Follow by Email

Tuesday, May 12, 2015

Waziri Membe aongoza Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa EAC


Waziri wa Mambo wa Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri  wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Burundi. Kulia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Richard Sezibera 

Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Watu Mashuhuri wanaofuatilia hali ya usalama nchini Burundi akijadili jambo na Mjumbe wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika kujadili hali nchini Burundi
Wajumbe mbalimbali wakimsikiliza Waziri Membe (hayupo pichani). 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Mhe. Louise Mushikiwabo  
 Mkurugenzi Msaidizi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi Bi. Victoria Mwakasege akinukuu yaliyokuwa yakijadiliwa kwenye mkutano.
Mkutano ukiendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe (Mb.) akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba kabla ya kuanza kwa  mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Mhe. Mushikiwabo (aliyetangulia), akiongozana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Amina Mohammed kuelekea kwenye ukumbi wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Picha na Reginald Philip.
==============================


Waziri Membe aongoza Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa EAC

Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) umefanyika leo Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuandaa agenda za Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi  wa Jumuiya  hiyo utakaofanyika tarehe 13 Mei, 2015 kujadili hali ya usalama nchini Burundi.

Akifungua Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alisema kuwa nchi ya Burundi inapita kwenye wakati mgumu wakati ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika hivi karibuni, hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameitisha mkutano huo wa dharura kujadili suala hilo na kutafuta ufumbuzi.

Waziri Membe alieleza kuwa, hali ya usalama nchini humo kwa sasa si shwari huku kukiwa na mfululizo wa maandamano ya wananchi na tayari zaidi ya Wakimbizi 50,000 wamekimbilia nchi  jirani ikiwemo Tanzania, Rwanda na Uganda.

“Lengo mojawapo la Jumuiya ya EAC ni kuhakikisha nchi zote wanachama zinakuwa katika hali ya amani, usalama na utulivu hivyo ni wakati muafaka mkutano huu kufanyika” alisisitiza Waziri Membe

Mhe. Membe aliongeza kuwa Mkutano huo ambao umehudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa EAC yaani Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda pamoja na mambo mengine utapokea na kujadili Taarifa ya Timu ya Watu Mashuhuri (Eminent Persons) walioteuliwa kufuatilia hali ya usalama nchini Burundi kutoka EAC na Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Aidha, Mkutano huo pia utapokea na kujadili Taarifa ya Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje waliotembelea Burundi hivi karibuni kwa ajili ya kupata taarifa za ndani za hali ilivyo nchini humo; Taarifa ya Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Eneo la Maziwa Makuu; Taarifa ya Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na Taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya Uenyekiti wa Rais Kikwete utafanyika Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2015 na utahudhuriwa na Marais wan chi wanachama wa Jumuiya hiyo akiwemo Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda, Mhe. Paul Kagame, Rais wa Rwanda, Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Burundi na Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya.

Viongozi wengine walioalikwa kushiriki Mkutano huo ni pamoja na Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Jacob Zuma ambaye atawakilishwa na Naibu Rais, Mhe. Cyril Ramaphosa, Kamishna wa Umoja wa Afrika, Mhe. Bibi Nkosazana Dlamini Zuma, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ukanda wa Maziwa Makuu, Bw. Said Djinnit; Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Prof. Ntumba Luaba, Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU).

-Mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.