Follow by Email

Monday, July 8, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI220px-Coat of arms of Tanzania.svg f1f71TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kikao cha 15 cha Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (The SADC Ministerial Committee of the Organ on Politics, Defence and Security Cooperation), kitafanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam tarehe 10-13 Julai, 2013.

Kikao hicho kinachohusisha sekta ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kitatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu na Maofisa Waandamizi tarehe 10 na 11 Julai, 2013 na kitahudhuriwa na Nchi zote wanachama wa SADC isipokuwa Madagascar, ambayo imesimamishwa uanachama.

Mawaziri watakutana tarehe 13 Julai, 2013, chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Mheshimiwa Bernard Kamilius Membe (Mb).

Pamoja na mambo mengine, Kikao hicho kitajadili hali ya kisiasa Kusini mwa Afrika, uimarishaji wa Demokrasia, Utekelezaji wa  Mpango Mkakati wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, Mikataba ya ushirikiano katika Nyanja za Ulinzi na Usalama pamoja na Ushirikiano baina ya SADC na Umoja wa Ulaya (EU).

Washiriki wa vikao vya Maofisa Waandamizi wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam tarehe 9 Julai, 2013 wakati Mawaziri watawasili tarehe 12 Julai, 2013.  

Kikao hicho cha Mawaziri kitafuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi, utakaofanyika Lilongwe, Malawi, tarehe 17-18, Agosti, 2013, ambao utahitimisha Uenyekiti wa Tanzania wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, ulioanza tangu Agosti, 2012.  Mwenyekiti anayefuata wa Asasi hiyo atakuwa Namibia wakati Uwenyekiti wa SADC utachukuliwa na Malawi.

Nchi Wanachama wa SADC ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Sheli Sheli, Afrika Kusini, Swaziland, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.


IMETOLEWA NA:


WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM

8 JULAI,  2013


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.