Follow by Email

Friday, March 6, 2015

Wizara ya Mambo ya Nje yajipanga kutekeleza Sera ya Elimu n Mafunzo ya Mwaka 2014

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Prof.Sifuni Mchome akiwasilisha mada kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 kwa Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika warsha fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa  Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam tarehe 06 Machi, 2015.

Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Idara ya Asia na Austaralasia, Balozi Mbelwa Kairuki (katikati) na Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Sera na Mipango  Bw. Joachim Otaro wakifuatilia kwa makini warsha hiyo
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakimsikiliza Prof. Mchome ambaye hayupo pichani wakati akiwasilisha mada kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014
 Prof. Mchome akiendelea na mada yake
 Balozi Kairuki akichangia hoja kuhusu sera hiyo mpya ya elimu.
  Kaimu Mkureugenzi wa Idara ya Diaspora, Bibi Rosemary Jairo akiuliza swali wakati wa warsha hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,  Bi.Mindi Kasiga akitoa maoni yake kuhusu Sera ya Elimu.
Katibu wa Waziri wa Mambo ya Nje,  Bw.Thobias Makoba akiuliza swali juu ya sera mpya ya elimu
 Afisa Mambo ya Nje, Bw. Bartholomeo Jungu akitoa mchango wake kuhusu sera hiyo ya Elimu.

Picha na Ruben Mchome

================================


Wizara ya Mambo ya Nje yahamasishwa kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Sifuni Mchome ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuishirikisha Jumuiya ya Kikanda na Kimataifa kuisaidia Tanzania katika kutekeleza Sera mpya ya Elimu  na Mafunzo ya Mwaka 2014.

Prof. Mchome aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu Sera mpya ya Elimu kwa Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika warsha fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa  Julius Nyerere, Dar es Salaam hivi karibuni.

Prof. Mchome alisema kuwa ili kutekeleza Sera hii kikamilifu, upo umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambao kwa kutumia nafasi  ya ushirikiano na mataifa mbalimbali watahamasisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia hususan katika maabara, vitabu na wataalam wa masuala mbalimbali.

 “Lengo la kukutana nanyi leo ni kuwapatia mwelekeo wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ni kwa kutambua umuhimu wa Wizara hii katika kutekeleza Sera hiyo hususan katika nyanja za kikanda na kimataifa” alisema Prof. Mchome.

Aidha, aliongeza kuwa Sera hiyo ambayo ilianza kuandaliwa mwaka 2008 imejikita katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na inalenga kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu nchini ikiwemo uhaba wa walimu, vifaa na ithibati ambavyo kwa kiasi fulani vimechangia kushuka kwa ubora wa elimu na mafunzo hapa nchini.
Alifafanua kuwa, Sera hiyo pia inalenga  kuangalia viwango vya elimu vya Watanzania ili viendane na  vile vya kimataifa na kikanda na pia kutoa fursa sawa kwa watoto wote nchini kupata elimu na hatimaye kupata Watanzania wachapakazi, weledi na wenye vipaji kupitia elimu bora.

“Lengo kubwa la elimu ni kupata rasilimali watu yenye weledi, ujuzi na maarifa ya hali ya juu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu na hiyo ndiyo dhamira yetu, alisisitiza Prof. Mchome.

Akielezea masuala muhimu katika Sera hiyo, Prof. Mchome alisema kuwa kwa sasa Elimu ya Msingi itakuwa ni ya lazima na itatolewa bure kwa kipindi cha miaka 10 ikijumuisha Elimu ya Sekondari.

Pia, ufundishaji utaimarishwa hususan katika masomo ya hisabati, sayansi na teknolojia; kuhakikisha uwepo wa vifaa, nyenzo na zana muhimu za kufundishia; kuwa na kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo na kila mwanafunzi; kuimarisha ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na kuimarisha mbinu za ufundishaji.

Vile vile alisema kuwa bado kuna haja ya kuhamasisha Watanzania kujiunga na elimu ya juu na vyuo vya ufundi ambapo alisema kati ya Watanzania milioni 11.5 ambao ni wanafunzi wa ngazi mbalimbali ni asilimia 1 pekee wapo elimu ya juu ikiwemo elimu ya juu.

“Hadi sasa kuna jumla ya Watanzania milioni 11.5 ambao ni wanafunzi kwa ngazi mbalimbali.  Kati yao asilimia 71 wapo katika elimu ya msingi, asilimia 15 elimu ya Sekondari, asilimia 10 vyuo ya ufundi na nyinginezo, asilimia 1 elimu ya juu na ufundi na asilimia 0.7 Elimu ya Sekondari kwa kidato cha tano na sita,” alifafanua Prof. Mchome.

Kwa mujibu wa Prof. Mchome, Tanzania imeridhia Itifaki ya SADC (1997) kuhusu elimu na mafunzo inayozitaka nchi wanachama kuwa na elimumsingi ya lazima isiyopungua miaka tisa; Itifaki ya Dakar (2000) kuhusu Elimu kwa wote; Makubalinao ya Perth chini ya UNESCO (2007) kuhusu Elimu ya Sayansi na Teknolojia na mafunzo ya ufundi.

Awali akimkaribisha Prof. Mchome kuwasilisha mada yake, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Simba Yahya alisema kuwa anayo imani kubwa na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kwamba Wizara itashirikiana kikamilifu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutekeleza Sera hiyo.

Sera hiyo ilizinduliwa rasmi na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 13 Februari, 2015.


-Mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.