Follow by Email

Monday, September 21, 2015

Balozi Mulamula aongoza maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Amani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akizungumza wakati akifungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Alliance Francaise, Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Septemba, 2015. Balozi Mulamula alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo


Sehemu ya wageni waalikwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani akiwemo Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini, Mhe. Thami Mseleku (mwenye suti ya kahawia) wakimsikiliza Balozi Mulamula (hayupo pichani) akihutubia wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez nae akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani. Bw. Rodriguez pia alisoma ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu maadhimisho hayo
Sehemu ya wageni waalikwa akiwemo Mama Shamim Khan ( wa kwanza kushoto) wakimsiliza Bw. Rodriguez (hayupo pichani)
Aliyekuwa Kamanda wa Kwanza wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Vikundi vya Uasi nchini DRC, Meja Jenerali James Mwakibolwa akiwasilisha mada kuhusu "Wajibu wa Raia katika Kutunza Amani" wakati wa maadhimisho hayo
Sehemu ya wageni waalikwa na waandaaji wa maadhimisho hayo  akiwemo Bi. Stela Vuzo (kushoto), Afisa  kutoka Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) wakimsikiliza Meja Jenerali Mwakibolwa (hayupo pichani)  
Bw. Baraka Chelego akiwasilisha mada kuhusu Vijana na Uchaguzi: Fursa na Changamoto wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani
Sehemu ya Maafisa wa Jeshi wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa.
Kikundi cha Burudani kikitumbuiza wakati wa maadhimisho hayo huku mgeni rasmi Balozi Mulamula na wajumbe wengine kwenye meza kuu wakifurahia
Wageni waalikwa wakikishangilia kikundi cha burudani ( hakipo pichani). Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Maulidah Hassan.
Mmoja wa Wanafunzi walioshiriki maadhimisho hayo akitoa ujumbe wake kuhusu umuhimu wa wazazi na wananchi kwa ujumla wenye sifa ya kupiga kura kutumia fursa hiyo kuchagua viongozi bora na kuzingatia amani. 
Balozi Mulamula akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya maadhimisho kumalizika
Balozi Mulamula akiagana na Bw. Alvaro
Balozi Mulamula akiagana na Kiongozi wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini ambaye pia ni Balozi wa DRC, Mhe. Juma Halfan Mpango.
Balozi Mulamula akiagana na Balozi Mseleku
Picha ya pamoja

Picha na Reginald Philip
==================================================

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula ametoa wito kwa Watanzania hususan vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuhakikisha amani iliyopo nchini inadumu.

Balozi Mulamula ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Alliance Française, Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamuala ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema kuwa kila Mtanzania anao wajibu wa kuchangia katika amani ya nchi huku akiwataka vijana ambao ni wengi kuhakikisha wanailinda amani iliyopo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na vizazi vijavyo.

Aliongeza kuwa fursa mbalimbali zikiwemo za uongozi na maisha bora hazipatikani  kwa kutumia nguvu wala vurugu na kuwataka vijana kujikita katika elimu, kufanya kazi kwa bidii  na uadilifu ili kutimiza ndoto zao ikiwemo kuwa viongozi wanaofaa hapo baadaye.

“Nahamasika kwamba vijana ambao ni asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania wanao wajibu mkubwa katika kulinda amani ya nchi yetu na ninaamini kuwa kijana anaweza kuwa kiongozi popote pale alipo na katika lolote analolifanya hivyo nawaomba mjijenge kwenye elimu, bidii katika kazi na kuwa waadilifu ili muwe viongozi bora baadaye”, alisema Balozi Mulamula.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015, Balozi Mulamula aliwahakikishia wananchi kuwa utakuwa wa amani na utulivu na kwamba wananchi wote wanao mchango mkubwa wa kuhakikisha amani inakuwepo wakati wote wa uchaguzi hadi hapo utakapokamilika. Vile vile alitoa rai kwa wananchi kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaowataka badala ya kuingia mitaani na kusababisha uvunjifu wa amani.

“Tumieni fursa iliyopo kuchagua viongozi bora. Kura yako ndio amani yako. Hivyo nawaomba wote wenye sifa mjitokeze kupiga kura wakati ukifika” alisisitiza Balozi Mulamula.

Awali akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa hapa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez alisema kuwa maadhimisho hayo ya 33 yanayobeba kauli mbiu isemayo Ushirikiano kwa ajili ya Amani; Utu kwa Wote yamefanyika wakati muafaka huku Tanzania ikijiandaa na uchaguzi mkuu na kuwataka vijana kuzingatia utawala wa sheria kwani kupanga ni kuchagua na kwamba  amani ndio kitu cha kwanza.

Aidha, katika ujumbe wake kwenye maadhimisho hayo uliosomwa na Bw. Rodriguez, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Kimoon ametoa wito kwa nchi zote duniani zinazokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani kuweka silaha chini na kurejea katika meza za mazungumzo. Aidha amezitaka nchi zote duniani kuwekeza kwa vijana ambao ndio wajenzi wa amani.

Akiwasilisha mada wakati wa maadhimisho hayo kuhusu  Wajibu wa Raia katika Kutunza Amani” Kamanda wa Kwanza wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa kupambana na Waasi huko DRC, Meja Jenerali, James Mwakibolwa alisema kuwa Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kutokana na juhudi za viongozi katika kuhakikisha amani inadumishwa na vilevile ushirikiano mkubwa wa wananchi kwa serikali yao.

Aidha, aliongeza kuwa ili amani iliyopo idumu ni muhimu kuwa na viongozi thabiti wanaotenda haki na pia elimu ya uraia itolewe kwa wananchi kwani amani ikitoweka kila mtu ataathirika kwa namna moja au nyingine.

“Nimekuwa kwenye maeneo ya vita na ukosefu wa amani na nimejifunza kuwa amani ikitoweka si rahisi kuirejesha. Hivyo nawasihi Watanzania wenzangu kudumisha amani kwa kutii sheria bila shuruti na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama pale inapohitajika ili nchi iendelee kuwa na amani na kukuza uchumi kwa maendeleo ya nchi” alisema Meja Jenerali Mwakibolwa.

Siku ya Kimataifa ya Amani huadhimishwa duniani kote  tarehe 21 Septemba kila mwaka ambapo maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Ushirikiano kwa ajili ya Amani; Utu kwa Wote”.  

-Mwisho-


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.