Follow by Email

Thursday, June 18, 2015

Tanzania na India zinaweza kufanya vizuri zaidi kibiashara. Rais Kikwete

Na Ally Kondo, Delhi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa licha ya biashara kati ya Tanzania na India kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi endapo fursa zilizopo zitatumiwa ipasavyo.

Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa anaongea na Watendaji Wakuu wa Makampuni Makubwa ya India jijini Delhi leo tarehe 18 Juni 2015.

Rais Kikwete yupo nchini India kwa ziara ya Kitaifa ya siku nne iliyoanzia Siku ya Jumanne tarehe 17 Juni, 2015. Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na India, kuaga na kuishukuru India kwa misaada inayotoa tokea uhuru hadi sasa pamoja na kuisihi nchi hiyo kumpa ushirikiano Rais atakayechaguliwa mara uongozi wake utakapokamilika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba 2015.  

 Katika kikao hicho, Rais Kikwete alibainisha masuala mbalimbali ambayo yanaifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza kwa Mfanyabiashara anayetaka kuwekeza. Alieleza Serikali imefanyia mabadiliko makubwa Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali ambazo sasa zinaruhusu na kuimarisha Uchumi wa Soko. Kutokana na mabadiliko hayo, hakuna mwekezaji anayetakiwa kuwa na khohu ya kutaifishwa vitega uchumi vyake endapo atawekeza nchini Tanzania. Aliendelea kueleza kuwa Tanzania ni mwanachama wa kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara, hivyo, mwekezaji yeyote ana uhuru wa kufikisha suala lolote katika kituo hicho ili kupata haki yake, endapo atahisi amedhulumiwa.

 Aliwambia Wakuu hao waje kuwekeza nchini kwa sababu Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu wa hali ya juu kwa muda mrefu na aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kudumisha amani na utulivu huo.

 Sanjari na amani na utulivu, Tanzania imejaliwa kuwa na fursa lukuki za uwekezaji katika sekta za kilimo; viwanda vya uzalishaji; kilimo cha biashara; madini; utalii; uchukuzi na usafirishaji; miundombinu kama vile reli, barabara na bandari; afya; elimu na ujenzi wa makazi. 

Kwa upande wa kilimo, Rais Kikwete alisisitiza umuhimu wa kufanya uwekezaji katika pembejeo hususan, matrekta ili nchi iachane na matumizi ya jembe la mkono. Uzalishaji wa mbolea na dawa za kuua wadudu wanaoshambulia mazao, uzalishaji wa mbegu za kisasa pamoja na kujenga viwanda vya kusindika mazao, matunda na nyama.

Aidha, alisema jiografia ya Tanzania inatoa fursa nyingi za uwekezaji hususan katika uchukuzi na usafirishaji. Hii inatokana na nchi nyingi zinazopakana na Tanzania kuwa hazina bandari, hivyo bidhaa zao wanazoagiza au kusafirisha nje ya nchi zinategemea Bandari ya Dar es Salaam.

 Rais aliwambia wafanyabiashara hao kuwa, atakayekuja kuwekeza Tanzania ana uhakika wa soko kubwa la bidhaa zake ndani na nje ya  nchi. Alisema Tanzania ina fursa ya kuuza bidhaa zinazozalishwa nchini katika nchi za SADC na EAC bila kulipa ushuru. Nchi hizo kwa pamoja zinakadiriwa kuwa na soko la watu zaidi ya milioni 300. Aidha, nchi za EAC, SADC na COMESA zimekubaliana kuanzisha Eneo huru la Biashara ambalo litakuwa na soko la watu zaidi ya milioni 600.


Kwa upande wao, wafanyabiashra hao walivutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na walionesha dhamira ya kuwekeza, isipokuwa waliomba kuwepo na ushirikiano mzuri na serikali ili nia yao hiyo iweze kufanikiwa.No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.