Follow by Email

Sunday, November 2, 2014

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA LA VERNE WAPEWA SOMO KUHUSU USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA UMOJA WA MATAIFA

Bw. Noel Kaganda, Afisa katika Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York; na Bw. Suleiman Saleh, Afisa katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani, Washington D.C wakiwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha La Verne cha California waliotembelea Ubalozi wa Tanzania Washington D.C. kujifunza namna Tanzania inavyoshiriki katika Umoja wa Mataifa. Wanafunzi hao walipeperusha bendera ya Tanzania katika National Model United Nations (NMUN), iliyofanyika kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi 2 Novemba 2014, huko Washington D.C.

Bw. Kaganda, akiwasilisha mada kuhusu ushiriki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na vipaumbele vya nchi katika vyombo, kamati, kamisheni, bodi na mikutano ya nchi wanachama wa mikataba mbalimbali ya Umoja wa Mataifa. Programu ya NMUN inatoa fursa kwa wanafunzi wa vyuo zaidi ya 5000 kutoka pembe zote za dunia kuvaa kofia za Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia, ikiwemo migogoro, mabadiliko ya tabianchi, maafa, janga la umaskini, magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza na usawa na uwiano sawa wa kijinsia. Mafunzo haya kwa vitendo yanawajengea uelewa wa shughuli za Umoja wa Mataifa na  kuwapatia kionjo cha shughuli za kidiplomasia.

Washiriki wakifuatilia kwa makini mada inayowasilishwa. Pamoja na taarifa za kiuwakilishi katika Umoja wa Mataifa, wanafunzi hao walipata wasaa wa kufahamu misingi na mikakati ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania iliyojikita katika kuendeleza mahusiano ya kiuchumi na kibiashara na kukuza fursa za uwekezaji. Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani na Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa zinaendelea kupokea wanafunzi kutoka shule na vyuo mbalimbali vya Marekani ambavyo vimeonesha kiu ya kupata uelewa wa shughuli za kidiplomasia na habari za vivutio vya kiutalii vilivyopo nchini.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.