Follow by Email

Thursday, September 10, 2015

Waziri Membe azungumza na Mabalozi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe (Mb.), akizungumza na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, kuhusu nafasi na majukumu yao katika uchaguzi mkuu ujao, pamoja na jinsi Serikali ilivyojipanga kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani, huru na haki kwa vyama vyote.
Waheshimiwa Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini,wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe (Mb), wakati wa mkutano huo uliofanyika leo 10-09-2015 katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIC) jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kulia), Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Mambo ya Nje Balozi Celestine Mushy na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bi Rosemary Jairo (kushoto) wakimsikiliza Mheshimiwa Waziri.
Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Balozi Mohammed Maharage Juma, akiwatambulisha Mabalozi waliowasili nchini hivi karibuni ambao ni mara yao ya kwanza kuhudhuria Kikao cha aina hii, Wizara ya Mambo ya Nje. 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye pia alikua muendeshaji wa mkutano huo Bi. Mindi Kasiga, akiratibu kipindi cha maswali na majibu kwenye kikao hicho. 
Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini Mhe.Thamsanga Dennis Mseleku akiuliza swali katika mkutano huo.
Balozi wa Namibia hapa nchini Mhe. Japhet Isaack, akiuliza swali katika mkutano huo.
Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi, akiuliza swali katika mkutano huo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe (Mb), akijibu Maswali ya Waheshimiwa Mabalozi, kushoto kwa Mhe. Waziri ni Balozi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini Mhe. Juma Khalifan Mpango, Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Dkt. Mahadhi Juma Maalim (kulia kwa Mhe. Waziri) na Mwisho kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula.

Baadhi ya Mabalozi wakisikiliza majibu yanayotolewa na Mhe. Waziri Membe katika mkutano huo.

Mhasibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bw. Paulo Kabale (kulia), Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Wizara hiyo Bw. Abisai Mathias (katikati), na Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa wizara hiyo, Bw. Lucas Suka wakibadilishana mawazo baada ya mkutano kuisha.
 Balozi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini Mhe. Juma Khalfan Mpango, akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga, ambaye pia alikua muendeshaji wa mkutano huo.
 (pichani juu na chini) Baadhi ya  Mabalozi wakibadilishana mawazo na kusalimiana muda mfupi kabla ya mkutano huo kuanza. 
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Mambo ya Nje Balozi Celestine Mushy akibadilishana mawazo na baadhi ya Mabalozi.
Waheshimiwa Mabalozi wakibadilishana mawazo.
Mkutano ukiendelea
 Mkutano ukiendelea....
Mhe. Bernard Membe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo kumalizika.
Picha ya pamoja.
=======================
PICHA NA REUBEN MCHOME.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI  
Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wamehimizwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Hayo yamesemwa leo Septemba 10, 2015 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb), alipokutana na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa wa hapa nchini kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.Tanzania inatarajiwa kupokea waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kati ya 400 hadi 600 katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
“Tunatarajia kupokea waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi kati ya 400 na 600 kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), nchi za SADC, Jumuiya ya Ulaya (EU), Marekani, Uingereza, Norway na nchi nyingine. Hivyo, kupitia kwenu (Mabalozi) nawaomba muwasisitize wazingatie sheria na kanuni kama zilivyoainishwa na NEC na ZEC”. Waziri Membe alisikika akisema.
Waziri Membe alitaja baadhi ya kanuni ambazo waangalizi wa Kimataifa wanatakiwa kuzingatia kuwa ni pamoja na kutotoa taarifa kwenye vyombo vya habari wakati wa zoezi la uchaguzi linaendelea; kutoingilia zoezi la uchaguzi kwa maana ya kwamba, wanatakiwa kuwa waangalizi wa uchaguzi na sio kushiriki zoezi la uchaguzi; kuandaa ripoti baada ya uchaguzi na kuziwasilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Tume za Uchaguzi na mamlaka nyingine zinazohusika pamoja na kuainisha kwa maandishi kasoro zote zitakazojitokeza wakati wa zoezi hilo.
Aidha Mhe. Membe aliwahakikishia waangalizi wa uchaguzi kuwa Serikali itatota uhuru wa kutembelea majimbo yote ya uchaguzi bila kikwazo chochote kwani Serikali imejipanga kuendesha uchaguzi wa huru, haki na wazi, hivyo, haina chochote cha kuficha.
Kuhusu utulivu wakati wa uchaguzi, Waziri Membe aliongeza kuwa Serikali imejipanga vyema kuhakikisha uchaguzi wa Oktoba unafanyika kwa amani na utulivu, kama ilivyokuwa mila na desturi ya taifa la Tanzania. Alisisitiza kuwa vyombo vya usalama havitashiriki katika uchaguzi huo, isipokuwa vitahakikisha kuwa amani inakuwepo wakati wote wa uchaguzi. Pia usalama wa Watanzania kwa ujumla na mali zao utaimarishwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Membe alisema kuwa yeye kama mwana CCM ana uhakika chama chake kitaibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu ujao. Alisema haoni sababu ya CCM kushindwa kwani tofauti na vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo ni CCM pekee ndio chama kinachojivunia rekodi nzuri na madhubuti; mpango kazi unaoainisha shughuli zilizotekelezwa, zinazotekelezwa na zinazotarajiwa kutekelezwa pamoja na kuwa na mgombea bora wa nafasi ya Rais ukilinganisha na wagombea wengine wote nane wanaowania nafasi hiyo.
Waziri Membe alihitimisha mkutano wake kwa kulishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Washirika wengine wa maendeleo kwa kuchangia gharama za uchaguzi huo ambazo ni Shilingi bilioni 265 za Kitanzania.
Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Urais utafanyika nchini tarehe 25 Oktoba 2015 na Watanzania takriban milioni 23.7 wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo.   

MWISHO.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,


10 Septemba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.