Follow by Email

Monday, December 21, 2015

WAZIRI WA MAMBO YA NJE AKAGUA UJENZI WA MAHAKAMA YA UMOJA WA MATAIFA JIJINI ARUSHA

Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akipata maelekezo ya ziada kuhusu ujenzi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa kwenye eneo la Lakilaki Jijini Arusha. Aneyetoa maelezo ni Afisa Mambo ya Nje na Mwansheria Bw. Elisha Suku. Kushoto kwa Waziri Mahiga ni Nd. Hamdouny Mansour, Katibu Tawala Msaidizi upande wa miundombinu. Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na ujumbe wake wakiangalia eneo la eka 16 ambapo majengo manne ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa yanajengwa. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Mwezi Aprili mwaka 2016.
 Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha Mhe. Wilson Nkhambaku baada ya kukagua eneo hilo na kuridhika na kasi ya ujenzi uliozingatia viwango vya kimataifa na vile vya Umoja we Mataifa. 

Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiwa na ujumbe wake baada ya kumaliza ukaguzi wa ujenzi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa jijini Arusha. 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI  
Serikali imeridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Masalia ya kesi za Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (Mechanism for International Criminal Tribunals (MICT) katika eneo la Lakilaki jijini Arusha, uliozinduliwa rasmi Julai mosi mwaka huu.

Akikagua ujenzi huo na kupokea taarifa kutoka kwa wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa majengo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga, amesisitiza kuwa ujenzi huo uzingatie viwango vya kimataifa ili kuhakikisha usalama wa nyaraka na ushahidi utakaohifadhiwa kwenye majengo hayo.

Alieleza kuwa ahadi ya Serikali iko palepale kushirikiana na Umoja wa Mataifa na kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu kama vile barabara, umeme na maji vinapatikana kwenye eneo hilo ambapo ujenzi unaendelea kwa kasi ya kuridhisha.

“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi huu kwani hii ilikua kazi yangu ya mwisho nilipokuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kule Umoja wa Mataifa, kutetea mahakama hii ijengwe hapa Arusha.

Akifafanua miundombinu iliyowekwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha, Katibu Tawala Msaidizi upande wa miundombinu Nd. Hamdouny Mansour alisema kuwa kwa upande wa upatikanaji wa maji, mkoa umefanikisha upatikanaji wa bomba maalum linaloleta maji kwenye eneo la ujenzi mojakwamoja bila kuathiri upatikanaji wa maji maeneo mengine pembezoni ili kutimiza azma hiyo ya Serikali.

Ujenzi huo wa Mahakama unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwa na majengo makuu manne; jengo la mahakama, jengo la uhifadhi wa nyaraka, jengo la ulinzi na jengo la ofisi za Umoja wa Mataifa. Msimamizi wa ujenzi wa Umoja wa Mataifa alielezea teknolojia ya kisasa itakayotumika kujenga jengo la kuhifanyia nyaraka haitahitaji kutumia viyoyozi ili kuhifadhi uhasilia wa nyaraka.

Kwa upande wa wakandarasi wanaojenga ambao ni kampuni kutoka India walielezea changamoto iliyopo kwenye ujenzi huo ni kutekeleza mpango wa kupanda mti aina ya mshita-acacia, utakaomaanisha haki ambayo kihistoria na jadi za kiafrika ilipatikana kwa mazungumzo kwenye mabaraza ya kijiji. Mti huo wa mshita au Tree of Justice utapandwa ndani katikati ya majengo hayo manne.

Serikali kupitia Hazina ilinunua eneo hilo la Lakilaki lenye ekari 431 na kukabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje ambapo limetengwa mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa taasisi mbalimbali za kimataifa. Taasisi nyingine zinazotarajiwa kujengwa kwenye eneo hilo ni African Union Advisory Board on Corruption (AUABC), African Institute of International Law (AIIL) na African Court on Human and Peoples' Rights (ACHPR).

Ujenzi wa majengo haya ya awali kwenye eneo la Lakilaki unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwakani. Ujenzi huo ulizinduliwa rasmi Julai mwaka huu wa 2015 na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

MWISHO.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,

20 Desemba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.