Follow by Email

Thursday, April 16, 2015

Serikali kuwarudisha nchini Watanzania waliopo Yemen


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akiwasili katika Hoteli ya Hyatt ya mjini Muscat, Oman mara baada ya kuwasili nchini humo kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili. Wengine katika picha ni Balozi wa Tanzania, Oman, Mhe. Ali Ahmed Saleh (kulia) na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika Mashariki katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman, Bw. Abdullah bin Said al-Riyami. Wakati wa ziara hiyo Mhe. Membe alitangaza azma ya Serikali kuwarudisha nchini Wanzania waliopo Yemen kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo.
Mhe.  Membe akiwa na Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini Oman (kulia) na Bw. Abdullah bin Said al-Riyami, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afrika Mashariki wakimsikiliza Bw. Fahad al-Bulushi, Afisa Itifaki wa ujumbe wa Mhe. Membe mara baada ya kuwasili nchini Oman.
========================================= 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali kuwarudisha Watanzania waliopo Yemen

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ametangaza hatua ya Serikali kuwarudisha Watanzania waishio nchini Yemen, kufutia mapigano yanayoendelea nchini humu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Akizunguza na Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini Oman siku ya Alhamis tarehe 16 Aprili 2015, Waziri Membe amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi, wanarejea nyumbani salama.

Zoezi la kurudisha Watanzania hao lilianza siku chache zilizopita ambapo familia ya watu watano ilisaidiwa na kurudi nyumbani kupitia Oman, wakati zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha Watanzania likenddelea.

“Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko ya Yemen wanarejeshwa salama nyumbani mara moja” alisema Mhe. Membe.

Watanzania hao ambao wengi wao hadi sasa wameshafika kwenye miji midogo ya Sarfat na Al-Mazyouna kwenye mkoa wa Salala mpakani mwa Oman na Yemen, walituma maombi ya dharura (distress call) kwenye Ofisi za Ubalozi Oman, kuelezea mazingira ya hatari yanayowakabili, na kuomba kurudishwa nyumbani.

“Kulingana na maelekezo ya Waziri Membe, zoezi la kuwarejesha Watanzania limeanza. Nimewapeleka maafisa wa ubalozi kule Salala ni kilometa takriban elfu moja kutoka Muscut, ambapo watahakiki na kukabidhiwa Watanzania wote sitini na nne (64) na wataruhusiwa kuingia nchini Oman na kuelekea Tanzania” alimaliza Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini Oman.

Mgogoro wa Yemen unaoendelea baina ya maafisa wa polisi waaminifu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh, na makundi ya usalama yanayomuunga mkono rais wa sasa, Abed Rabbo Mansour Hadi, umeua mamia ya watu na kujerui maelfu.

Mhe. Membe ametoa rai kwa Watanzania wote wenye ndugu au jamaa nchini Yemen kuchukua tahadhari na kuwataarifu watafute msaada kupitia Ubalozini Muscat ili kujihakikishia usalama wao. Aidha ametoa tahadhari kwa Watanzania wanaotegemea kusafiri kwenda Yemen, kusitisha safari zao hadi hali ya usalama itakaporejea.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
16 Aprili, 2015


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.