Follow by Email

Friday, May 9, 2014

Matukio mbalimbali ya ziara ya kikazi ya Mhe. Membe nchini Uturuki


Waziri Mkuu wa Uturuki, Mhe. Recep Tayyip Erdogan (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Mhe. Bernard K. Membe (Mb). mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Ankara, Uturuki tarehe 08 Mei, 2014.
Mazungumzo yanaendelea kati ya Waziri Mkuu wa Uturuki (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania. Mwingine katika picha ni Bibi Victoria Mwakasege, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Waziri Membe kulia akishikana mkono na Waziri Mkuu wa Uturuki mara baada ya viongozi hao kumaliza mazungumzo. 

Mazungumzo kati ya Waziri Membe na Waziri na Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki 

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa aliyevaa shati la njano kulia ukiwa katika mazungumzo na ujumbe wa Uturuki unaongozwa na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler wa tatu kutoka kushoto. 

Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard K. Membe akipokea zawadi kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki
Waziri Membe naye akimpa zawadi ya kinyago Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki 
Mhe. Membe na Naibu Waziri Mkuu wa Uturuki wakijadili suala baada ya zoezi la kukabidhiana zawadi kukamilika


Mazungumzo ya Waziri Membe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe wa tatu kutoka kushoto na ujumbe wakijadili masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano na Uutruki na ujumbe wa Uturuki unaonekana katika picha ya chini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Almet Dovutoglu wa pili kutoka kulia akiwa na ujumbe wake wakati wa mazungumzo na Mhe. Membe.

Mkutano na Waandishi wa Habari


Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mhe. Bernard K. Membe akihutubia Mkutano wa Waandishi wa Habari huku akimshika mkono Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mhe. Almet Dovutoglu
Waziri Membe akiendelea kuwahutubia waandishi wa habari hawapo pichani


Mapokezi ya Mhe. Membe nchini Uturuki


Waziri Membe akipeana mikono na watu waliofika Uwanja wa Ndege wa Ankara kumpokea
Waziri Membe kushoto akibadilishana mawazo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania katika Chumba cha Wageni Maalum kwenye Uwanja wa Ndege wa Ankara
Waziri Membe akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Italia ambaye pia anawakilisha Uturuki aliyekaa kushoto pamoja na Bw. Salvator Mbilinyi, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia aliyechutama wakibadilishana machache katika Chumba cha Wageni Maalum ndani ya Uwanja wa Ndege wa Ankara.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe akisalimiana na Naibu Meya wa jiji la Ankara ambaye naye alikuja Uwanja wa Ndege kumlaki


Naibu Meya wa jiji la Ankara aliyeketi kushoto akibadilishana mawazo na Mhe. Membe kabala ya kuondoka kutoka katika kiwanja hicho

Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Bw. Frank Muhina akiwa kazini kunukuu mambo mbalimbali kutoka kwa Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki. Na Ally Kondo, Uturuki

 WATURUKI WAHIMIZWA KUWEKEZA TANZANIA

Waturuki wenye mitaji wamehimizwa kuja Tanzania kuchangamkia fursa lukuki za uwekezaji zinazopatikana nchini. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Uturuki tarehe 08 na 09 Mei, 2014.
Katika ziara hiyo, Waziri Membe aliweza kuonana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Kitaifa wa Serikali ya Uturuki akiwemo Waziri Mkuu, Mhe. Recep Tayyip Erdogan; Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler; Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Ahmet Dovutoglu na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Lutfi Elgan.
Aidha, Mhe. Waziri na mwenyeji wake, Mhe. Dovutoglu walifanya mkutano wa pamoja na waandishi habari pamoja na kushiriki chakula cha mchana na wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki.  
Mhe. Waziri alieleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji ambazo hazijatumiwa ipasavyo, hivyo ni muda muafaka kwa Waturuki kuwekeza mitaji yao nchini Tanzania kwa faida ya pande zote.
Baadhi ya maeneo ambayo yatakuwa na faida kubwa endapo yatapata wawekezaji ni pamoja na sekta ya usafiri wa anga. Hivyo,  Mhe. Waziri alilihamasisha Shirika la Ndege la Uturuki kuangalia uwezekano wa kuingia ubia na Shirika la Ndege la Tanzania. “Endapo Shirika la Ndege la Tanzania litapata mwekezaji, likawa na ndege za kutosha na kwa sababu Tanzania imezunguukwa na nchi nyingi, wasafiri wengi wa nchi hizo, watatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuunganisha safari zao kwenda nchi za Ulaya”. Mhe. Membe alisikika akiwambia Viongozi wa Uturuki pamoja na wafanyabiashara wakubwa
Waziri Membe pia aliwahahakishia wawekezaji wa Uturuki watakaokuwa na dhamira ya kuwekeza nchini, kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) itatoa eneo maalum ili wawekezaji hao waweze kujenga viwanda vya uzalishaji. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda vya nguo, mbolea, gesi, zana za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji, umwagiliaji wa matone  pamoja na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, nyama na maziwa. Alisema endapo sekta hizo zitafanyiwa kazi ipasavyo basi ukuaji wa uchumi utaenda sambamba na ustawi wa maisha ya watu wa kawaida, kwa sababu sekta hizo zitaongeza ajira kwa maelfu ya vijana wa Tanzania.
Aliendelea kueleza kuwa ili ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki uendelee kuimarika, Serikali itatimiza ahadi yake ya kufungua Ubalozi nchini Uturuki katika mwaka wa Fedha 2014/2015.
Kwa upande wao, Viongozi wa Uturuki walimuhakikishia Mhe. Membe kuwa watawahamasisha wafanyabiashara wa Uturuki kuja kuwekeza Tanzania. Walisema kazi hiyo kwao ni nyepesi na wanahakika itapokelewa vizuri na jumuiya ya wafanyabiashara kwa sababu Tanzania mbali na kuwa na fursa nyingi, pia  ina utulivu wa kisiasa ambao ni kigezo muhimu katika uwekezaji. 
Katika hatua nyingine, Mhe. Membe aliishukuru Serikali ya Uturuki kwa kitendo chake cha kukubali wanamichezo 10 wa Tanzania kuweka kambi ya mafunzo kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Scotland mwezi wa Julai, 2014.
Sanjari na shukrani hizo, alimshukuru pia Balozi wa Uturuki nchini Tanzania na Mke wake kwa jitihada zao za kunusuru maisha ya watu wenye ualbino. Alisema uamuzi wao wa kujenga kijiji ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchukuwa watu wenye ualbino 500 kwa ajili ya kuwapa elimu na stadi nyingine za maisha ni mfano wa kuigwa na jamii ya wasamalia wema.  
Vile vile, Mhe. Waziri aliishukuru Uturuki kwa kulisaidia Shirika la Utangazaji la Taifa Tanzania (TBC)  kwa kulipa vifaa na teknolojia ya kisasa. Alisema kabla  ya msaada huo, TBC ilikuwa inafanya kazi katika mazingira magumu.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.