Follow by Email

Sunday, May 11, 2014

TANZIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa John M. Haule akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Juu ya Kifo cha aliyekuwa Balozi wa Mwalawi nchini Tanzania Hayati Mhe. Flossie Chidyaonga kilichotokea kwenye Hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa Tarehe 09 Mei 2014.

Bwa. John M. Haule akiendelea kuzungumza huku Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Vicent Kibwana (kushoto) akiyafuatilia kwa makini mazungumzo hayo na waandishi wa Habari (hawapo pichani)

Mazungumzo yakiendelea kati ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Picha na Reginald PhilipTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Serikali  imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Balozi wa Malawi hapa nchini Hayati Mhe. Flossie Gomile Chidyaonga kilichotokea juzi Ijumaa tarehe 09 Mei, 2014. Balozi Chidyaonga alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Aga Khan ya hapa Dar es Salaam.

 Balozi Flossie Chidyaonga alizaliwa tarehe 16 Juni, 1960 huko Blantyre nchini Malawi. Balozi Chidyaonga aliitumikia Serikali ya Malawi katika nyadhifa mbalimbali.  Kati ya mwaka 2006 hadi 2010 alikuwa Naibu Balozi wa Malawi nchini Uingereza na baadaye Kaimu Balozi hadi alipoteuliwa kuwa Balozi wa Malawi hapa Tanzanaia.

Siku ya Jumatatu, tarehe 05 Mei, 2014, Balozi Flossie Chidyaonga alishinda vizuri na kufanya shughuli zake kama kawaida. Hata hivyo, ilipofika usiku,  alijisikia vibaya na kupelekwa hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam ambapo alipatiwa Matibabu na kuwekwa mapunziko kuanzia saa 6 usiku hadi saa 12 asubuhi aliporuhusiwa na kupewa dawa za kutumia nyumbani. Balozi Chidyaonga aliendelea kutumia dawa hizo na hali kuonekana kuimarika hadi siku hiyo ya ijumaa, tarehe 09 Mei, 2014. Siku hiyo, aliamka vizuri hadi ilipofika majira ya saa 6 mchana, hali yake ilipobadilika na kukimbizwa tena hospitali ya Aga Khan ambapo alipokelewa Daktari alisema amekwishafariki. Sasa hivi, Mwili wa Marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Uchunguzi wa madaktari umeonesha kuwa marehemu amefariki kutokana na Mshipa Mkuu wa AORTA kuvimba na kupasuka kulikosababisha damu kukusanyika kwenye mfuko wa moyo na hivyo kufanya moyo ushindwe kufanya kazi yake.

Kesho tarehe 12 Mei, 2014 mwili wa Marehemu utachukuliwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kupelekwa kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambapo kutafanyika misa ya kumuombea Marehemu na kutoa heshima za mwisho kuanzia saa 4 asubuhi. Mwili wa Marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwenda Blantyre, Malawi siku ya Jumanne tarehe 13 Mei, 2014 na mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 14 Mei 2014 huko Blantyer, Malawi.

Katika kipindi chote alichokuwa mwakilishi wa Malawi hapa nchini, Balozi Chidyaonga alifanya kazi yake ya kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya nchi zetu mbili kwa umahiri wa hali ya juu. Siku zote alikuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano kwa Serikali na Mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Mungu aiweke roho ya marehemu Balozi Flossie Chidyaonga, mahali pema peponi.

AMEN

Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
 Dar Es Salaam, Tarehe 11 Mei, 2014

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.