutokea Ngorongoro Crater kupitia kipindi chake maarufu cha “Good Morning America.”
Matangazo hayo ambayo yamerushwa tarehe 23 Februari, 2016 yanatarajiwa kutazamwa na watu milioni 5 Jijini New York na zaidi ya watu milioni 50 katika Marekani yote yanalenga kutangaza vivutio vya Utalii hapa nchini hususan Bonde la Ngorongoro pamoja na kuelezea jitihada za Serikali ya Tanzania katika uhifadhi wa mazingira na maliasili.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kutokea Bonde la Ngorongoro mara baada ya matangazo hayo kurushwa, Mwakilishi wa Serikali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Herman Keraryo alisema kuwa kuna  faida kubwa kwa matangazo hayo kurushwa nchini Marekani kwani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuleta Watalii hapa nchini. Pia matangazo hayo ni moja ya jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto  za kutangaza utalii ambapo njia hii iliyotumiwa na Shirika la ABC News ni nzuri kwani imefanikiwa kuwafikia watu wengi na kwa muda mfupi.
Bw. Keraryo ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutunza mazingira na Wanyamapori ambao wameendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii nchini.
“Kama mnavyojua utalii wa Tanzania bado unategemea wanyamapori kwa kiasi kikubwa pamoja na kuwa na vivutio vingine Kama vile  mambo ya kale lakini bado wanyamapori wanatangaza zaidi utalii wetu hivyo ni wajibu wetu kuendelea kuwatunza” alisema Bw. Keraryo.
Mbali na Bw. Keraryo wajumbe wengine kutoka Serikalini walioshuhudia urushwaji wa matangazo hayo ni  Bi. Devotha Mdachi, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dkt. Freddy Manongi, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Bi. Mindi Kasiga,  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu, Dkt. Manongi alisema kuwa anaishukuru na kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Ubalozi wake wa New York, Marekani kwa jitihada za kulishawishi na kufanikisha shirika hilo la utangazaji kuja nchini na kwamba ana imani utalii utaongezeka kufuatia  matangazo hayo. Alisema kuwa Tanzania imepata fursa nzuri ya kujitangaza bure kwa vile imekuwa ikutumia fedha nyingi kwa ajili ya kazi hiyo.
“Kitendo cha kuleta shirika la ABC News nchini kwa ajili ya kutangaza utalii ni cha kujivunia na pia ni fursa kubwa sana kwetu Watanzania. Hivyo napenda kuushukuru Ubalozi wetu New York kwani ninaamini kupitia matangazo haya tutafaidika sana na tunatarajia baada ya miezi michache kupata watalii wengi hususan hapa Ngorongoro” alieleza Dkt. Manongi.
Naye Bi. Kasiga, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje alieleza  jitihada zilizofanywa na Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania, New York pamoja na Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika kufanikisha matangazo hayo ya moja kwa moja. Aliongeza kwamba jitihada hizo  zitaendelea ikiwemo kuzitumia Balozi zetu zilizopo nje katika kuhakikisha vivutio vya utalii vya hapa nchini vinatangazwa duniani kote. Pia alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa    Mashirika mengine makubwa ya utangazaji duniani kuja nchini kutangaza vivutio hivyo.
Kwa upande wake Bi. Mdachi kutoka Bodi ya Utalii aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Tanzania ina Mabalozi wa hiari wa utalii watano nchini Marekani na kwamba matangazo hayo ya ABC News yatakuwa ni nyenzo mojawapo itakayotumiwa na mabalozi hao kuendelea kuitangaza Tanzania.
Naye Mwakilishi wa Shirika la ABC News  Bi. Farhoun aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwawezesha kufanikisha matangazo hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yataongeza watazamaji wa kituo chao kwa vile walihakikisha ni wanyama pekee wanaooneshwa kwenye matangazo hayo tangu mwanzo hadi mwisho.
Pia alisema kwamba wamevutiwa na hifadhi hiyo ya kipekee duniani na kuipongeza Tanzania kwa jitihada  za utunzaji wa mazingira hususan Bonde la Ngorongoro na hawajutii uamuzi wao wa kuichagua Ngorongoro kwa matangazo hayo.
-MWISHO-No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.