Follow by Email

Tuesday, March 5, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mkuu wa Denmark, Mhe. Helle Thorning-Schmidt anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 05 Machi, 2013 kwa ziara ya kitaifa ya siku nne. Ziara hiyo ya Mhe. Thorning-Schmidt inafuatia mwaliko wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Thorning-Schmidt ambaye anatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 05 Machi, 2013 saa 12:45 jioni atapokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Akiwa hapa nchini, Mhe. Thorning-Schmidt atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Kikwete tarehe 06 Machi 2013 na baadaye kwa pamoja na Mhe. Rais Kikwete watakutana na Waandishi wa Habari, Ikulu, Dar es Salaam.

Aidha, siku hiyo hiyo ya tarehe 06 Machi 2013, Mhe. Thorning-Schmidt atatembelea Meli ya Kijeshi ya Denmark ya Iver Huitfeldt ambayo imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam  tarehe 1 Machi, 2013 na kuzungumza na Mabaharia katika meli hiyo.

Mhe. Thorning-Schmidt pia anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam siku hiyo ya tarehe 6 Machi, 2013 kuhusu Elimu na Maendeleo kabla ya kushiriki Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu, Dar es Salaam.

Mhe. Thorning-Schmidt ataondoka Dar es Salaam tarehe 7 Machi, 2013 kuelekea Arusha ambako ataendelea na ziara yake kwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Kijiji cha Wamaasai cha Lepurko na kukutana na Waandishi wa Habari.

Akiendelea na ziara yake Mkoani Arusha tarehe 8 Machi, 2013 Mhe. Thorning-Schmidt atatembelea Shamba la Kahawa linalomilikiwa na Bw. Christian Jespen lililoko pembezoni mwa Bonde la Ngorongoro na baadaye anatarajiwa kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Mbulu.

Aidha siku hiyo hiyo, Mhe. Thorning-Schmidt anatarajiwa kutembelea Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo atakuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dkt. Richard Sezibera. Mhe. Thorning-Schmidt pia atatembelea Kituo cha Mafunzo kinachofadhiliwa na Serikali ya Denmark cha Mellemfolkeligt Samvirkes, MS-TCDC kilichopo Usa River.

Mhe. Thorning-Schmidt anatarajiwa kuondoka hapa nchini tarehe 08 Machi  2013 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kurejea nchini kwake Denmark.


IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
04 MACHI, 2013No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.