Follow by Email

Monday, September 23, 2013

Mabalozi wetu wawe chachu ya kuwavuta wawekezaji
Mabalozi wetu wawe chachu ya kuwavuta wawekezaji


NA Maoni ya MHARIRI wa Gazeti la NIPASHE JUMAPILI,
22 Septemba 2013

Moja ya sera na mikakati ya kuinua uchumi wa nchi ni pamoja na kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na wa nje katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo itasaidia kuinua pato la taifa.

Ni rahisi zaidi kuwahamasisha wawekezaji wa ndani kwa vile wao nao ni sehemu ya jamii inayopambana na kujikwamua kutoka uchumi uliopo ambao ni tegemezi na unaoonekana kuwa dhaifu.

Kikwazo kinachojitokeza kwenye sera ya uwekezaji ni pamoja na umaskini wa wananchi wengi ambao kimsingi wanakosa mitaji mikubwa ya kuwafanya wawekeze katika sekta zinazohitaji mitaji mikubwa.

Wenye uwezo wa kuwekeza kwa mitaji inayoweza kuzalisha faida kubwa ni wageni wa nchi mbalimbali za duniani, ambako pia kuna wawakilishi wetu ambao ni mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwa masuala ya kidiplomasia.

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika ziara ya Marekani jijini Washington mwishoni mwa wiki hii, alisema kazi kubwa ya mabalozi wa Tanzania katika nchi za nje, ni kutetea maslahi na kuijengea marafiki katika nchi na maeneo ambako wanaiwakilisha nchi.

Rais alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila balozi wa Tanzania popote alipo, kuonyesha sura nzuri ya Tanzania, kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali na kutangaza nafasi nyingi za uwekezaji nchini.

Tanzania ina utajiri mkubwa wa utalii duniani, na mojawapo ya majukumu ya mabalozi wetu hao ni kutangaza utajiri huo, na hasa Marekani ambayo kwa sasa ndiyo nchi inayoongoza kwa kuleta watalii wengi nchini.

Rais Kikwete alipata fursa ya kuongea na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje, ilikuwa wakati alipozungumza kwenye hafla ya kutiwa saini kwa makubaliano kati ya Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula na mabalozi saba wa heshima ambao wataiwakilisha Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini Marekani.

Katika hafla hiyo, Rais Kikwete aliwaasa mabalozi hao wa heshima kuwa wanawajibika kulijenga jina la Tanzania katika maeneo yao, na kuitengenezea nchi yetu marafiki wa kila aina ikiwa ni pamoja na kuwavutia wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.

Watu wenye fedha na rasilimali za kuwekeza wanatakiwa waelimishwe kuwa Tanzania ni nchi nzuri kupeleka mitaji yao na kuwa mitaji hiyo itabakia kuwa salama. Rais aliwasisitizia mabalozi hao wa heshima kuwa pia watangaze utajiri mkubwa wa utalii uliopo nchini.

Tuna imani kubwa kuwa wito alioutoa Rais Kikwete kwa mabalozi wetu utatekelezwa kwa umakini, na pia tuaamini kuwa muda si mrefu Tanzania itanufaika na fedha za kigeni ambazo zitatokana na utalii pamoja na uwekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani.

Wapo wawekezaji wazalendo ambao baadhi wamewekeza katika sekta mbalimbali kama za hoteli za kitalii, mashamba ya mazao ya biashara na chakula, viwanda vidogo vidogo pamoja na katika masuala ya elimu. Bado jitihada zinatakiwa zifanyike ili kutanua wigo wa uwekezaji katika maeneo mengine ya kiuchumi.

Faida kubwa za uwekezaji si kwa ajili ya serikali kuongeza pato peke yake, bali hata ajira kwa vijana huongezeka. Uchumi wa nchi unapokua, unatoa pia fursa nyingi za ajira kwa vijana, na vijana ndiyo nguvu kazi inayotegemewa na nchi.

Mabalozi popote w alipo duniani, wanawajibu kutambua jukumu hili kubwa ambalo ni msingi mkubwa wa kuongeza pato la taifa na kuinua uchumi wa nchi. Wawekezaji wengi walioko nchini wamejikita katika uchimbaji wa madini, na sasa wameanza kuonyesha nia ya kuwekeza katika maliasili nyingine kama gesi asilia na mafuta.

Tunampongeza Rais Kikwete kwa kuwahamasisha mabalozi kuinadi Tanzania katika maeneo ya uwekezaji pamoja na utalii, tunaamini kasi ya kujituma kwa kazi hiyo ikifanyika kwa uadilifu, Tanzania itakuwa moja ya nchi itakayojizolea fedha nyingi za kigeni zitakazosaidia maendeleo ya taifa.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.