Follow by Email

Friday, March 27, 2015

Tanzania yaikabidhi Malawi msaada kwa ajili ya Wahanga wa mafuriko

Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Patrick Luciano Tsere (kulia) akikabidhi  Dawa za Binadamu na Mahindi  kwa Bw. Paul Chiunguzeni, Katibu Mkuu na pia Kamishna  anayeshughulikia masuala ya Maafa aktika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Malawi  ikiwa  ni sehemu ya msaada wa Tani 1,200 za Mahindi na Dawa za Binadamu zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa nchi hiyo kufuatia mafuriko makubwa yaliyoikumba nchi hiyo mwezi Januari 2015. 
Bw. Paul Chiunguzeni, Katibu Mkuu na pia Kamishna anayeshughulikia masuala ya Maafa katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Malawi akitoa hotuba ya shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa msaada huo wa Mahindi na Dawa za Binadamu.
Mhe. Balozi Tsere akiwa katika picha ya pamoja na Bw. Chiunguzeni. Wengine katika picha ni Mwambata wa Jeshi katika Ubalozi wa Malawi nchini Tanzania, Ufulu Kalino (kushoto) akifuatiwa na Kanali Rugeumbiza kutoka JWTZ ambaye alikuwa msimamizi wa zoezi la usafirishaji wa msaada huo kutoka Tanzania na Luteni Kanali B.B. Kisinda (wa tatu kulia) kutoka JWTZ ambaye alikuwa Kiongozi wa Msafara pamoja na Makamanda wa JWTZ.
Balozi Tsere akizungumza machache kabla ya kukabidhi msaada huo
Balozi Tsere akiteta jambo na Bw. Chiunguzeni.
Balozi Tsere akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa Habari kuhusu msaada uliotolewa na Serikali ya Tanzania.
=============================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA YAIKABIDHI MALAWI MSAADA KWA AJILI YA WAHANGA WA MAFURIKO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekabidhi Tani 1,200 za Mahindi na Dawa za Binadamu kwa Serikali ya Malawi ikiwa ni msaada wake kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea nchini humo mwezi Januari mwaka huu na kusababisha maafa makubwa.

Msaada huo umekabidhiwa hivi karibuni na Mhe. Patrick Luciano Tsere, Balozi wa Tanzania nchini Malawi kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kupokelewa na Katibu Mkuu na Kamishna wa Idara ya Maafa, Bw. Paul Chiunguzeni kwa niaba ya Serikali ya Malawi. Aidha, msafara uliopeleka msaada huo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), uliongozwa na  Luteni Kanali B.B. Kisinda.

Katika hotuba yake fupi wakati wa makabidhiano, Balozi Tsere alisema kwamba msaada huo umetolewa na Tanzania ikiwa ni agizo kutoka kwa  Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na kuguswa kwake na maafa hayo makubwa na pia kuitikia wito uliotolewa na Rais wa nchi hiyo Mhe. Prof. Arthur Bingu Mutharika kwa Jumuiya ya Kimataifa na watu mbalimbali wenye uwezo kutoa msaada kwa wahanga hao wa mafuriko.

Aidha,  Balozi  Tsere alieleza kwamba, Malawi na Tanzania ni nchi jirani, marafiki na zinazoshirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo majukwaa ya kimataifa kama vile Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa.

“Hivyo, kwa kutambua mahusiano hayo ya ujirani mwema na udugu baina ya nchi hizi na watu wake, Tanzania imeona ni jambo jema kushirikiana na jirani yake katika kupunguza athari za maafa hayo kwa wahanga hao kwani siyo vyema kuona jirani yako amepatwa na matatizo na kisha unakaa kimya” alisema Balozi Tsere.

Mhe. Tsere aliongeza kwamba ingawa msaada huo hautoshelezi kutatua tatizo hilo kabisa bado utaweza kusaidia wahanga hao na kupunguza tatizo lililopo kwa kiasi Fulani

Malawi ilikumbwa na mafuriko mwezi Januari mwaka huu. Mafuriko hayo yalisababisha maafa makubwa ikiwemo watu kupoteza maisha, nyumba kuharibiwa na mazao mashambani kusombwa na maji. Kwa hivi sasa familia katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko hayo hazina mahali pa kuishi na zinahitaji msaada wa chakula na kumekuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo hayo kama vile kipindupindu.


IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.

27 MACHI, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.