Follow by Email

Friday, October 10, 2014

Bunge kupigia kura Katiba Mpya ni Ishara ya kuimarika kwa Utawala Bora


Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Lilian Mukasa akisoma hotuba katika kikao cha Kamati ya Sita ya Umoja wa Mataifa jijini New York, MarekaniNa. Ally Kondo, New York

Serikali imesema kuwa mchakato wa kuandaa Katiba mpya ambayo imepitishwa na Bunge Maalum la Katiba hivi karibuni ni ishara ya wazi kuwa, Serikali imedhamiria kuongoza nchi kwa mujibu ya matakwa ya wananchi wake na kuzingatia Utawala wa Sheria.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bibi Lilian Mukasa alipokuwa anahutubia Kamati ya Sita ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani siku ya Ijumaa tarehe 10 Oktoba 2014.

Bibi Mukasa aliwambia wajumbe wa Kamati hiyo hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha kuwa huduma za kisheria ambazo kwa kawaida zina gharama kubwa, zinawafikia wananchi, hata wale wenye kipato cha chini.

Hatua hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya wanasheria wa Serikali, majaji, mahakimu, kujenga mahakama mpya na kuzifanyia ukarabati zile za zamani.

Aidha, Serikali imekuwa ikiboresha huduma za kiamahakama mara kwa mara na hivi sasa inakusudia kuanzisha mpango  utakaowawezesha wananchi kupata huduma za kisheria kupitia simu zao.

Hatua nyingine ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Mawakili wa kujitegemea pamoja na kuanzisha Shule ya Sheria ambayo inatoa mchango mkubwa katika sekta hiyo. Aidha, Serikali imekuwa na uataratibu wa kuzihamasisha Kampuni za uwakili zilizoimarika ili zisaidie kutoa msaada wa kisheria bure kwa watu masikini na makundi maalum,

Bibi Mukasa aliendelea kueleza kuwa Serikali inatambua nafasi ya mifumo ya sheria katika maendeleo ya nchi, uundaji wa Serikali, ulindaji wa kanuni za demokrasia kupitia Katiba, kulinda haki za binadamu na kutoa miongozo katika mgawanyo wa  rasiliamali. Hivyo, katika nchi yenye mfumo wa sheria unaotambulika na utawala wa sheria ulioimarika, maendeleo na demokrasia pia vinaimarika.

Alibainisha kuwa ili haki ipatikane lazima kila mtu katika jamii husika awe na nafasi sawa katika vyombo vya sheria. Vikwazo vyovyote kama vile kutojua kusoma na kuandika, umasikini, urasimu katika vyombo vya sheria, upungufu wa fedha na wataalamu wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka kwa wanasiasa pamoja na matajiri vyote vinakwamisha maendeleo.

Vikwazo hivi, pamoja na vingine ni changamoto kubwa katika nchi zinazoendelea. Katika jitihada za kukabiliana nazo, Serikali ya Tanzania imeanzisha  Kitengo cha Msaada wa Sheria katika Wizara ya Katiba na Sheria ambacho jukumu lake ni kuhakikisha kuwa kinatoa msaada wa sheria kwa wanaohitaji.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.