Follow by Email

Thursday, August 29, 2013

MAAZIMIO YA BARAZA LA KATIBA LA WIZARA
TAARIFA KWA UMMAMAAZIMIO YA BARAZA LA KATIBA LA 

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa lilikutana tarehe 26 Agosti, 2013 kujadili Rasimu ya Katiba mpya.  Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Mkutano ulifanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kufunguliwa na mgeni rasmi, Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Balozi wa Tanzania nchini Misri na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mabalozi Wastaafu, Wafanyakazi wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
  
Wizara iliamua kuunda Baraza la Katiba kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni Wizara ya Muungano; Rasimu ya Katiba imependekeza masuala ya Sera ya Nje kuendelea kuwa miongoni mwa masuala ya Muungano; na kuwa yako masuala yaliyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba ikiwemo mipaka, uraia na muundo wa muungano ambayo yanagusa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, liliazimia mapendekezo yafuatayo katika maeneo ya Mipaka, Muundo wa Jamhuri, Uraia wa Jamhuri na Sera ya Mambo ya Nje:- 

1)             Mipaka ya nchi iwekwe wazi mwishoni mwa Ibara ya 2 ili isomeke kama ifuatavyo: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na Zanzibar ikijumuisha ardhi, maziwa na sehemu yake ya bahari (Territorial Waters) pamoja na anga kwa mujibu wa sheria za kimataifa;

2)             Baraza pia lilipendekeza mabadiliko katika Muundo wa Jamhuri ya Muungano kwamba Muundo wa Serikali Mbili uliopo, uendelee na kuboreshwa kwa kuwekewa mifumo imara ya kisheria itakayoakisi maslahi ya pande zote mbili za Muungano ili kupunguza changamoto na manung’uniko kutoka kwa wadau wa Muungano. 

3)             Kuhusu suala la uraia katika Jamhuri ya Muungano; Baraza lilipendekeza kuwa suala la uraia wa nchi mbili kwa Mtanzania wa kuzaliwa litamkwe Kikatiba na Raia huyo asipoteze uraia wake wa kuzaliwa kwa sababu ya kupata uraia wa nchi nyingine. Uraia wa nchi mbili utatoa fursa kwa Taifa letu kufaidika kimaendeleo kutokana na kutumia rasilimali za Watanzania walioko nje ya nchi;

4)             Kuhusu Uraia, Ibara ya 55(4) inayozungumzia kumpa uraia wa kuzaliwa mtoto atakayekutwa ndani ya mipaka ya nchi yetu, ambaye wazazi wake hawajulikani ni raia wa nchi gani,  Baraza linapendekeza “….Uraia huo utasitishwa endapo uraia wa asili (wa nchi nyingine) wa mtoto huyo utagundulika na kuthibitishwa pasipo na shaka au kama itagundulika kuwa ulifanyika udanganyifu wa kumtupa kwa makusudi mtoto huyo kwa nia ya kupata uraia wa Jamhuri ya Muungano.”

5)             Kuhusu Uraia wa kuandikishwa, Ibara ya 56(2), mtu aliyefunga ndoa na raia wa Jamhuri ya Muungano anaweza kutuma maombi ya kuandikishwa kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano baada ya kuomba uraia wa Muda wa kuishi nchini kama mwanafamilia wa ndoa (dependant) mpaka ndoa iwe imedumu kwa miaka kadhaa (miaka itamkwe na sheria)”.

6)             Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje; Baraza linapendekeza mabadiliko katika Ibara ya 12 ya rasimu kwamba Misingi (Principles) ya Sera ya Mambo ya Nje ijumuishwe badala ya majukumu ya Wizara kwa kuwa majukumu hubadilika na nyakati. Aidha, Katiba ilielekeze Bunge litunge Sheria itakayosimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

7)             Kuhusu Ibara ya 39 (3) inayohusu raia wa Tanzania kutokupelekwa nje ya nchi kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote bila ya ridhaa yake, Baraza linapendekeza Kifungu hicho kifutwe, kwa sababu kuna ugumu wa haki inayotajwa kwenye Kipengele hiki kutekelezeka bila kuathiri wajibu ya kimataifa wa nchi (international obligations) katika makosa ya jinai, kwa kuwa ni vigumu sana kupata ridhaa ya mtuhumiwa kuhojiwa kwa makosa aliyoyatenda au anayotuhumiwa kuyatenda.


WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

28 AGOSTI, 2013

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.