Follow by Email

Sunday, November 10, 2013

Kenya yaipongeza Tanzania kwa msimamo wake kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akimtambulisha Mhe. Amina Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa pamoja Mkutano na Waandishi hao kuhusu pongezi za Serikali ya Kenya kwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa hivi karibuni kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika hotuba hiyo Mhe. Rais Kikwete alieleza msimamo wa Tanzania wa kutojitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Waandishi kutoka Vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani)
Mhe. Mohammed akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari huku Mhe. Membe akisikiliza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. John haule (wa pili kulia) akimsikiliza Mhe. Mohammed (hayupo pichani) alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu pongezi za Serikali ya Kenya kwa Tanzania. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa,Balozi Celestine Mushy (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Vincent Kibwana (wa pili kushoto) na Mjumbe kutoka Kenya.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu (katikati), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bw. Robert Kahendaguza (kushoto), Mjumbe kutoka Kenya na Bw. Mkumbwa Ally (mwenye koti jeusi), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wakati wa Mkutano kati ya Mhe. Membe na Mhe. Mohammed na Waandishi wa Habari (hawapo pichani)
Mhe. Membe akiagana na Mhe. Mohammed mara baada ya kukutana na Waandishi wa Habari.
Waandishi wa Habari kazini.

-----------------------------------------------------------------

KENYA YAIPONGEZA TANZANIA KWA MSIMAMO WAKE KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Serikali ya Kenya imetoa pongezi nyingi na shukrani kwa hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu nafasi ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika hotuba yake kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 7 Novemba, 2013 mjini Dodoma, Mhe. Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania haina nia wala mpango wa kujitoa katika Jumuiya hiyo pamoja na kwamba baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ikiwemo Kenya wamekuwa wakifanya vikao pasipo kuishirikisha Tanzania.

Pongezi za Kenya ambayo ni nchi ya kwanza kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuipongeza Tanzania, ziliwasilishwa nchini na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mhe. Bibi Amina Mohammed ambaye aliwasili nchini tarehe 08 Novemba, 2013 kama Mjumbe Maalum wa Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Katika mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari Mhe.Mohammed ambaye alisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alisema kuwa, Serikali ya Kenya imeridhika na hotuba iliyotolewa na Mhe. Rais Kikwete na wameisoma kwa makini na kuielewa kikamilifu na wanashukuru sana kwa hotuba hiyo kwani ni faraja kubwa kwao kuwa Tanzania bado ni mwananchama hai wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kenya imefurahi na kuridhika na hotuba ya Mhe. Rais Kikwete kwani Tanzania na Kenya zimetoka mbali pamoja. Pia ni waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo Kenya inaamini kuwa, tutaendelea kujenga Jumuiya hii kwa pamoja na kuendelea kuwa majirani wazuri ili kukuza uchumi kwa pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi wa nchi zetu”, alisema Mhe. Mohammed.

Mhe. Mohammed aliongeza kuwa anawashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono Mhe. Rais Kikwete kwa hotuba yake na hiyo inaonyesha umoja uliopo hapa nchini. “Tunawashukuru sana Watanzania kwa kumuunga mkono Rais Kikwete na hii inadhihirisha umoja na mshikamano uliopo baina ya Watanzania na Serikali yao,”aliongeza Bibi Mohammed.

Akizungumzia vikao vinavyoendelea kati ya nchi tatu za Kenya, Uganda na Rwanda, Mhe. Mohammed alifafanua kuwa, Tanzania haijatengwa na haiwezi kutengwa na kwamba masuala yote yanayojadiliwa katika vikao hivyo hayako nje ya Mkataba na Itifaki za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, Mhe. Mohammed alitumia pia fursa hiyo kuishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika  kuiunga mkono nchi yake katika kesi inayowakabili Rais na Makamu wa Rais wan chi hiyo huko Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Alieleza kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazounga mkono kesi hiyo iahirishwe hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa Viongozi hao kuwatumikia wananchi waliowachagua.

“Tunaishukuru sana Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono Kenya katika suala linalowakabili  viongozi wetu la  kushitakiwa ICC. Tumaamini kabisa kuwa hatuwezi kumaliza kesi hiyo wala kupata kibali (deferral) cha kesi hiyo kusogezwa mbele bila kuungwa mkono na nchi kama Tanzania” alisisitiza Mhe. Mohammed.

Awali akimkaribisha Bibi Mohammed kuzungumza na Waandishi wa Habari, Mhe. Membe alisema kuwa Serikali ya Tanzania imefurahishwa sana na ziara  ya Ujumbe huo mzito kutoka Kenya na Tanzania inazipokea kwa mikono miwili pongezi hizo za Kenya kwa Rais Kikwete na kwa Watanzania kwa ujumla. 

Kuhusu suala la viongozi wa Kenya kupelekwa ICC, Mhe. Membe alisema kuwa, Tanzania bado inaunga mkono maamuzi yaliyofikiwa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ya kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuahirisha kesi hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapa nafasi Viongozi hao kukamilisha baadhi ya mambo waliyojipangia kuyatekeleza kwa  nchi yao.

“Tunashukuru Mwendesha Mashitaka wa ICC ametoa tamko la dharura kwa kesi dhidi ya Rais Kenyatta kuanza kusikilizwa tarehe 5 Februari, 2014 badala ya tarehe 12 Desemba, 2013. Hata hivyo bado tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusogeza mbele kesi hiyo kwa mwaka mmoja hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa Viongozi hawa kuitumikia nchi yao kikamilifu kwani tunaamini katika kipindi hicho Serikali ya Kenya itakamilisha mengi” alisisitiza Mhe.  Membe.

Mhe. Membe aliongeza kuwa, kulingana na kauli ya Mhe. Mohammed alipozungumza nae, migogoro ya Kenya iliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 imetatuliwa kwa asilimia 75, ambapo baadhi  ya wahusika wamepatiwa ardhi, watuhumiwa wamepelekwa mahakamani na baadhi yao wamepewa fidia kutokana na madhara mbalimbali waliyoyapata. “Tanzania ipo pamoja na Kenya na ipo kuhakikisha Serikali hiyo inatawalika kwa kuwapa nafasi viongozi waliochaguliwa na wananchi kuongoza”, alisema Mhe. Membe.

Mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari kati ya Mhe. Membe na Mhe. Mohammed ulifanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule na Maafisa Waandamizi kutoka Serikali zote mbili.

-MWISHO-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.