Follow by Email

Friday, March 13, 2015

Tanzania na China kuendeleza ushirikiano kwenye Sekta ya Uwekezaji na Viwanda

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha akizungumza wakati wa mkutano kati yake na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Balozi Liu Songtian  (hayupo pichani). Balozi Liu na ujumbe wake wapo nchini kwa ajili ya kufuatilia masuala ya uwekezaji na maendeleo ya viwanda Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika zilizochaguliwa na China kwa ajili ya kuwa mfano katika uwekezaji na maendeleo ya viwanda. Nchi zingine ni Ethiopia na Kenya. Wengine katika picha ni Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto kwa Bal. Gamaha), Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Mhe. Abdulrahman Shimbo (mwenye tai nyekundu), Balozi wa Tanzania nchini China na Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia (kulia), Mkurugenzi Mkuu wa EPZA.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Balozi Liu Songtian akizungumza wakati wa mkutano kati yake na Balozi Gamaha na ujumbe wake. Kulia ni Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Lu Yoqing
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Maalum ya Uwekezaji (EPZA), Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia akitoa mada kuhusu maeneo maalum ya uwekezaji yaliyopo nchini kwa ujumbe kutoka China unaoongozwa na Balozi Liu
Balozi Gamaha (katikati), akiwa pamoja na Balozi Shimbo (kushoto) na Balozi Kairuki (kulia) wakifuatilia mada iliyowasilishwa na Bw. Simbakalia (hayupo pichani)
Bw. Simbakalia akiendelea kutoa mada huku wajumbe kutoka China na Tanzania wakisikiliza
Balozi Liu akimkabidhi zawadi Balozi Gamaha
Balozi Mbelwa akimkabidhi Balozi Liu zawadi ya majani ya chai na kahawa ya Tanzania

Picha na Reginald Philip


=================================
Tanzania na China kuendeleza ushirikikiano katika Sekta ya Uwekezaji na Viwanda

Na Mwandishi Maalum

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Rajabu Gamaha amaihakikishia Serikali ya China kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu na kwamba inawaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo.

Balozi Gamaha aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana na ujumbe wa Maafisa kutoka China ukiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Balozi Liu Songtian. Ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya kikazi ya kufuatilia hatua zilizofikiwa na Serikali ya Tanzania juu ya uamuzi wa China wa kuzifanya nchi tatu za Afrika ikiwemo Tanzania kuwa mfano katika masuala ya Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda.

Balozi Gamaha alisema kuwa moja ya vigezo muhimu katika kuvutia wawekezaji ni pamoja na nchi kuwa na amani na utulivu wa kisiasa, kigezo ambacho Tanzania inacho na itaendelea kukilinda.

“Pamoja na Tanzania kujiandaa na Uchaguzi Mkuu mwaka huu, bado naamini hakuna kitu kinaweza kuvuruga amani iliyopo. Hivyo kitu muhimu ni kuendeleza ushirikiano wetu uliopo ambao ni wa kuheshimiana na kufaidishana na si wa kinyonyaji”, alisema Balozi Gamaha.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Balozi Songtian alisema kwamba China ina nia ya dhati ya kushirikiana na Tanzania katika masuala ya uwekezaji na maendeleo ya viwanda kwa kuzingatia ushirikiano uliopo pia ni miongoni mwa nchi nzuri zaidi kwa uwekezaji hapa duniani.

Aidha, Balozi Songtian aliongeza kuwa China ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya uwekezaji ikiwemo miundombinu, teknolojia na elimu ya ufundi ili hatimaye iendelee kiviwanda.

“Lengo langu ni kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha Tanzania na China zinafanikiwa katika Sekta ya Uwekezaji. Hivyo upo umuhimu mkubwa wa kusomesha watu wengi zaidi katika masuala ya Teknolojia na kuwa na Vyuo vingi zaidi vya Ufundi hapa Tanzania ili hatimaye tufanikiwe katika sekta ya Viwanda”, alisisitiza Balozi Songtian.

Aidha, Balozi Songtian alisema kuwa upo mpango wa Serikali ya China chini ya Mpango wa Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC) wa kuwaalika Wajasiriamali wachanga wapatao 500 kutoka Afrika kwenda nchini humo kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali yatakayowasaidia kuendeleza shughuli zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Eneo Maalum la Uwekezaji (EPZA), Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia ambaye aliwasilisha mada kuhusu Maeneo Maalum ya Uwekezaji hapa nchini, alisema kuwa Tanzania ni nchi ambayo ina fursa nyingi za uwekezaji na tayari kuna maeneo Maalum ya Uchumi yametengwa kwa kazi hiyo. Maeneo hayo ni pamoja na Bagamoyo, Dar es Salaam (Eneo la Benjamin William Mkapa) na Mtwara.

Pia, alieleza kuwa ili sekta ya uwekezaji nchini ikue na kufikia maendeleo ya viwanda ni muhimu kuimarisha rasimaliwatu, miundombinu ikiwemo barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, nishati ya umeme na sekta za kibenki.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika zilizochaguliwa na China kwa ajili ya kuwa mfano wa uwekezaji na maendeleo ya Viwanda. Nchi zingine ni Ethiopia na Kenya.


-Mwisho-


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.