Follow by Email

Friday, April 24, 2015

Membe awahimiza Watanzania kuchangamkia fursa Comoro


Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania akihutubia Kongomano la Biashara baina ya Tanzania na Comoro jijini Moroni Alhamis tarehe 23 Aprili 2015Membe awahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara na kuwekeza katika Visiwa vya Comoro

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.)  amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji Visiwani Comoro kwani uhusiano baina ya nchi hizi mbili umeimarika.

Mhe. Membe alitoa kauli hiyo wakati akilihutubia Kongamano la Biashara baina ya Tanzania na Comoro lililoandaliwa na Balozi za Tanzania na Comoro kwa kushirikiana na sekta binafsi za nchi hizo mbili jijini Moroni, Comoro tarehe 23 Aprili, 2015.

 “Watanzania tunathaminiwa sana hapa kutokana na mchango wetu mwaka 2008 tulipokikomboa Kisiwa cha Anjouan kutoka kwa Kanali Bacar. Sasa Serikali ya Umoja wa Visiwa vya Comoro imeimarika na uhusiano wetu umeshamiri. Wanatukaribisha sisi kwanza kushirikiana kibiashara, tuchangamkie fursa hii” alisema Waziri Membe.


Vilevile,  Mhe. Membe alisifu jitihada za ofisi za ubalozi wa nchi hizi mbili kwa kuitikia wito wa kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa kuandaa kongamano hilo la kihistoria.

“Rais Kikwete alipofanya ziara yake hapa mwaka 2014, aliahidi kukuza uhusiano wetu na kutoa wito wa kushirikiana kibiashara kwa manufaa ya nchi zetu. Nawapongeza sana Balozi Kilumanga na Balozi Fakih kwa kushirikiana na sekta binafsi na kutekeleza hili kwa wakati”alisema Waziri Membe, ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye kongamano hilo.

Kwa upande wake, Rais wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ikililou Dhoinine alisema kuwa yeye na Serikali yake wanathamini mchango mkubwa wa Tanzania kwa watu wa Comoro na hivyo atahakikisha uhusiano wetu unakua kwenye nyanja zote, Serikalini, sekta binafsi na hata baina ya watu wa nchi zote mbili.

Aidha, baada ya ufunguzi rasmi wa kongamano hilo, wafanyabiashara wa Tanzania walikutanishwa na wenzao wa Comoro kwenye makundi madogo madogo ili kuibua changamoto zinazokwaza biashara baina ya nchi hizo. Mikutano hiyo inatarajiwa kuibua njia bora zaidi ya kuwezesha biashara baina yao na kuimarisha uhusiano baina ya watu wake.

Akiwa jijini Moroni, Mhe. Membe alipata fursa ya kutembelea fukwe za bahari ambazo ni vivutio vikubwa vya utalii kwenye nchi hiyo ya visiwa akiwa na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Alanrif Said Hussane, Waziri wa Mambo ya Nje wa Visiwa vya Comoro.

Serikali ya Tanzania ilifungua ofisi zake za ubalozi mwaka 2013 ambapo inawakilishwa nchini humo na Mhe. Chabaka Kilumanga, Balozi wa Tanzania, mwenye makazi yake Moroni. Kwa upande wa Serikali ya Comoro ilifungua Ubalozi wake nchini Tanzania mwaka 2014 na inawakilishwa na Mhe. Ahamed El Badaoui Mohamed Fakih Balozi wa Comoro mwenye makazi yake Dar es salaam.

Kongamano hilo la siku mbili lililofunguliwa na Mhe. Ikililou Dhoinine, Rais wa Visiwa vya Comoro, lilifanyika kwenye ukumbi wa bunge jijini Moroni, mojawapo ya visiwa vitatu vinavyounda Umoja wa Visiwa vya Comoro, na kuhudhuriwa na wafanyabiashara takriban mia moja kutoka Tanzania. Visiwa vingine vinavyounda umoja huo wa Comoro ni Ngazija (Grand Comoro), Anjouan na Moheli huku mji mkuu ukiwa Moroni.

-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Sehemu ya Wafanyabiashara waliohudhuria Kongamano hilo wakimsikiliza Mhe. Membe 

 Picha ya meza kuu ya viongozi wa Tanzania na Comoro,

katikati ni Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dk. Ikililou Dhoinine, 
akiwa na Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa 
Kimataifa wa Tanzania na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye 
Kongomano la Biashara wakifuatilia ufunguzi.

 Rais wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dk. Ikililou Dhoinine, akizungumza na Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania wakati wa ufunguzi rasmi wa Kongamano la BIashara baina ya Tanzania na Comoro tarehe 23 Aprili 2015 Moroni.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.