Follow by Email

Tuesday, February 19, 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Mwai Kibaki anatarajia kuwasili nchini tarehe 20 Februari, 2013 kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili. Ziara hiyo ya Mhe. Rais Kibaki inafuatia mwaliko wa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, ziara ya Mhe. Rais Kibaki inafanyika kufuatia ziara ya Mhe. Rais Kikwete nchini Kenya mwezi Septemba, 2012.

Mhe. Rais Kibaki ambaye anatarajiwa kuwasili katika  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 20 Februari, 2013 saa 9.00 alasiri, atapokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Akiwa hapa nchini, Mhe. Rais Kibaki atafanya mazungumzo rasmi na Mhe. Rais Kikwete tarehe 20 Februari 2013 kabla ya kushiriki katika Dhifa ya Kitaifa itakayoandaliwa kwa heshima yake na Mhe. Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.

Mhe. Rais Kibaki anatarajiwa pia kukutana na  Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 21 Februari, 2013, kuzindua Barabara ya Mwai Kibaki na kutembelea Gereza Kuu la Ukonga Jijini Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali zinazolenga kuwarekebisha Wafungwa kuwa Raia wema na kuwapa mafunzo ya kiufundi kuwawezesha kujitegemea wanapomaliza vifungo vyao. Shughuli hizo ni pamoja na  ushonaji, useremala na kilimo cha kisasa.

Mhe. Rais Kibaki ataondoka nchini tarehe 21 Februari, 2013 kurejea nchini kwake.

IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
19 FEBRUARI, 2013
No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.