Follow by Email

Tuesday, May 6, 2014

Waziri Membe Ziarani UturukiTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Waziri wa Mambo   ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Uturuki kuanzia tarehe 07 – 09 Mei, 2014 kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Ahmet Davutoglo. Madhumuni ya ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki ambao umedumu kwa kipindi kirefu sasa.

Aidha, katika ziara hiyo Mhe. Membe na mwenyeji wake watajadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki hususan, katika maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika na Uturuki uliofanyika mwaka 2008. 

Maeneo hayo ni pamoja na biashara, uwekezaji, kilimo, mawasiliano, afya, elimu pamoja na amani na usalama.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri ataonana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Uturuki akiwemo mwenyeji wake, Mhe. Davutoglo; Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler; Waziri wa Uchukuzi, Usafiri wa Majini na Mawasiliano, Mhe. Lutfi Elvan; Waziri wa Nishati na Maliasili, Mhe. Tarrer Yildiz pamoja na kuongea na wafanyabiashara wa Uturuki.

Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri atafuatana na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Mamlaka ya Majengo Tanzania na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).

Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es salaam.
 6 Mei 2014.
  

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.