Follow by Email

Tuesday, August 25, 2015

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Balozi wa Algeria nchini.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Wizarani Balozi wa Algeria nchini, Mhe. Saad Belabeb alipofika kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria pamoja na kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu.
Balozi Mulamula akizungumza na Balozi Belabeb 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Zuhura Bundala kwa pamoja na Afisa Mambo ya Nje katika Idara hiyo wakifurahia jambio wakati wa mazungumzo kati ya Balozi Mulamula na Balozi Belabeb (hawapo pichani).
Balozi Mulamula akimsikiliza Balozi Belabeb
Mazungumzo yakiendelea

=================================

TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA USHIRIKIANO


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Tanzania na Algeria zitaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Balozi Mulamula ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa Algeria hapa nchini, Mhe. Saad Belabeb ambaye alimtembelea Wizarani leo kwa lengo la kumpongeza kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu.

Katika mazungumzo yao, Balozi Mulamula alisema kuwa Tanzania na Algeria zimekuwa na ushirikiano wa karibu na wa kihistoria tangu kipindi cha waasisi wa mataifa haya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais Ahmed Ben Bella na kwamba kuuimarisha ushirikiano huo ni kuendelea kuwaenzi.

Aliongeza kusema kuwa, katika kipindi chote Tanzania na Algeria zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya na katika masuala yanayohusu Bara la Afrika  chini ya Umoja wa Afrika.

“Tanzania itasimama na Algeria  pamoja na marafiki zetu wengine ili kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarika na unaendelea mbele zaidi,” alisisitiza Balozi Mulamula.

Kwa upande wake, Balozi Belabeb alimpongeza Balozi Mulamula kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo alimhakikishia ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwake.

Balozi Belabeb alisema kuwa Tanzania ni rafiki muhimu kwa Algeria na hilo linathibitishwa na ziara mbalimbali za viongozi wakuu wa nchi hizi ikiwemo ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete mapema mwaka huu nchini Algeria.

-Mwisho-


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.